Biashara na Uchumi

Fedha inavyoweza kuwa neema au balaa kwako

Fedha ni nyenzo muhimu inayomuwezesha mtu kupata bidhaa au huduma fulani. Fedha, au pesa kama wengine wanavyoiita, yenyewe haina faida ila inatumika katika jamii kama njia ya kujipatia mahitaji mengine.

Labda kabla sijasonga mbele, kwanza tukariri kichwa cha habari cha makala hii. Kimeandikwa ‘Fedha inavyoweza kuwa neema au balaa kwako.’ Kichwa hiki hakisemi ni dhambi kuwa na pesa au kutafuta pesa. Lakini kama tujuavyo, pesa ni nguvu, na nguvu ni muhimu kuliko kitu chochote hapa duniani.

Hata kabla ya kuanza mfumo wa pesa za karatasi tunazotumia leo, pesa zilikuwa zinatumika. Kwa kutambua thamani na umuhimu wa fedha, wapo wanaodiriki kusema fedha ni sabuni ya roho au fedha ni kila kitu maishani. Wanazo sababu nyingi wanaoiamini dhana hii. Ukiwachunguza ndugu, jamaa na marafiki, utagundua wengi wanatamani kuwa matajiri bila kujua ni kwa namna gani watapata utajiri.

Ingawa watu masikini wanapenda maisha mazuri, ukweli ni kwamba wengi wao hasa wale wasiokuwa na hofu ya Mungu hawajali ni njia gani au mfumo upi wanaweza kuutumia ili wapate pesa. Wanachojali wao ni kutajirika ili wathaminiwe na kuheshimika mbele za watu. Hii ndiyo sababu hasa iliyonifanya niandike makala hii.

Tukirejea katika historia za Manabii, tunakutana na kisa cha Mfalme mmoja mkubwa ambaye alisifika kwa kila tabia njema. Namzungumzia Nabii Suleiman bin Daudi (amani ya Allah imshukie), ambaye kutokana na hekima yake alipata nguvu ya kiutawala (kisiasa) na utajiri (uchumi) usiofikiwa na mfalme yeyote duniani.

Qur’an Tukufu inaeleza wazi kuwa, Nabii Suleiman alipoanza kutawala alimuomba Mungu ampe hekima, maarifa na ufahamu ili aweze kuongoza watu kwa haki, amani, uadilifu na uwajibikaji. Mfalme huyu anakumbukwa kama kiongozi aliyewaongoza watu wake kwa kuzingatia misingi ya utu, uadilifu na unyenyekevu wa hali ya juu bila kujali hali zao za maisha.

Suleiman alijua kuwa anawaongoza watu wenye wasifu mbalimbali – masikini, matajiri, wasomi, mambumbumbu n.k. Je, ni viongozi wangapi wa Kiislamu wamefikia sifa hizo, au moja ya sifa hizo, hasa uvumilivu? Katika kisa hiki cha Nabii Suleiman tunajifunza kuwa, mtu anao uwezo wa kutumia madaraka au fedha kuwatendea watu mambo mema kama ambavyo anaweza kutumia fedha au madaraka kuwadhuru.

Fedha ikitumika vizuri inaweza ikawa msaada katika kufanya maamuzi, lakini ikitumika vibaya inaweza kuleta uharibifu mkubwa katika jamii, taasisi, jumuiya, asasi na mashirika. Maisha ya Nabii Suleiman (amani ya Allah imshukie) ni mfano wa kuigwa kwa mtu anayetaka kujenga uhusiano mwema na Mola wake na jamii inayomzunguka.

Ole wao wenye ‘kuabudu’ mali

Ukiangalia maisha ya Qarun utaona yamejaa majivuno, kiburi na kufru. Qarun alijaaliwa kuwa na mali nyingi, lakini alisahau lengo la kuwepo kwake hapa duniani akawa mwenye majivuno na kuona kuwa utajiri aliyonao kaupata kwa juhudi na elimu yake.

Watu wake wa karibu walipomnasihi aache kiburi na majivuno aliwaambia: “…hakika nimepewa haya (mali hizi) kwa sababu ya elimu niliyonayo.” [Qur’an, 28:78].

Kwa kutakabari kwake huko, aliangamizwa kwa kudidimizwa ardhini yeye na nyumba yake. “Basi tukamdidimiza yeye (Qarun) na nyumba yake ardhini, wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia kinyume na Mwenyezi Mungu, wala hakuwa miongoni mwa walioweza kujisaidia.” [Qur’an, 28:81].

Ninachotaka uelewe katika kisa cha Qarun ni kwamba, tamaa ya kupenda sana mali inaweza kukufarakanisha na Muumba wako. Hii ina maana, ukisukumwa na upendo wa kutaka ‘maisha mazuri’ ya dunia ni rahisi sana kuitupa imani yako. Hivyo, usikubali fedha iweke rehani uhusiano wako na Mola wako.

Muombe Allah akuondolee kiu ya kupenda fedha ili usije farakana nae. Msingi wa kuwa na mafanikio kwa chochote unachotaka ni kufanya kazi ya halali na kumtegemea Allah, na si vinginevyo. Mali (fedha) inaweza kukutia upofu usione umuhimu wa kumtii na kumuabudu Muumba wako.

Zaidi ya yote, fedha inaweza kukufanya uhalalishe maovu. Mwenyezi Mungu anasema: “Na katika watu wapo wanaojifanyia waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama mapenzi yapasayo kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walioamini mapenzi yao ni kwa Mwenyezi Mungu.” [Qur’an, 2:165].

Aya inaashiria namna wanadamu walivyolewa mapenzi ya kuwapenda zaidi viumbe kuliko Muumba wao, jambo ambalo ni vigumu kulitenganisha na dhambi ya shirk. Hali hii inajiri katika zama hizi ambazo jamii imezingwa na matamanio ya kupenda mno mali.

Ikiwa huo ndiyo ukweli, tujiulize, ni kwanini Uislamu umewaonya watu juu ya jambo hili? Jawabu ni kwamba, onyo na karipio ni dhidi ya kupenda mali kiasi cha kumfanya mtu kuitafuta kwa gharama na njia ya aina yoyote kama vile ushirikina, kumtoa mtu kafara, wizi, kudhulumu au kunyang’anya.

Kutokana na huruma na mapenzi aliyonayo Allah Ta’ala juu ya viumbe wake, ni dhahiri hakuna hoja inayoweza kuukataa ukweli huu wa wanadamu juu ya kupenda sana mali. Hili ni jambo linalostahiki kutazamwa kwa kupitia dirisha la moyo pamoja na macho ya hekima.

Kwa sababu hiyo, ni Allah Mtukufu ndiye anayestahiki kuthaminiwa na kutukuzwa kwani Yeye ndiye aliyeziumba nyoyo zetu kwa kuzifungamanisha na mfumo wa mapenzi yenye hisia katika kupenda mali. Ajabu ni kwamba kadri siku zinavyosonga ndivyo watu wengi wanavyozidi kutafuta mali bila kujali kama njia (mifumo) wanazotumia kutafuta mali hizo ni za halali au za haramu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button