Wapo ndugu, jamaa, marafiki zetu ambao wana tatizo la kutoka harufu kinywani. Tatizo hili linaweza kukukosesha raha katika maisha kwa sababu watu wa karibu yako watakuwa wanakaa mbali na wewe, na kukufanya ujihisi unanyanyapaliwa. Hii inaweza kukupelekea kuona aibu, kuwa na wasiwasi, kutojiamini na kupata msongo wa mawazo.
Mwanzo unaweza usijijue kuwa una tatizo hilo sababu huwezi kujisikia mwenyewe kuwa unanuka; na wanaosikia harufu wanaogopa kukwambia. Lakini siku moja atatokea mtani wako, mtoto mdogo au mwenza aliyeshinwda kuvumilia na kuamua kukwambia ukweli.
Hata usipoambiwa ukweli, unaweza kujua pia kwa kuona namna watu wanavyokaa mbali na wewe wakati wa mazungumzo maana wataalamu harufu ya mdomo inaweza kusikika hadi umbali wa mita nne.
Kwa mujibu wa jarida la afya la Medical News Today (MNT), mtu mmoja kati ya wanne (asilimia 25) wana tatizo la harufu mbaya ya kinywa mara kwa mara.
Hata hivyo, habari njema ni kuwa tatizo hilo linaweza kutibika. Lakini kabla ya kuzungumzia njia ya kutibu tatizo, kwanza tuangalie vyanzo vya tatizo hilo.
Sababu za tatizo la harufu mbaya ya kinywa
Kwa mujibu wa makala kadhaa nilizozisoma kutoka gazeti la Taifa Leo la Kenya, tovuti ya shirika la utangazaji la Uingereza BBC na blogu moja ya afya, Afya Class, chanzo kikuu cha tatizo la harufu mbaya ya kinywa ni usafi duni wa kinywa unaopelekea kubaki kwa masalia ya chakula kwenye meno na kuozea humo.
Vyanzo vingine vya tatizo hilo ni maambukizi ya aina fulani wa bakteria au fangasi kinywani au Fangasi wa Mdomoni na kwenye Ulimi, kuoza meno na maradhi ya ufizi.
Kichocheo kingine ni kushuka kiwango cha wanga mwilini, mathalan wakati wa mfungo wa Ramadhan, jambo ambalo hupelekea mwili kuyeyusha mafuta na kuchochea uzalishaji wa kemikali ya ‘ketones’ ambayo husababisha harufu kinywani.
Kingine kinachoweza kuchochea mdomo kunuka ni kinywa kuwa kikavu kwa kutokunywa maji ya kutosha, kuvuta bangi, kutumia baadhi ya dawa za hospitali au huenda hata za kienyeji.
Kula aina fulani za vyakula kama vitunguu maji, vitunguu saumu, baadhi ya viungo na samaki pia hupelekea tatizo hili, ingawa ikiwa hivyo hilo ni tatizo la muda ambao huondoka kirahisi kwa kupiga mswaki.
Njia ya kuondoa tatizo
Wataalamu wa meno wanasema kwamba unapaswa kupiga mswaki baada ya kula na kabla ya kulala, na kuondoa masalio ya chakula kwa kutumia uzi maalum wa hariri (floss) angalau mara moja kwa siku na pia usugue ulimi wako. Vilevile, unaweza kusukutua kwa dawa maalumu kila baada ya kusugua meno.
Mbali na kuzingatia usafi na afya ya kinywa, nenda kwa daktari ukaguliwe ili kujua ikiwa kuna meno yoyote yameharibika na yanaweza kusababisha harufu mbaya ya kinywa. Jitahidi kumuona daktari wa meno walau mara mbili kwa mwaka.
Kwa upande mwingine inatajwa kuwa kuna vyakula ambavyo ukila, vitakusaidia kukabiliana na tatizo hili vikiwemo mboga na matunda kama vile tangawizi, pea, mrihani, kotimiri karoti, tufaha, cheri, na machungwa. Vyakula hivi, kwa namna tofauti, husaidia kuondoa tatizo la harufu mbaya.
Unashauriwa kuosha kinywa chako na maji ya vuguvugu na chumvi kwani inaua vijidudu mdomoni mwako ambavyo vinaweza kusababisha harufu mbaya ya kinywa. Usiruhusu kinywa kukauka bali kunywa maji mengi hata ikiwa haujala chochote wakati wa mchana.
Kingine muhimu epuka kuvuta sigara au vileo vingine bali kula bigijii na pipi hasa zisizo na sukari
Ikiwa mtu amejaribu hatua hizi zote nyumbani na mdomo hauachi kunuka basi kuna haja ya kuonana na daktari kwani huenda kuna meno yameoza yanahitaji kuondolewa.
Usisukutue mdomo wako mara moja baada ya kupiga mswaki. Tema dawa ya mswaki ya ziada, lakini usisuuze kinywa chako mara moja. Ukisuuza mapema unaondoa Floride iliyomo ndani ya dawa jambo kabla haijafanya kazi yake.
Kuna wataalamu wanakosoa matumizi ya vijiti kuondoa chakula vilivyokwama kwenye meno kwa hoja kuwa vinaathiri ufizi na kuweza kusababisha maambukizi lakini hili haya siyo maoni ya wengi. Ila wataalamu wengi hushauri kutumia mswaki na uzi kuondoa mabaki ya chakula kwenye mianya ya meno. Namna ya kutumia uzi ni katikati ya meno yako na kuuvuta mbele na nyuma ili kuondoa mabaki ya vyakula yaliyokwama yanayosababisha harufu mbaya kinywani. Hata hivyo, uzi pia usitumike mara kwa mara.
Usafi wa kinywa kwa watoto
Inashauriwa kuwasaidia watoto kupiga mswaki hadi watakapotimiza umri wa miaka saba. Kwa kufanya hivyo, utakuwa unawafunza na kuwazoesha kupiga mswaki wenyewe