Familia

Wazazi wetu kama fursa kuipata pepo ya Allah Ta’ala

 Mtume mwingine baada yake. Rehema na amani pia ziwaendee pia jamaa zake na Maswahaba zake kwa ujumla.

Katika hadith sahihi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), Swahaba Abu Huraira (Allah amridhie) ameeleza kuwa Mtume wa Allah, (rehema na amani zimshukie) amesema: “Amepata hasara, kisha amepata hasara, kisha amepata hasara.” Ikasemwa: “Ni nani Ewe Mtume wa Allah?”, akasema: “Yule aliyewadiriki wazazi wake wawili, mmoja wao au wote wawili, katika uzee, kisha asiingie Peponi.” [Muslim].

Kutokana na hadith hii, ni wazi kuwa wazazi ni fursa. Ni fursa ya mtu kuingia peponi kwa kuwafanyia wema tu. Huu ni upendeleo wa hali ya juu alioutoa Allah Mtukufu kwetu wanadamu kwa sababu kuwaenzi wazazi lingepaswa kuwa jambo la asili tu. Wamekuzaa, wamekulea, wamekusomesha; kimantiki nawe ni wajibu wako kuwashukuru, kuwatii na kuwasaidia.

Lakini Allah kwa hekima na mapenzi yake akajaalia kuwa huko kuwafanyia wema ni ibada ambayo inatusogeza karibu na Pepo.

Kwa kuwa ni kuwatendea wema wazazi ni ibada, Allah Mtukufu ametoa maelekezo ya wazi kuhusu wajibu wa mtoto kwa mzazi pale aliposema: “Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata, ‘Ah!’ Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyonilea utotoni,” [Qur’an 17: 23-24].

Amri ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake wasimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu, iko wazi. Lakini kwa mujibu wa aya hiyo, baada ya kumpwekesha Allah katika ibada, kinachofuata kwa umuhimu ni kuwatendea wema wazazi ikijumuisha kuwaheshimu, kuwaenzi na kuwatumikia

Mwenyezi Mungu katika Aya hizi amekataza kusema ‘Ah’ kwa wazazi, sauti inayoonesha uchovu na kutokuwa tayari kufanya jukumu fulani. Pia, inaposemwa: “Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima”, inamanisha usiwapandishie sauti kwenye jambo walilolipenda madamu hawamuasi Mwenyezi Mungu, na tafuta lugha nzuri na maneno matamu ya kusema nao.

Na neno la Mwenyezi Mungu.

“Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma,” inamaanisha tuwajali wazazi, tuwatumikie, tuwalinde kama walivyotufanyia sisi tulipokuwa watoto wakituhangaikia kutulisha, kutuvisha, kutusafisha bila kusahau kukesha usiku kutubembeleza tulipokuwa tunaumwa.

Katika aya nyingine, Mwenyezi Mungu anasema:

“Na muabuduni Allah wala msimshirikishe na chochote na watendeeni wema wazazi wawili” (Qur’an 4:36). Vilevile, Mwenyezi Mungu anasema: “Sema, ‘Njooni nikusomeeni aliyokuharamishieni Mola wenu Mlezi. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema.’” [Qur’an, 6:151].

Katika hadith iliyopokewa na Abdullah bin Abbas (Allah awaridhie) ambaye amehadithia kuwa alimuuliza Mtume: “Ni amali gani inayopendwa zaidi na Allah?” ( Mtume akajibu): “Ni kuswali kwa wakati.” Akasema kisha nini. Mtume akasema: “Kuwatendea wema wazazi.” [Bukhari na Muslim].

Katika hadith nyingine ya Abdallah bin Amr bin al-As asmesimulia kuwa mtu mmoja alimuomba ruhusa Mtume (rehema za Allah na amani ya zimfikie) kushiriki katika Jihad. Mtume akamuuliza:

“Je, wazazi wako wapo hai?” Akasema: “Ndiyo.” Akamwambia: “Kapigane Jihadi kwa kuwatumikia wao. Nenda ukawatendee wema.” [Bukhari na Muslim].

Na hapa niseme kuwa kuwatendea wema wazazi kunajumuisha kuwaangalia katika mambo yao yote ya kimaisha. Inapotokea wazazi ni mafukara na ni wahitaji, ni wajibu kwa mtoto kuwahudumia kwa kuwapa chakula, mavazi na makazi lakini tusisahau mahitaji ya kihisia yaani kuwapenda, kukaa nao, kuwafariji na kuwafurahisha.

Baadhi ya watu katika zama hizi tunafanya kosa la kupeleka mahitaji ya kipesa lakini wenyewe hatuonekani. Hii haina tofauti tabia zilizoenea huko nchi za wazungu ambapo mzazi hupelekwa nyumba maalum za wazee akalelewe huko eti watoto wako bize kutafuta maisha.

Kama ilivyo fursa ukiwatii, ukiwaasi wazazi ni tiketi ya motoni

Allah amemuahidi adhabu kali mtu anayewaasi wazazi. Kuwaasi wazazi ni pamoja na kuwafanyia jambo linaloudhi na kuwakera, iwe kero kubwa au ndogo.

Kati ya mifano ya uasi kwa wazazi ni kuwatukana na kuwadhalilisha. Ama wenye hali mbaya zaidi ni wale waliofikia hata kuwapiga wazazi wao, na hii siyo jambo la kudhania bali ni matukio yanayotokea katika jamii.

Imepokewa kwenye Sahihi Bukhari na Muslim kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani ya zimfikie) akisema: “Hivi ni kwanini nisiwaeleze kuhusu dhambi kubwa kuliko zote? Swahaba wakasema: “Tuambie ewe Mjumbe wa Allah.” Akasema: “Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuwaasi wazazi wawili.”

Na kutoka kwa Abdallah bin Amr bin al-As kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ameeleza: “Miongoni mwa dhambi kubwa ni mtu kuwatukana wazazi wake.” Maswahaba wakasema: “Ewe Mjumbe wa Allah! Hivi mtu anaweza kuwatukana wazazi wake?” Akasema: “Ndiyo, Mtu akimtukana mzazi wa mwenzake naye atamtukania baba yake, na akimtukania mama yake naye atamtukania mama yake,” [Bukhari].

Imamu Bukhari na Muslim wamepokea kutoka kwa al-Mughira bin Shu’bah (Allah amridhie) akieleza: “ Mtume amesema, ‘Mwenyezi Mungu ameharamisha kuwafanyia utovu wa adabu wazazi, kuwaua wasichana, kuzuwia na kutaka kupewa, kuzungumza tusiyo na hakika nayo, kuuliza sana, na ubadhirifu wa mali.”

Imepokewa na Abdallah bin Umar kuwa Mtume (rehema za Allah na amani ya zimfikie) amesema: “Watu wa aina tatu Allah amewaharamishia pepo. Mtu aliyedumu katika ulevi, anayewaasi wazazi, na dayuthi (mtu anayeridhia uchafu kwa familia yake),” (Ahmad). Na imepokewa na Abi Umamah kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema: “Watu wa aina nne hawatatazamwa na Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Mtu anayewaasi wazazi, anayejisifu, anayedumu katika ulevi, na anayekana qadari ya Mwenyezi Mungu”. (At-Twabaraaniy).

Ole wao

Na mwisho, wema ni tunda linaloweza kuchumwa hapa duniani kabla ya akhera. Uchungu na madhara ya kuwaasi wazazi huanza hapa hapa duniani kabla ya akhera. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mambo mawili Allah huyalipa duniani, uonevu na kutowatii wazazi,” (Tirmidhi).

Hivyo tunasem ole wao watoto wengi wanaowaasi wazazi wao, wasioishi nao kwa, wasiowaheshimu na badala yake kuwatolea maneno mazito na machafu.

Na mwisho, wema ni tunda linaloweza kuchumwa hapa duniani kabla ya akhera. Uchungu na madhara ya kuwaasi wazazi huanza hapa hapa duniani kabla ya akhera. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mambo mawili Allah huyalipa duniani, uonevu na kutowatii wazazi,” (Tirmidhi).

Hivyo tunasem ole wao watoto wengi wanaowaasi wazazi wao, wasioishi nao kwa, wasiowaheshimu na badala yake kuwatolea maneno mazito na machafu.

Ole wao tena wanaofikia hadi hatua ya kuwatusi na kuwapiga, kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu ambaye amefaradhisha wazazi watendewe wema na ameharamisha kuwafanyia uasi, kuwapunguzia kero badala ya kuwafanyia ukatili na kuwatolea maneno ya hovyo.

Wote hao, ole wao, ole wao, ole wao

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button