Darsa la wiki

Ushauri kwa wanaokaribia kufa!

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya wiki iliyopita, tulimalizia na kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema za Allah na amani zimshukie) aliyoitoa siku tatu kabla ya kufariki: “Asife yeyote miongoni mwenu isipokuwa awe na maoni mazuri kuhusu Mwenyezi Mungu.” [Sahih Muslim].

Kauli hii inasisitiza kwamba ni muhimu kwa yule anayeteseka kwa ugonjwa, na zaidi kwa yule anayekaribia kufa kuwa na fikra chanya kuhusu Mwenyezi Mungu na hali hiyo. Sasa endelea na sehemu inayofuata…

Anas bin Malik (Allah amridhie) amesimulia kwamba, Mtume alikwenda kumtembelea kijana mmoja wakati alipokuwa mahututi kitandani na kumuuliza anajisikiaje. Yule kijana akajibu: “Namtumainia Allah, lakini naogopa kwa sababu ya madhambi yangu.”

 Mtume akamshauri: “Hisia hizi mbili (hofu na matumaini) huwa hazikai pamoja ndani ya moyo wa mtu katika hali kama hii, isipokuwa Allah atampa kile anachotumainia na kumuweka salama na kile anachohofia.” [Tirmidhi].

Kutekeleza haki za Allah na haki za waja wake

Maamrisho na makatazo ndani ya Qur’an tukufu na hadith za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), mara nyingi husisitiza haki mbili muhimu (haki za Allah na haki za waja wake), ambazo tunapaswa kuzitekeleza kadri tunavyoweza kabla ya kuondoka hapa duniani: “Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na yatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanaojigamba.” [Qur’an, 4:36].

“Sema: Njooni nikusomeeni aliyokuharamishieni Mola wenu. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema. Wala msiwaue watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayoonekana, na yaliyofichikana. Wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha kuiua ila kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini.” [Qur’an, 6:151].

“Wala msizikaribie mali za yatima ila kwa njia ya wema kabisa, mpaka afikie (umri wa) utu uzima. Na timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu. Sisi hatumkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni. Hayo amekuusieni ili mpate kukumbuka.” [Qur’an, 6:152].

“Na Mola wako ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa maneno ya heshima.” [Qur’an, 17:23]. “Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako.” [Qur’an, 17:38].

Ingawa haki za Allah ‘Azza wa Jallah’ kwa waja wake zina umuhimu mkubwa na zinastahili zaidi kutekelezwa, baadhi ya wanazuoni wameweka umuhimu mkubwa katika kutimiza haki za waja, kwa kuwa kuzipuuza husababisha kuwajibika katika maisha yajayo, wakati kila mmoja atakapokuwa na mahitaji makubwa, na sarafu pekee ya kufidia hayo ni amali zake, [Sahih Bukhari na Sahihi Muslim].

 Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani zimshukie) ametaja kwamba aliyefilisika zaidi ni yule atakayevuliwa mali yake halisi, yaani matendo yake mema Siku ya Hukumu wakati wa kulipa haki na kufidia makosa aliyowafanyia wengine alipokuwa duniani, [Sahih Muslim].

Kwa hiyo, yule anayekaribia kufa, ambaye ataiacha hii dunia akiwa na amali zake tu, ni muhimu zaidi kufikiria haki zifuatazo:

Haki za Allah

Kuhusiana na haki za Allah, wajibu wowote ambao haukutekelezwa kwake na unaweza kufidiwa, basi unapaswa kutekelezwa haraka. Kama hukutoa zaka basi inapaswa kutolewa, na kama hukutekeleza ibada ya Hijja kwa sababu ya uzembe, basi kumtafuta mtu wa kufanya Hijja kwa niaba yako (Hajj badal) inashauriwa zaidi.

Na kama hili halitekelezeki, kama ilivyo kwa maeneo mengine ya kughafilika, mfano kuacha ibada ya sala kwa uzembe au kutumbukia kwenye makatazo, basi toba ya kweli na kuomba msamaha ndiyo njia bora zaidi.

Mwenyezi Mungu atapokea toba ya mja wake maadam roho yake haijafika kooni: “Hakika toba inayokubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndiyo Mwenyezi Mungu huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hekima.” [Qur’an, 4:17]. Wanazuoni wa mwanzo wa tafsiri ya Qur’ an wamekubaliana kwamba, maneno: “Wakatubia kwa haraka,” yaliyotumika katika aya hii, maana yake ni kutubia kabla ya kufa.

Haki zako na za watu wengine

Asili ya wanadamu na muingiliano wetu wa kijamii, una maana kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kusema au kutenda kwa makusudi au kwa bahati mbaya kwa kuwaumiza na kuwakwaza wengine. Hadith iliyorejewa hapo juu kuhusiana na mtu aliyefilisika, ambaye siku ya Kiyama atalipa fidia kwa amali zake, inajumuisha yule ambaye amesababisha majeraha ya maneno au ya kimwili.

Zingatia kwamba wakati wa kuwaomba msamaha wengine kutokana na majeraha uliyoyasababisha, siyo sharti kwako kutaja kitendo ulichokifanya au kauli uliyoitoa, iwapo kufanya hivyo kutaleta maumivu zaidi.

Badala yake inatosha tu kutumia kauli za jumla kama: “Tafadhali nisamehe kama nimekuumiza au kukukwaza kwa namna yoyote ile.” Mbadala wa kauli hii, ikiwa unahisi kutaja matukio maalumu itasaidia kuponya majeraha ya zamani – basi bila shaka inashauriwa kufanya hivyo.

Na kama haiwezekani kutafuta msamaha wao, basi inatosha kwetu kuwaombea dua, kuwasifu na kuwazungumza vizuri kwa watu baada ya vifo vyao.

Haki zako za kifedha na za wengine

Madeni yoyote ya marehemu ambayo hayajalipwa yanapaswa kulipwa kwa waliowakopesha. Kama hili haliwezekani, basi mipango lazima iwekwe ili madeni hayo yalipwe – aidha kutokana na mali zilizoachwa na marehemu au yalipwe na ndugu, jamaa na marafiki haraka iwezekanavyo.

Watu bora kabisa katika umma huu, yaani Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) na Maswahaba Abubakar na Umar (Allah awe radhi nao) – wote waliondoka duniani wakiwa na madeni. Lakini muhimu zaidi, waliacha utaratibu wa madeni hayo kulipwa.

Ikiwa kuna mali yoyote iliyochukuliwa kinyume na sheria, basi mali hiyo inapaswa kurejeshwa kwa wamiliki wake halali na kuwaomba msamaha. Kama hili haliwezekani, basi tafuta ushauri kutoka kwa wanazuoni au wanasheria wa Kiislamu ili kujua nini cha kufanya.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button