Muhimu ni kutubia, siyo kuzidisha maasi
Allah Mtukufu anatuambia: “…enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 39:53].
Katika aya hii tunajifunza kwamba Allah hutupa rehema zake zisizohesabika, na kupitia rehema zake hutusamehe makosa (madhambi) yetu. Kwa hiyo, ni kosa kwa muumini kukata tamaa ya kusamehewa madhambi yake, kwani kufanya hivyo kutapelekea ashindwe kufikia malengo ya kupata radhi za Allah na hatimae kuingia katika Pepo yake.
Tunavyotambua na ndivyo ilivyo, ni kwamba hakuna mkamilifu miongoni mwetu (Sote ni wakosaji), hivyo yapasa tuwe wanyenyekevu mbele ya Allah, tukiri makosa yetu kwake, tufanye toba na kumuomba msamaha.
Nafahamu kuwa, wapo baadhi yetu ambao hawaoni umuhimu wa kutubia madhambi yao kwa hoja kuwa kufanya madhambi ni sehemu ya udhaifu wa kibinadamu, hivyo hawawezi kutubia kwani wataendelea kufanya madhambi. Pia wapo wanaodhani kuwa Allah hawezi kuwasamehe, kwa kuwa wamefanya madhambi mengi makubwa (Al–Kabaair) na hivyo kuamua kuendelea kufanya madhambi.
Wale wanaodhani kuwa Allah hawezi kuwasamehe watambue kuwa wapo katika upotovu mkubwa. “Na ni nani anayekata tamaa na rehema za Mola wake Mlezi isipokuwa wale waliopotea.” [Qur’an, 15:56].
Ni hakika kwamba sisi wanadamu ni dhaifu, tuna upungufu mkubwa na makosa mengi,ndiyo maana Allah Mtukufu ametufungulia mlango wa toba na msamaha kama njia ya kujitakasa.
Ni wajibu kutubia kwa kila dhambi
Muislamu anapotenda dhambi ni lazima atubie haraka. Kufanya hivyo kunaonesha kuwa mtu huyo amedhamiria kumuomba Allah Aliyetukuka msamaha kikwelikweli. Umuhimu wa kuharakisha toba unakuja kwa sababu, shetani hupata nguvu pale binadamu anapoghafilika.
Ilivyo ni kwamba, kila binadamu ana mnon’gonezaji ambaye humshawishi kufanya vitendo visivyofaa. Mnong’onezaji huyo si mwingine bali ni Iblis (shetani aliyelaaniwa). Shetani hutia wasiwasi katika nyoyo za wanadamu na kuwapambia mawazo mabaya yenye madhara ili waweze kuyaamini, kuyasema au kuyafanyia kazi.
Sheikh Tantwawi (Allah amrehemu) ametaja kwamba wasiwasi ni maneno yaliyojificha ambayo shetani anayapenyeza ndani ya moyo wa binadamu ili atende dhambi. Kama vile ukweli unavyoweza kusemwa wazi bila ya kificho wala aibu, maneno hayo maovu ya shetani yanafichwa ili yasidhihirike.
Kwa mfano, shetani aliwaambia Adam na Hawa kwamba wamekatazwa kuusogelea mti ule kwa sababu Mwenyezi Mungu hakupenda wawe Malaika na kuishi milele. Namna bora ya kukabiliana na minong’ono kama hiyo ni kumtaja Allah ‘Azza Wajallah’ kwa usahihi na utukufu wake sanjari na kumlaani shetani.
Kwa mujibu wa Uislamu, kila kitendo anachofanya mwanadamu katika maisha yake ya hapa duniani kinaambatana na kiasi fulani cha usahaulifu. Hiyo ndiyo sababu ya wasiwasi wa shetani, Khannas (mwenye kurejea nyuma), anayetia wasiwasi katika vifua vya watu, [Rejea sura ya An–Nas, Qur’an 114:4–5].
Kwa mantiki hiyo, kila Muislamu anapaswa kuishi kwa kuzingatia umuhimu uliopo katika maisha ya sasa (Dunia) na yajayo (Akhera) kwa kushikamana na mambo ambayo Allah Mtukufu anayapenda na kuyaridhia.
Lakini wakati tunatafakari hayo, pia tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya hila na vitimbi vya Iblis, ambaye aliahidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa atawapoteza wanadamu kwa kuwatoa katika njia aitakayo Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kila mwanadamu ni mkosa; na kwa kulitambua hilo, Allah Mtukufu kwa rehema zake ametufungulia mlango wa toba na msamaha ikiwa tutahiyari kufanya hivyo. Ili tusamehewe, tunawajibika kufanya toba ya kweli, safi, na isiyokuwa na uongo ndani yake.
Kadhalika, hatupaswi kukata tamaa kwa sababu ya madhambi tuliyotenda kwani Allah hawapendi wenye kukata tamaa na rehema zake. Kushindwa kutubia ni kununua adhabu ya Allah Siku ya Kiyama.
Ni muhimu tutumie fursa ya uhai wetu katika kutekeleza ibada, kutubia na kumuomba Allah msamaha. Mwenye kutenda maasi pasina kutubia ni kama nguo iliyochafuka halafu isioshwe. Kwa msingi huo, kila anayetaka kuutakasa moyo wake hana budi kumrejea Allah kupitia mlango wa toba na Maghfira.