Darsa la wiki

Neema ya mvua na hukumu zake katika Uislamu

Katika Kitabu cha Allah (Qur’an Tukufu), kuna aya nyingi zinazozungumzia dalili au ishara za Allah katika ulimwengu huu. Mwanadamu anatakiwa atafakari na kuzingatia kupitia dalili na ishara zote za Allah – ziwe ni za kusomwa katika kitabu chake (Qur’an) au zile za kilimwengu zinazoonekana na kuonesha utukufu, nguvu na uwezo wake.

Kutafakari huku kutampa majibu ya maswali mengi ambayo yanaonesha nguvu ya Allah juu ya viumbe wake, udhaifu wa mwanadamu na hitajio lake kubwa kwa Mola wake. Miongoni mwa dalili au ishara hizo, ni kuwepo kwa mvua kama ilivyotajwa ndani ya Qur’an katika mfululizo wa ishara mbalimbali za Allah ulimwenguni.

Allah anasema: “Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kuhitilafiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Allah kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo ishara kwa watu wanaozingatia.” [Qur’an, 2:164].

Pia Allah anasema: “(Yeye ndiye) ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona, na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni, na ametawanya humo kila aina ya wanyama, na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasiokuwa Yeye! Lakini madhalimu wamo katika upotovu uliyo dhahiri.” [Qur’an, 31:10–11].

Kupitia tafakuri ya aya hizi, tunatambua kuwa mvua ni neema kubwa inayostawisha maisha ya viumbe. Allah huitumia mvua kuwaneemesha waja wake na kuwasaidia kupata mahitaji yao ya msingi katika maisha yao, kuwaondoshea ukame, kustawisha mazao na hutumika kunywa wao na mifugo yao.

Allah anasema: “Je! Mnayaona maji mnayokunywa? Je! Ni nyinyi mnayoyateremsha kutoka mawinguni, au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha? Tungelipenda tungeyafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru?” [Qur’an, 56:68–70].

Hata washirikina walikiri kuwa neema hii kubwa (mvua) inatoka kwa Allah ‘Azza Wajallah’. “Na ukiwauliza: Ni nani anayeteremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: ‘Ni Allah’. Sema: Alhamdulillahi, sifa njema zote ni za Allah. Bali wengi katika wao hawafahamu.” [Qur’an, 29:63].

Katika aya nyingine, Allah Mtukufu anasema: “Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapowafikishia awatakao katika waja wake, mara hao huwa na furaha. Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa. Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyoihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye Mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.” [Qur’an, 30:48–50].

Mvua hushuka kwa kipimo na makadirio maalumu

Hakuna awezaye kuishusha mvua, tena kwa wakati atakao isipokuwa Allah ‘Azza Wajallah’. Allah ndiye anayekadiria kila jambo na anateremsha mvua katika eneo atakalo na kwa kiwango atakacho (nyingi au chache).

Hili tunaliona kupitia tabia ya mvua, kwani Allah Ta’ala hukadiria inyeshe eneo fulani tu na sehemu nyingine ikakosekana, na wakati mwingine hunyesha kwa wingi mpaka ikaleta madhara sehemu fulani huku eneo lingine likiwa na ukame.

Anasema Mwenyezi Mungu: “Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu. Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayoyaweka.” [Qur’an, 15:21–22].

Ibn Mas’ud (Allah amridhie) aliwahi kusema: “Hakuna mwaka ambao mvua hunyesha kuliko mwaka mwingine isipokuwa Allah hugawa atakavyo, mwaka huu ikashuka hapa na mwakani ikashuka hapa.” [Tafsiri ya Qur’an Al–Qurtubi].

Pamoja na utaratibu huu, Allah anatutaka tuzingatie hatua zifuatazo:

Kwanza, kuchukua sababu katika yale tunayoyataka

Tumeeleza hapo awali kuwa, Allah ndiye anayekadiria kila jambo na ndiye anayeamua wapi na wakati gani mvua inyeshe na kwa kiwango gani.

Sisi wanadamu tumeelekezwa kutunza na kulinda vyanzo vinavyopelekea mvua kunyesha, kama vile misitu na mito kwani kila kitu Allah amekiwekea sababu zake kama anavyobainisha: “Allah ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo.” [Qur’an, 30:48].

Allah angelitaka angeiamuru mvua inyeshe vile atakavyo, lakini kwa hekima yake ameweka sababu mbalimbali zinazopelekea mvua inyeshe ili tujifunze kuwa kila kitu kina sababu zake na Allah ndiye msababishaji.

Pili, kutambua uwezo wa Allah

Kupitia mvua, tunashuhudia uhalisia wa uwezo wa Allah anaotuonesha kupitia viumbe vyake, ikiwemo kuteremsha mvua kutoka mbinguni, ambayo huotesha mimea na matunda yenye ladha tofauti:

“Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbalimbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbalimbali, na myeusi sana. Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinahitilafiana. Kwa hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.” [Qur’an, 35:27–28].

Allah anayafanya haya ili tupate msukumo wa kumpwekesha katika ibada zake: “Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliyekuumbeni nyinyi na wale waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu. (Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe riziki zenu. Basi msimfanyie Mwenyezi Mungu washirika hali ya kuwa mnajua.” [Qur’an, 2:21–22].

Tatu, kuingiza hofu katika nyoyo

Mvua, kwa upande mwingine Allah huitumia kama adhabu kwa waja kutokana na matendo maovu waliyofanya. Tusiitazame mvua kama neema tu, wakati mwingine huja kama adhabu kutokana na matendo yetu maovu.

Mafuriko ya mara kwa mara yanayozikumba nchi nyingi duniani na kusababisha majanga mbalimbali ikiwemo vifo na kubomoka kwa barabara, nyumba na madaraja ni ushahidi tosha kuwa Allah ana uwezo wa kuwaadhibu waja kwa aina mbalimbali ya adhabu kwa sababu ya matendo yao maovu.

Allaah aliwaangamiza watu wa Nabii Nuh kwa mvua kubwa, na akawaangamiza watu wa Nabii Lut kwa mvua ya mawe. “Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao wapo tuliyowapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walionyakuliwa na ukelele; na kati yao wapo tuliyowadidimiza katika ardhi; na kati yao wapo tuliowazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe nafsi zao.” [Qur’an, 29:40].

Allah anatueleza yale yaliyowasibu watu wa Nabii Nuh kwa kusema: “Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika. Na tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lililokadiriwa.” [Qur’an, 54:11–12].

Ama watu wa Nabii Hud, Allah aliwaangamiza kwa upepo mkali uliowajia kwa sura ya wingu la mvua, kama anavyobainisha: “Basi walipoliona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: ‘Wingu hili la kutunyeshea mvua! Kumbe sivyo, haya ni hayo mliyoyahimiza, upepo ambao ndani yake imo adhabu chungu.’” [Qur’an, 46:24].

Nne, kujiandaa na Siku ya malipo (Kiyama)

Allah anasema: “…na utaiona ardhi ni kame, lakini tunapoiteremshia maji hutikisika na kuumuka, na inaotesha mimea ya kila namna, mizuri ya kupendeza. Hayo ni kwa sababu Allah ndiye wa Haki, na kwamba yeye anahuisha wafu, na kwamba yeye juu ya kila kitu ni Muweza. Na kwamba Saa (Kiyama) itafika tu haina shaka ndani yake, na kwamba hakika Allah atawafufua waliomo makaburini.” [Qur’an, 22:5–7]. Kupitia mvua na namna ardhi iliyokufa inavyostawi na mimea kuota, tunajifunza namna Allah atakavyohuisha viumbe baada ya kufa Siku ya Kiyama.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button