Fahamu usiyoyajua

MJUSI MPOLE MWENYE MAAJABU.

Mjusi mpole mwenye maajabu mengi.

Naam ndugu yangu msomaji, karibu tena katika safu hii tujifunze mambo mbalimbali kuhusu viumbe wa Allah, Mbora wa Uumbaji. Juma hili nataka tukamtazame kiumbe anayefahamika kwa jina la armadillo girdled lizard.

Huyu ni mjusi anayepatikana katika pwani ya Magharibi mwa Afrika ya Kusini. Maeneo ambayo Armadillo girdled hupendelea kuishi ni katika miamba na kwenye miteremko ya milima.

Mjusi huyu ana mkia mrefu na mgumu na miguu minne; miwili mbele na miwili nyuma. Allah, Mbora wa Uumbaji, amempamba mjusi huyu kwa rangi ya kahawia nyepesi kuelekea nyeusi pamoja na rangi ya manjano.

Urefu wa Armadillo girdled kuanzia kichwani hadi kwenye mkia unaanzia inchi 3 hadi 3.5, na urefu wake kuanzia kichwani hadi miguuni unaweza kufikia hadi sentimita 20.

Mwili wa Armadillo girdled umefunikwa kwa gamba gumu ambalo humsaidia kujikinga dhidi ya mashambulizi ya wanyama wakali. Mijusi hawa wanaweza kuishi hadi miaka 25 kwenye mazingira ya kufugwa. Kwa wale wanaoishi kwenye mazingira yao ya asili (katika miamba na milimani) bado haijajulikana wanaishi miaka mingapi.

Uzazi na chakula

Wataalamu wa elimu ya viumbe wanasema, mijusi hawa hutaga mayai lakini hawayatoi nje. Wao hutaga mayai na kuyatotoa yote ndani ya mwili na siku chache baadae watoto wawili au mmoja huzaliwa.

Kwa upande wa chakula, Armadillo girdled hupendelea kula wadudu wadogo jamii ya reptilia kama buibui, mchwa na wengineo.

Mambo 10 usiyoyafahamu kuhusu armadillo girdled lizard

Kwanza, mijusi hawa hutumia muda wao mwingi wa mchana kupumzika na hutafuta chakula wakati wa usiku.

Pili, ni wanyama wanaopenda kuishi kijamaa, na mara zote utawaona wakiwa katika makundi ya mijusi 30 hadi 60.

Tatu, ingawa muonekano wake huwatisha wengi, Armadillo girdled ni kiumbe mtulivu sana ambaye muda wote hutembea polepole.

Nne, ana mkia mrefu unaoweza kufikia hadi sentimita 40.

Tano, wanyama wengi hushindwa kuwawinda Armadillo girdled kutokana na ugumu wa ngozi yao.

Sita, hutaga mayai na kuyatotoa ndani ya miili yao (Ovoviviparity).

Saba, mikia yao inaweza kurefuka zaidi kuliko miili yao.

Nane, ni katika wanyama wanaokabiliwa na matatizo mengi ya kimazingira ikiwemo joto kali katika maeneo wanayoishi.

Tisa, tabia ya kushangaza ya mijusi hawa ni kwamba, huficha vichwa vyao kwenye mikia na hawavitoi mpaka wajiridhishe pasipo shaka kwamba maadui wameondoka. Kumi, maadui zao wakubwa ni tai na falcon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button