Darsa za wiki

Nilivyogundua rafiki mwema ni mtaji wa Akhera

Wakati nasoma chuo kikuu miaka kadhaa iliyopita nilikuwa na rafiki yangu mmoja ambaye tulishibana sana. Miongoni mwa mambo muhimu ambayo alikuwa akinisisitiza mara kwa mara ni kujiepusha na anasa za dunia.

Daima alikuwa akinikumbusha kusali muda wa sala unapofika, na hakuacha kunikumbusha juu ya kutumia neema ya afya kwa mambo yenye faida kwa Akhera na dunia. Kwa hakika najivunia kuwa rafiki yake, maana rafiki wa kweli hawezi kukuacha upotee.

Kiukweli, wakati ule sikuwa namuelewa kabisa anachoongea, labda kwa sababu ya kutawaliwa na hisia kali za ujana. Lakini sasa naona faida yake. Kumbe basi, nimejifunza kuwa kusuhubiana na rafiki mwema kuna umuhimu wake hasa pale urafiki huo unapofungamana na maslahi ya Akhera.

Katika moja ya mafundisho yake kwetu kuhusu kuamiliana na marafiki, Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) amesema: “Mfano wa rafiki mzuri na rafiki mbaya ni kama muuza misk (manukato) na mhunzi (mfua vyuma). Muuza misk – aidha atakupa au utanunua kutoka kwake, ama utanusa harufu nzuri kutoka kwake. Na yule mhunzi – aidha atachoma nguo yako au utapata harufu mbaya kutoka kwake.” [Bukhari na Muslim].

Katika kuifasiri hadith hii, Imam Nawawi (Allah amrehemu) amesema, Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amelinganisha rafiki mzuri na muuza misk kwa sababu, mtu akisuhubiana na rafiki mzuri, mpole na mwenye elimu atapata faida kwake.

Imesemwa pia kuwa kusuhubiana na watu wema hupelekea kupata elimu yenye faida, tabia nzuri na kudumisha ibada. Kwa maana hiyo, rafiki akiwa mbaya utaathirika na tabia zake kama ilivyokuwa kwa mzuri pia utaathirika na tabia zake.

Ni muhimu sana kuchagua rafiki mwema kutokana na taathira kubwa iliyopo kati ya mtu na rafiki zake. Mtume ametwambia: “Mtu anakuwa katika dini ya rafiki yake, hivyo mmoja wenu atazame ni nani anayemfanya kuwa rafiki.” [Abu Daudi na Tirmidhi].

Kwa hiyo, mtazame kwa makini rafiki yako ili ujue ni mtu wa namna gani na ana sifa zipi. Je, ni rafiki mwema anayefaa kusuhubiana nawe? Vinginevyo, unaweza kusuhubiana na rafiki asiyestahiki.

Ni muhimu sana kutafuta sifa zenye kumridhisha Allah kwa unayemfanya kuwa rafiki ili kuepuka kupata hasara hapa duniani na kesho Akhera. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an: “Siku hiyo (ya Kiyama) marafiki watakuwa ni maadui wenyewe kwa wenyewe isipokuwa wachamungu.” [Qur’an, 43:67].

Hakuna shaka kwamba kusuhubiana na rafiki mwema kunatia nguvu mafungamano yaliyopo kati ya undugu wa nasaba na ule wa kiimani; na pia hukuza upendo uliopo kati yao na kuwafanya washikamane kama jengo moja.

Manufaa ya kushikamana na marafiki wema yanarejea kwetu wenyewe kwa kutufanya kuwa na tabia njema zinazopelekea kusaidiana na kuhurumiana. Hebu sasa tuangalie baadhi ya mambo yanayopelekea marafiki wema waliopendana kwa ajili ya Allah kudumisha uswahiba wao.

Mosi, tabia njema

Mtume (rehema za Allah na amani iwe juu yake) ametufahamisha kuwa katika kipawa bora kabisa alichopewa mtu ni tabia njema.

Mtume aliamrisha kuchanganyika na kuishi na watu kwa tabia njema aliposema: “Mche Allah popote ulipo, na fuatisha baya ulilofanya kwa kufanya jema, (hilo jema) litafuta hilo baya, na changanyika/ishi na watu kwa tabia njema.” [Tirmidhi].

Hadith hii tukufu inaonesha jinsi tabia njema inavyoweza kuimarisha uhusiano na mafungamano baina ya watu, na pia humpendeza sana Allah. Mtume ametufahamisha kuwa, miongoni mwa malengo makubwa ya kutumwa kwake ni kukamilisha (kutimiza) tabia njema, kama anavyothibitisha: “Hakika nimetumwa ili nikamilishe tabia njema.” [Ahmad].

Kwa maana hiyo, tabia njema ni sehemu ya kumuiga Mtume Muhammad. Mtume alikuwa ni mwenye tabia njema hata kabla ya kupewa utume hadi ikafikia hatua ya kuitwa Mkweli Mwaminifu. Tabia hizi mbili (ukweli na uaminifu) ndizo zilizowafanya Maswahaba (Allah awaridhie) wapende kusuhubiana naye.

Pili, kumpa kila mmoja haki yake anayostahiki

Na miongoni mwa mambo yanayodumisha urafiki ni kuwapa marafiki haki zao kulingana na nafasi zao katika jamii. Baadhi ya wataalamu wamesema, kuna namna tofauti za kusuhubiana na marafiki.

Mtu mzima, Sheikh na kiongozi, unatakiwa usuhubiane nae kwa wema na kumpa huduma zilizo katika uwezo wako. Kwa yule unayelingana nae kiumri suhubiana nae kwa kumpa nasaha na kusaidiana katika mema.

Kwa mwanafunzi, suhubiana nae kwa kumuelekeza na kumfundisha adabu anazopaswa kujipamba nazo kwa mujibu wa adabu za kielimu na kufuata mwenendo wa Uislamu.

Tatu, kusamehe makosa madogo madogo

Wasamehe marafiki zako makosa madogo madogo ambayo hayana athari katika dini wala kimaadili. Allah Aliyetukuka anasema: “Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.” [Qur’an, 15:85].

Kusamehe huku ni kusamehe kusikoleta madhara kwa kukumbushana na kurekebishana katika mambo yenye kasoro, na si kugombana na kuhasimiana.

Mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu, Fudhwail bin I’yaadh (Allah amrehemu) amesema: “Kama ambavyo mtu anapendelea kusamehewa pale anapokosea, na yeye pia anatakiwa awe mwepesi kusamehe pale anapokosewa.” Pia, Ibn Arabi (Allah amrehemu) amesema: “Sahau makosa ya ndugu, upendo wao utadumu kwako.”

Nne, kusitiriana aibu

Baadhi ya watu hugundua au hukuta aibu fulani kwa wenzao. Jambo lililo bora ni kujitahidi kuiondosha aibu hiyo kwa kumtanabaisha, kumuongoza na kumsaidia, badala ya kumfedhehesha na kumuaibisha mbele za watu au kumtangazia aibu yake hiyo.

Baadhi ya wema waliopita walisema: “Muumini humtafutia udhuru mwenzake na mnafiki humtafutia dosari mwenzake.” Maana yake ni kwamba, muumini anapoona udhaifu kwa mwenzake huanza kumdhania vizuri na kuona ndugu yake huyo aidha amejisahau, hajui au amekosea.

Lakini mnafiki hungojea na kufuatilia ili kuona kama mwenzake atajikwaa ili apate kumfedhehesha.

Tano, kusaidiana katika mambo ya heri

Jambo jingine linaloweza kudumisha urafiki wa watu wema waliopendana kwa ajili ya Allah ni kusaidiana katika mambo ya heri pale mmoja anapohitaji msaada – uwe wa kielimu, mazingira, nasaha na mengineyo ambayo yana msaada katika jamii.

Allah anatwambia: “Na saidianeni katika wema na uchamungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.” [Qur’an, 5:2].

Urafiki uliojengeka katika misingi inayomridhisha Allah huwa ni wenye kudumu. Ama ule uliojengeka katika misingi ya maslahi ya kilimwengu ni vigumu kudumu hasa pale yanapokosekana maslahi husika.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button