
Wepesi wa Uislamu katika ibada na miamala
Hakika Uislamu umekuja na sheria tukufu inayowiana na mahitaji ya watu katika nyanja mbalimbali za maisha. Kadhalika, sheria ya Kiislamu ina sifa lukuki, na miongoni mwa hizo ni kuondoa vikwazo katika maisha ya binadamu na viumbe wengine.
Uislamu umeondoa uzito kwenye sheria, miamala na hukumu zake zote. Kwa mantiki hiyo, Uislamu ni mwepesi katika nyanja zote. Ingawa yapo mambo ya kiibada ambayo kwa dhahiri yanaonekana kama ni mateso au usumbufu, mfano kufunga, kuhiji, kupigana katika njia ya Allah na mengineyo, kimsingi mambo hayo yamewekwa mahsusi kwa lengo la kumpandisha daraja mwenye kuyatenda, na jamii ya Kiislamu kwa ujumla.
Siku zote faida za kufanya ibada huwa kubwa licha ya ugumu anaoupata mtu, na hii inatokana na ile nguvu ya ndani iliyowekwa kwetu na Allah ‘Azza Wajallah’.
Katika sheria zote za Kiislamu, kuna vipengele kadhaa vya kuondosha vikwazo na kuleta wepesi katika ibada, miamala mbalimbali, na pia kwenye maeneo mengine ya maisha ya kila siku ya Muislamu. Vifuatavyo ni baadhi ya vipengele hivyo vya kuleta wepesi.
Uwepesi katika twahara
Wakati wowote nguo ya mtu ikipatwa na najisi, inatosha kuosha mahali paliponajisika, na wala halazimiki kuifua nguo yote. Kadhalika, inatosha kukipaka maji kichwa badala ya kukiosha wakati wa kutia udhu. Vilevile, mwanamke anapohisi uzito au usumbufu wakati wa kuoga janaba hashurutishwi kufumua nywele. Pia, kutayamamu kumewekwa kama mbadala wa maji pindi yanapokosekana.
Allah anasema: “Enyi mliyoamini! Mnaposimama kwa ajili ya swala, basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake kwenye vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Mwenyezi Mungu hapendi kukutieni katika tabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.” [Qur’an 5:6].
Ibada ya sala
Na kwenye ibada ya sala, kuna wepesi katika sala ya watu wenye udhuru, mfano wagonjwa, watu wasioweza kusimama au kuketi, watu wenye maradhi ya kutokwa na haja ndogo, au kutomudu kukaa na udhu.
Pia, Uislamu umeweka wepesi kwa msafiri ambapo sheria inamruhusu kukusanya na kupunguza sala mbili za Adhuhuri na Alasiri na Magharibi na Isha kwa kuzitanguliza au kuziahirisha. Kadhalika, sheria inaruhusu waumini kukusanya sala mbili kwa sababu ya mvua, vita na wakati wa kupambana na adui.
Na katika ibada ya zaka, Allah ametaja vitu vinavyopaswa kutolewa zaka na akaweka masharti maalum ya kutoa zaka, kama vile kufikia kiwango (Niswab), kupitiwa na mwaka, kutodaiwa, na kuweka tofauti kwenye mazao yaliyopata maji ya mvua na yale ya kilimo cha umwagiliaji.
Wepesi katika swaumu, Hijja na biashara
Katika ibada ya funga, Allah ameruhusu mgonjwa, msafiri na mjamzito kula mchana wa mwezi wa Ramadhan. Pia Allah ametoa msamaha kwa mtu aliyekula au kunywa kwa kusahau. Aidha, Allah Ta’ala ametoa ruhusa ya kuharakisha kufuturu na kuchelewa kula daku, na ameifanya funga ya Ramadhan kuwa ni mwezi mmoja tu kwa mwaka, tena wakati wa mchana.
Kwa upande wa Hijja, Allah ameshurutisha uwajibu wa kutekeleza ibada hii kuwa ni kuwapo kwa uwezo wa kimali, siha (afya) na usalama wa njia ya kwendea. Aidha, uwezo pia unaangaliwa katika kumiliki matumizi ya kwenda na kurudi pamoja na huduma kwa familia.
Katika kuuza na kununua, Uislamu unahimiza suala la maridhiano kama alivyoashiria Mtume (rehema za Allah na amani iwe juu yake) katika hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu amemrehemu mtu anayeridhia anapouza, anaponunua na anapodai.” [Bukhari]. Kwa maana hiyo, Uislamu unahimiza kuangalia hali ya mtu anayedaiwa.
Na katika masuala ya ndoa, Uislamu unaruhusu mwanaume kumuona mwanamke aliyemposa, pia Uislamu umempa mwanamke haki ya kuchagua mume pasipo kulazimishwa kuolewa na asiyempenda.
Malezi na kufanya ibada kwa kiasi
Historia ya Mtume (rehema za Allah na amani iwe juu yake) imesheheni matukio mengi yanayoonesha jinsi alivyokuwa anafundisha malezi na namna ya kufanya ibada kwa kiasi (wastani).
Mfano wa hili ni yule swahaba aliyeweka nadhiri ya kufunga na kutofungulia, na kusali usiku bila ya kulala. Mtume alimwambia swahaba yule: “Ibada haiwi hivyo na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi wa mtu kujitesa.” Suala la wepesi katika ibada na miamala lina umuhimu mkubwa kwenye sheria ya Kiislamu. Moja kati ya umuhimu wake ni kuzingatiwa hali halisi aliyonayo binadamu, sifa na uwezo wake wenye ukomo. Ijulikane kuwa, lengo ni kufikia kilele cha ibada, na wala siyo kumtesa binadamu kwani tabu mwishowe inatakiwa ilete wepesi.