Familia

Hatari tano zinazomzunguka mtoto katika malezi

Malezi ya watoto hayajawahi kuwa suala gumu na lenye changamoto kama katika nyakati hizi za maendeleo ya teknolojia, utandawazi na ukuaji wa miji inayopelekea mchanganyiko wa watu.

 Ukiacha changamoto hizo tatu nilizozitaja, kiimani ingetosha kututanabahisha hatari ya nyakati hizi maandiko ya dini yetu tukufu ya Uislamu pale Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliposema karne bora ni ile aliyoishi yeye na Maswahaba zake, kisha waliofuata na kisha waliofuata tena. Hii inaweza kutafsirika kuwa, kwa ujumla nyakati bora ni zilizotangulia.

Lakini masheikh pia wamekuwa wakituambia kuwa dalili kadhaa za nyakati za mwisho, ambazo Mtume alizitabiri, zimeanza kuonekana. Nyingi ya dalii hizo zinahusisha kuporomoka kwa maadili kama kuenea kwa unywaji pombe, nyimbo na miziki, zinaa, riba, mauaji, watu kutembea uchi – mambo ambayo yameanza kudhihiri.

Katika mazingira haya, ni muhimu kuwa muangalifu na vyanzo mbalimbali ambavyo vinaweza kuharibu maadili ya watoto, ambayo kwa miaka ya karibuni, yameporomoka kwa kiwango kikubwa. Leo hii, hata mzazi anapojitahidi kumuongoza mtoto, anakabiliana na nguvu nyingine kadhaa za ushawishi zinazomsukuma mtoto upande wa uovu na kumfundisha jeuri, dharau, na kila aina za maasi kama vile ulevi, kamari, zinaa na kadhalika.

Hebu tuone maeneo ambayo yanaweza kuwa asili na vyanzo vya nguvu za uovu ambazo mzazi wa leo yabidi awe makini kukabiliana nazo.

Vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki

Teknolojia ina faida zake lakini pia ina hasara zake hasa katika malezi ya watoto wetu. Katika miaka ya hivi karibuni, watoto wamekuwa wakitazama mambo maovu kwenye televisheni pamoja na mitandao ya kijamii na kuyaiga. Jambo hiili limepelekea watoto kujifunza tabia chafu kutoka kwenye tamaduni ngeni, hususan za kimagharibi.

Kutokana na maendeleo hayo ya sayansi na teknolojia yanayoruhusu watoto kuona utamaduni wa mbalimbali ya nje, hasa nchi za Magharibi. Utamaduni huo una ushawishi mkubwa kwa watoto na mara nyingi huwafanya vijana wetu waone kuwa watoto Uislamu na Uafrika wao hauna maana.

Kwa hali hii, wazazi tunatakiwa kuwa makini na watoto wetu hasa pale tunapowapa uhuru wa kumiliki simu janja ambazo ni mlango mpana wa kuonea mazuri na mabaya duniani kote. Tuwe makini tunapowapa watoto uhuru wa kumiliki akaunti za mitandao ya kijamii Mfano; Facebook, WhatsApp, Instagram pamoja na mitandao mingine. Ni muhimu pia tudhibiti nini wanaweza kuangalia katika televisheni na kusikiliza katika redio.

Mazingira ya ujirani tunapoishi

Jambo jingine linaloweza kuharibu maadili ya watoto ni mazingira mabaya ya mahali tunapoishi. Hapa sizungumzii hali ya nyumba au ukubwa wake, wala pia sizungumzii umaskini. Nazungumzia maeneo ya ujirani ilipo nyumba yenu. Je, mazingira hayo ni salama?

Hebu fikiri mtoto anakaa kwenye mazingira ya mtaa ambapo kunauzwa madawa ya kulevya au kuna kijiwe cha ukahaba na maskani ya wavuta bangi! Ni wazi kuwa, mtoto huyo atakuwa kwenye hatari kubwa ya kuiga tabia hizo chafu. Hata kama hataiga, huenda anayoyaona yatamuathiri kisaikolojia. Tunachosema ni kuwa, tuwe waangalifu na mitaa na hata nyumba tunazoamua kwenda kuishi.

Kwenye hili la nyumba ndio tuwe waangalifu zaidi maana kuna nyumba nyingine zimejaa wapangaji wahuni watupu: malaya, majambazi, wavuta bangi, wauza dawa za kulevya na kadhalika. Unaweza pia kujikuta unaishi nyuma ya wapenda sherehe za miziki na ngoma au wanawake ambao matusi kwao ni kama kusalimia tu. Unamlindaje mwanao katika mazingira hayo?

Muhimu katika hili ni kuwa tuwe waangalifu tunapotafuta eneo la kupanga au kujenga kwa ajili ya kuishi, lakini kama ikibidi kukaa mahali fulani ambapo majirani siyo wazuri basi tutafute namna ya kufanya ili kudhibiti maingiliano ya watoto na makundi ya watu waovu.

Unawajua marafiki wa mtoto?

Sababu nyengine inayopelekea kuharibika kwa maadili ya watoto ni marafiki. Inawezekana mtoto amelelewa vizuri nyumbani kwao lakini akajifunza mambo mabaya kutoka kwa marafiki zake anaokutana nao katika mazingira ya shuleni, ujirani na kwingineko anapotembelea.

Bahati mbaya ni kuwa, kama mzazi, huwezi kurekebisha tabia za watoto wote ambao mtoto wako anakutana nao kwani wao wana wazazi wao, lakini walau unaweza kumdhibiti mwanao kwenye suala la kuchagua marafiki. Tuongee na watoto wetu kuwaelezea kwa nini wanapaswa kuchagua marafiki wazuri na kuwapa elimu ya kupambanua kati ya rafiki mwema na muovu.

Na ikibidi, kama unahisi mtoto fulani analeta ushawishi mbaya kwa mwanao, iwe nyumbani au shule; tumia busara za kumuweka mbali na mwanao.

Watu wa karibu. Kikulacho….

Vitendo vya unyanyasaji vimeshamiri sana hivi leo. Watoto wamekuwa wakitukanwa, kuchomwa, kupigwa, kubakwa, kulawitiwa na kufanyiwa ukatili mwingine mbalimbali. Mtoto anapofanyiwa hivyo, anaathirika kisaikolojia na kumfanya akue akiwa na majeraha ya nafsi, akili na mwili. Mara nyingi watoto waliofanyiwa unyanyasaji hutaka kulipa kisasi au hukata tamaa na kuamua kuishi maisha ya hovyo.

Bahati mbaya sana aghlabu watoto wamekuwa wakinyanyaswa na watu wa karibu katika familia ambao sisi wazazi tunawaamini mno kiasi cha kuweza hata kuwaachia watoto tuwalee. Jambo linatulazimisha tuwe waangalifu, kwa kuchukua hatua kadhaa.

Mada hii tumeizungumza sana katika makala zetu lakini hatupaswi kuwaweka watoto katika mazingira hatarishi, hata mbele ya watu tunaowaamini. Mgeni kaja nyumbani, usimlaze na mwanao. Usiruhusu mtu kumtania kwa kumshikashika mtoto wako eti ‘njoo hapa mchumba’.

Labda hatari ni wewe mwenyewe mzazi

Fikiria, unataka kumkinga mwanao kumbe na hatari, kumbe wewe mwenyewe ndio hatari kubwa zaidi kutokana na aina ya malezi unayompa mwanao.

Wazazi au walezi wamekuwa mfano mbaya kwa watoto. Wazazi, kwa mfano, wamekuwa wakilewa, wakitukanana, wakipiganana au hata kufanya mambo mengine machafu kama vile uzinzi mbele ya watoto. Matokeo ya hali hii ni watoto kuiga tabia hizo, wakizichukulia kuwa ni jambo la kawaida kabisa.

Kwa mlezi ambaye amekuwa na tabia mbaya, mathalani tabia ya kutukana hovyo; hawezi kukataza au kumchapa mtoto wake anayetukana watoto wengine kwa sababu yeye mwenyewe hutukana na kuona kitu cha kawaida!

Ukiacha wazazi kuwa mfano mbaya, wengine wamekuwa wakipita njia mbaya za malezi kama kuwadekeza watoto pamoja na kutosimamia vyema maadili yao na hivyo kuwafanya wakue bila nidhamu ya kutosha. Waswahili husema: “Mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe.” Msemo huu unaelezea gharama ambazo mzazi anaweza kuingia kwa kulealea tabia mbaya za watoto. Mtoto mdokozi nyumbani, ndiye jambazi wa kesho, iwapo akiachwa bila kudhibitiwa. Unaijua adhabu ya jambazi anapokamatwa mtaani? Ni kifo. Na hapo ndiyo mzazi hulia yeye. Rekebisha tabia mbaya ya mtoto sasa maana dawa ya jipu ni kulitumbua tu.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Check Also
Close
Back to top button