Dhana ya Maendeleo
Neno “Maendeleo” (Development) hutukumiwa mno na wanasiasa wanapojinadi kwa wananchi. Wataalamu wa lugha ya Kiingereza wanasema neno “development” lilianza kutumika kuelezeya hatua za ukuaji wa viumbe katika miaka ya 1756 na baadaye likaanza kutumiwa na wachumi mwaka 1902.
Wachumi wanapozungumzia maendeleo wanamaanisha hali ya kupiga hatuwa za kiuchumi (state of economic advancement). Dhana hii ya maendeleo ya kiuchumi ilishika kasi zaidi baada ya Vita ya Pili ya Dunia, mijadala mingi ikafanyika hadi kuibuka somo liitwalo “development economics” ambalo hufunzwa katika vyuo vikuu mbali mbali ulimwenguni.
Kimsingi, kuna tafsiri nyingi na tofauti kutoka kwa wachumi kuhusiana na maana ya maendeleo. Wengi wetu tunahusisha na wingi wa fedha, hali nzuri ya maisha inayomwezesha mtu kuweza kujikimu bila hofu, kuwa na miundombinu imara kama vile barabara, maji, shule, umeme, vituo vya afya, ongezeko la ajira na kadhalika.
Mara nyingi viongozi na wanasiasa hukusudiya maana hii wanaposimama kujinadi majukwaani kuomba kura lakini ukweli ni kuwa haya ni sehemu moja tu ya maendeleo.
Maendeleo katika Uislamu
Wachumi wa Kiislamu wamefanya kazi kubwa katika kubainisha mtazamo wa Uislamu kuhusu maendeleo. Pamoja na mitazamo yao tofauti, wanachuoni hawa wanaona kuwa maendeleo ni lazima yajumuishe na yahusishe maeneo matatu muhimu na makubwa.
Eneo la kwanza ni uwepo wa fursa kwa wote na uhuru wa mtu binafsi kujiendeleza mwenyewe bila hofu wala upendeleo; pili, uwepo mazingira rafiki na bora yenye kumuwezesha mtu kufikiya malengo yake kipindi chote; na tatu uwepo wa hayo mawili kwa watu wote katika jamii husika.
Uislamu unaona kuwa eneo la kwanza ni muhimu zaidi na ndiyo chachu ya kupatikana maendeleo katika maeneo mengine. Uislamu unaona maendeleo yoyote yale lazima yamwezeshe mtu, ambaye ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu, kutoka katika umasikini wa kipato, fikra, imani na utamaduni na kueleya katika mabadiliko ambayo yatamwezesha kuwa na utajiri wa maarifa, wingi wa Imani kwa Muumba wake, muruwa mwema au tabia njema, fikra madhubuti za kielimu na kuyamudu mazingira yake muda wote.
Mtu lazima ajitambuwe, amtambuwe Mola wake na kutambuwa lengo la kuumbwa kwake na majukumu aliyopewa kama Khalifa wa Mwenyezi Mungu ambayo yana lengo la kumtowa katika upotofu na giza na kumwingiza katika nuru na uongofu. Kwa lugha ya Qur’an hawa ndiyo Ar Rashidun (walioongoka na walioendeleya)
Qur’an inayaona Maendeleo katika sura hii kuwa ni fadhila na neema kubwa, kama Mola alivyosema: “Lakini Mwenyezi Mungu amekupendezeeni Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na amekufanyeni muuchukie ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndiyo walioongoka (walioendeleya).Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima [49:7-8].
Mtume (rehema za Allah na amani zishukie) amesema: ” Amefaulu (katika kila jambo) yule ambaye ni Muislamu wa kweli aliyejisalimisha katika uongofu wa Mola wake, akaruzukiwa riziki yenye kumtosheleza mahitaji yake katika maisha ya Ulimwengu na Moyo wake ukawa wenye kushukuru na kukinai (usiokuwa na pupa na vitu au anasa za kilimwengu).”
Katika hadith nyingine, Mtume ametaja sifa nne mwenye nazo asiwe na hofu juu ya lolote alilolikosa ulimwenguni. Sifa hizo ni kwanza, uaminifu (juu ya amri za Mola wako na uliyoaminiwa na viumbe wenzio iwe siri, kazi, au mali); ya pili, ukweli (truthfulness) katika kauli na matendo; ya tatu, tabiya njema; na nne, kutosheka na chakula chako cha kila siku. [Musnad Ahmad]. Pamoja na hayo, Uislamu umempa jukumu mwanadamu aindeleze ardhi au ulimwengu na mazingira yanayomzunguka kwa kumtaka awe Mus-liheeena (mwenye kufanya wema) na siyo Mufsideena (mwenye kuharibu). Mola anasema “Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.” [28:77].
Maendeleo tuyatakayo
Dhana ya maendeleo ni mada pana mno ambayo makala haya haitoshi kuijadili kwa urefu wake. Hata hivyo, nakumbusha Waislamu na wasomaji kuwa Uislamu una mtazamo wake.
Mafundisho ya Uislamu yanalenga kumleteya maendeleo mwanadamu katika maeneo yake yote muhimu; kiimani, kiakili, kitabiya, kimali, kiafya na kimaisha na siyo kama nadharia za kimagharibi ambazo zimechukuwa baadhi ya mambo haya na kuyaacha mengine.
Hivyo maendeleo tuyakayo ni lazima yajikite katika ujumuifu mambo haya yote na katika kuelezea nukta hii nitatowa mifano miwili tu.
Maendeleo ya Kiimani.
Mwanadamu anahitaji maendeleo ya kiroho na kiimani (spiritual development). Kwa kuwa hili halimwepuki, anaweza kuishiya kuamini ipasavyo au kupoteya. Na haiwezekani bali ni ujuha uliofurutu ada kuwa mwanadamu anaweza kudai yeye hana anachoamini.
Je kama taifa, tunamjengeya imani gani mwananchi wa Tanzania? Ukitazama ilani za vyama mbalimbali, utaona vina ambayo vinayaamini. kwa mfano, kuna chama kinaamini katika usawa wa binadamu na kwamba kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake na kwama ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru. Huu ni mfano wa imani ya chama.
Je ni maendeleo gani ya kiimani tuyatakayo? Kama Waislamu, kiimani tunataka tuwe na taifa linaloamini uwepo wa Mwenyezi Mungu Mmoja na sifa zake tukufu.
Hivyo, kwa kuzingatia imani hii, wale wanaodai kutaka kutuleteya maendeleo hawatopuuza mchango wa wale ambao wanatukumbusha uwepo wa Mwenyezi Mungu na muongozo wake kama ambayo hali ilivyo sasa hivi.
Kwa mfano, kwa nini hamna walimu walioajiriwa kufundisha somo la dini mashuleni kama ilivyo masomo mengine? Je kwa nini serikali haitowi msaada katika kuchapa na kusambaza vitabu vya elimu ya dini mashuleni? Majibu mepesi tunayoweza kuyapata ni kuwa serikali haijihusishi na mambo ya dini au serikali haina dini.
Lakini, ikiwa kuyafanya haya ni kujihusisha na mambo ya dini kana kwamba dini ni jambo baya kabisa, basi ni wazi kuwa eneo hili la kimaendeleo limewachwa makusudi.
Sisi tunaona kuwa serikali kama ambavyo inasimamia taasisi zote za dini bila kuziingiliya uendeshaji wake, hivyo hivyo inayo nafasi ya kutowa machango wake katika eneo hili muhimu na nyeti la kimaendeleo. Hivyo, iwapo wanasiasa wetu wanadai na kuamini Mungu yupo, hatuna budi kuendeleza imani hiyo kwa kiwango cha kuthamini walimu wa masomo ya dini katika nchi yetu.
Maendeleo ya Kitabia
Mwanadamu ana tabia zake za kimaumbile na zile anazojifunza kila siku na kuamuwa kuchukuwa na kuziacha. Maendeleo yenye kubadilisha tabiya mbovu kuelekeya katika tabia nzuri (moral development) ni kipaumbele kinachostahiki.
Je kama taifa tunafunza, kusimamiya na kuhimiza tabiya gani kwa wananchi wetu bila kujali mwanachama wa chama au la? Nchi yetu imeshuhudiya na inaendeleya kushuhudiya mmomonyoko wa maadili mema kwa vijana na wazee wetu.
Kuporomoka kwa maadili ni matokeo ya kutofunza na kusimamia maadili ipasavyo katika ngazo zote. Watu wafunzwe tabia ya ukweli, uaminifu, uchapakazi, kufanya mambo kwa ajili Mungu n.k.
Kama taifa, tumewaachia viongozi wa dini, wazazi au mtu binafsi kufunza maadili, lakini je inatosha? Jawabu ni haitoshi. Kama ambavyo tunafunza masomo ya uraia (civic education), mazoezi (physical education) n.k, vilevile tunahitaji kuwekeza katika kufunza maadili mema kama taifa na kuyasimamia.
Haitoshi kuwa na watu ambao wanasema: “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko” na kisha wanapoenda kinyume chake kwa kusema uongo hadharani na kuleta fitina ikawa taifa halichukuwi hatuwa zozote.
Wamesema wanchuoni wa tabia kuwa ” Kuwepo na kubaki kwa Taifa / Umma wowote ule kunategemeya uwepo wa maadili yake. Iwapo maadili yake yataondoka, basi na umma huo utakuwa umeondoka hata kama vizazi vingalipo.”
Hivyo, maendeleo tuyatakayo yawe jumuishi kwa watu wote, yenye mtazamo mpana na mtambuka ambayo yatajikita kumbadilisha mwanadamu mwenyewe kuwa kiumbe bora kama Mungu anavyotaka awe na kuimarisha mazingira yake na kustawisha jamii yote kwa ujumla.
Tunataka maendeleo ambayo yanatowa fursa kwa wote kujiendeleza kwa uhuru bila uonevu wala kupendelewa au kukandamizwa. Maendeleo ambayo utu wetu unaheshimiwa, unalindwa, unaimarishwa na kuendelezwa na siyo kudunishwa, kupuuzwa au kudumazwa.