The Islamic Foundation yazindua kampeni kusaidia waathirika wa mafuriko
Siku chache baada ya taasisi ya The Islamic Foundation [TIF] kutoa shehena ya msaada wa chakula chenye thamani ya Sh 58.6 milioni kwa waathirika wa mafuriko mkoani Morogoro, taasisi hiyo imetangaza tena kampeni maalum ya kukusanya michango kusaidia zaidi waathirika kwa awamu ya pili.
Akitangaza kampeni hiyo kupitia kipindi maalumu klichorushwa moja kwa moja kupitia TV na Radio Imaan, Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Mussa Buluki amesema kampeni hiyo inatarajiwa kudumu kwa mwezi mmoja ambapo kiasi cha Sh 100 milioni zimelengwa kukusanywa.
Buluki alitoa wito kwa wapenda kheri popote walipo, nchini na nje ya nchi, kuchangia walichonacho ili kusaidia kurejesha furaha kwa wananchi waliopoteza mali zao.
Kwa mujibu wa Buluki, walipofikisha msaada wa awamu ya kwanza na kumkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, walishuhudia madhara makubwa yaliyowakuta wananchi na hivyo taasisi hiyo, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Aref Nahdi, iliamua kuomba wadau kusaidia zaidi jamii hiyo.
“Maafa yale yasikie kwa watu tu wakisimulia. Likikukuta ndio utajua athari zake. Kwa kweli, watu wengi wamepoteza michele yao ikiwa mashine, yaani wamelala tajiri wakaamka masikini. Inasikitisha sana,” alisema Buluki
Akifafanua zaidi, Buluki alisema kwa kutumia helikopta, waliweza kuona athari za mafuriko kwa upana wake.
“Mafuriko yameharibu sana mashamba ya wananchi, chakula kilichohifadhiwa maghalani, yameua mifugo na kubomoa nyumba za wananchi.”
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro (MUM), Bilal Majuva, amesema Uislamu unaelekeza watu kusaidiana, tena unawataka Waislamu kuwa wa kwanza kusaidia katika majanga
“Sio kwamba ni awamu ya kwanza, taasisi ilikwenda na kutoa msaada. Katika safari ile, walifanya tathmini nakuona athari ni kubwa. Waislamu wanapaswa kusaidia jamii kwa kadri wanavyoweza,” alisema.
Aliendelea: “Kusaidiana ni jambo muhimu. Aya na Hadith zinazungumzia kutoa zipo nyingi. Unapotoa, inaweza kuwa sababu ya kufunguliwa milango ya riziki yako, ukitoa kwa ajili ya wengine unaombewa dua na Malaika ili upewe badala,” alisema Majuva.
Michango kwa ajili ya kampeni hiyo inakusanywa kupitia namba ya Tigo pesa 0713627284, Airtel money 0785627284 na Mpesa 0767627284 zilizosajiliwa kwa jina la The Islamic Foundation.
Katika awamu ya kwanza, msaada uliopelekwa ulijumuisha tani 10 za mchele, mafuta ya kupikia lita 900, tambi kilo 100, katoni 27 za maji ya kunywa tani 27 ambapo mzigo wote huo una uzito wa tani 38 na kugharimu Sh 58,600,000.
Msaada ulipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, ambaye aliishukuru taasisi ya The Islamic Foundation kwa moyo wao na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano wa taasisi hiyo.
Taasisi ya The Islamic Foundation imekuwa na utaratibu wa muda mrefu wa kusaidia jamii zinazokumbwa na maafa na majanga mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa ibada ya kutoa sadaka na pia kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imeweka mkazo mkubwa katika kuinua maisha ya wananchi na kupambana na umaskini.