Darsa za wiki

Neema za Allah na umuhimu wa kuzishukuru – (1)

Neema za Allah kwa waja wake

Allah Mtukufu amewaneemesha waja wake kwa baraka nyingi na fadhila kubwa. Neema hizi zimegawika katika makundi makuu mawili. Kwanza, kuna neema za kidini na pili kuna neema za kidunia.

Neema za kidini

Neema za kidini ni zile zinazohusiana moja kwa moja na dini, mfano kuongozwa katika mambo ya kheri na kadhalika.

Jopo la Wanazuoni wa Kiislamu limesema, neema kubwa zaidi kwa mwanadamu ni kuongozwa katika Uislamu, ambao ndiyo dini ya haki aliyoichagua Allah kwa viumbe wake kupitia ujumbe wa Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah ziwe juu yake).

Neema za kidunia

Neema hizi zinajumuisha mambo yanayoonekana kama vile kuruzukiwa vyakula vya aina mbalimbali na vinywaji, makazi, mavazi, neema ya kusikia, kuona, kuhisi na kadhalika.

Hali ya Muislamu katika neema na mitihani

Muislamu anaweza kuwa katika mojawapo ya hali mbili. Aidha atakuwa katika hali ya kushukuru neema za Allah Mtukufu, au atasubiri mitihani na majaribu kutoka kwa Allah.

Hii inaonesha umuhimu mkubwa wa kumshukuru Allah Mtukufu, hasa kwa kuwa ameahidi kuongeza neema kwa wale wanaoshukuru, kama anavyosema ndani ya Qur’an: “…ikiwa mtashukuru, bila shaka nitakuzidishieni (neema zangu), na mkikufuru basi hakika adhabu yangu ni kali.” [Qur’an, 14:7].

Maana ya shukrani kwa Allah Mtukufu

Shukrani kwa Allah Mtukufu ina maana ya kuonesha athari ya neema za Allah kwa kauli na vitendo. Wamesema wanazuoni: “Shukrani ni kutambua neema za Allah Mtukufu kwa unyenyekevu.” Ibn Qayyim (Allah amrehemu) amesema: “Shukrani ni kuonesha athari ya neema za Allah kupitia ulimi kwa kumsifu na kumtukuza Allah; moyo kwa kutambua na kupenda neema hizo; viungo vya mwili kwa utiifu na unyenyekevu kwa Allah.”

Daraja ya shukrani na umuhimu wake kwa muumini

Shukrani ni miongoni mwa daraja za juu kabisa za kiimani, ikiwa shukrani hiyo itaambatana na kuridhia. Haiwezekani mtu akawa na shukrani ya kweli bila kuridhia.

Shukrani ni nusu ya imani kwa sababu imani imegawika sehemu mbili; shukrani na subira. Allah Mtukufu ameamrisha watu kushukuru na amekataza kinyume chake, amewasifu wenye shukrani na amewahusisha na waja wake maalumu.

Shukrani ni sababu ya kuongezewa neema kama alivyoahidi Allah Mtukufu. Allah amewapa wenye kushukuru sifa iliyotokana na mojawapo ya majina yake ‘Ash–Shakur’, yani mwenye shukrani. Na Allah humpa mwenye kushukuru kile anachostahili.

Anasema Allah: “Na mshukuruni Mwenyezi Mungu ikiwa mnamuabudu Yeye tu.” [Qur’an, 2:172) Pia amesema: “Na nishukuruni Mimi, wala msinikufuru.” [Qur’an, 2:152, pia rejea kitabu cha ‘Madarij As–Salikin’ cha Ibn Qayyim, juzuu ya 2, ukurasa 586].

Nguzo tatu za shukrani

Shukrani kamili haiwezi kupatikana isipokuwa kwa kuwepo nguzo kuu tatu. Kwanza, kutambua neema za Allah kwa moyo (ndani ya nafsi), pili kuzipenda na kuzitaja kwa ulimi neema ulizopewa, yani kumsifu Allah na kumtukuza kwa sifa njema na shukrani, na tatu kuzitumia neema hizo kwa utiifu (kumtii Yeye) na kujiepusha na maasi.

Mwanadamu anatakiwa kutumia neema ya viungo vya mwili wake katika kumtii Allah na kuviepusha na maasi.

Mtume wa Allah katika kushukuru

Imepokewa hadith katika Bukhari na Muslim kuwa, Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) alikuwa akisimama kusali mpaka nyayo zake zinavimba. Alipoulizwa kwanini anafanya hivyo ilihali Allah ameshamsamehe madhambi yake yaliyopita na yajayo alisema: “Je, basi nisiwe mja mwenye shukrani?”

Kushukuru kama njia ya kudumisha neema na kuzidishiwa baraka

Kushukuru ni sababu ya kuongezeka kwa baraka za Allah Mtukufu na kudumisha neema. Khalifa Umar bin Abdul–Aziz aliwahi kusema: “Dhibitini neema za Allah Mtukufu kwa kuzishukuru.”

Pia, siku moja Ali bin Abi Twalib (Allah amridhie) alimwambia mtu mmoja kutoka mji wa Hamdhan: “Neema zimeunganishwa na shukrani, na shukrani zinahusiana na kuongezewa. Zote mbili (neema na shukrani) zimefungwa kwa kifungo kimoja. Kwa hivyo, Allah Mtukufu hataacha kuzidisha neema kwa mja wake mpaka pale shukrani ya mja itakapokoma.” [Rejea kitabu ‘Al–Bahr ar–Raiq’ cha Ahmad Farid, ukurasa 216].

Nae mwanachuoni Hasan al–Basri amesema: “Ongezeni kutaja neema hizi kwani kuzitaja ni aina ya shukrani.” Allah Mtukufu alimwambia Mtume wake (rehema na amani ziwe juu yake): “Ama kwa neema ya Mola wako, basi itangaze.” [Qur’an, 93:11].

Allah alimuamrisha Mtume atangaze neema zake kwa sababu, Yeye, Allah anapenda kuona athari ya neema zake kwa waja, kwani hiyo ni aina mojawapo ya shukrani. Itaendelea wiki ijayo Insha Allah

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button