
Njia za kukwepa kujibu maswali ya kibinafsi kistaarabu
Sote tumewahi kuwa katika hali hii—mtu anakuuliza swali la kibinafsi linalokufanya usijisikie vizuri. Inaweza kuwa kuhusu mshahara wako, hali yako ya ndoa, mipango yako ya baadaye, au masuala mengine binafsi.
Kukabiliana na maswali kama haya kunaweza kuwa changamoto kwani unataka kuweka mipaka yako bila kuonekana jeuri. Zipo mbinu bora za kukabiliana na maswali ya kibinafsi kwa ustaarabu.
Mosi, elekeza mazungumzo kwingine
Njia rahisi ya kuepuka kujibu swali la kibinafsi ni kubadili mada ya mazungumzo kwa ustadi. Badala ya kulijibu swali moja kwa moja, toa jibu la jumla kisha hamisha mazungumzo kwenye mada nyingine.
Mfano, ukiulizwa: “Unapanga kuolewa lini?”, sema: “Ndoa muhimu sana lakini umesikia kuna mhadhara umeandaliwa wa kukaribisha mwezi wa Ramadhan. Utafanyika Temeke Mwembeyanga, umepanga kuhudhuria?”
Mfano mwingine: Akiuliza, “Kwa nini bado hujazaa watoto?”, jibu linaweza kuwa: “Hivi unajua Ramadhan inakaribia? Nimepanga kuchukua mapumziko kazini, je, wewe una mipango gani mwaka huu?”
Kubadili mada ghafla kunawafanya watu waelewe kuwa hupendi kuzungumzia jambo fulani na hakika njia hii inakusaidia kujiondoa kwenye mazungumzo yasiyofurahisha bila kumuudhi aliyekuuliza.
Pili, tumia mizaha au ucheshi
Ucheshi ni silaha bora ya kuepuka maswali ya kibinafsi. Jibu la kuchekesha linaweza kufanya watu waelewe kuwa hujisikii kujibu bila ya wao kukasirika. Mfano ukiulizwa: “Unalipwa kiasi gani kazini?”, unaweza kujibu: “Kiasi cha kutosha kulipa bili lakini haitoshi kununua ndege binafsi.” Jibu kama hili linabaki kuwa la kirafiki huku likionesha kuwa hupendi kujadili suala hilo.
Tatu, kwa heshima, weka wazi hutaki kuulizwa
Wakati mwingine unaweza kuamua kujibu swali binafsi kwa kuwa mkweli lakini kwa njia ya heshima. Mfano, mtu akikuuliza: “Kwa nini huna watoto bado?”, unaweza kujibu: “Asante kwa kuuliza lakini hilo ni jambo la kibinafsi kwangu na siko tayari kuliongelea. Hata hivyo, asante kwa kujali.”
Jibu hili linahifadhi heshima huku likionesha kuwa hutaki kulizungumzia. Mtu muelewa, hatauliza tena.
Nne, jibu swali kwa swali
Njia nzuri ya kumfanya mtu atambue kuwa anaingilia faragha yako ni kumrudishia swali lake. Mfano, mtu anakuuliza: “Kwa nini bado hujaolewa?”, unaweza kujibu: “Kwa nini unauliza?” au “Vipi unataka kunitafuta mume?” au “Unataka kunichangia fedha za gharama ya harusi.” Jibu hili linamweka mtu kwenye nafasi ya kutafakari na mara nyingi hufanya aache kuuliza maswali ya kibinafsi.
Tano, jibu kwa ujumla na jibu mahsusi
Kuna nyakati ambapo majibu mafupi na ya ujumla yanatosha kuzuia mazungumzo kuendelee zaidi. Kwa mfano mtu anapokuuliza: “Unapanga kununua nyumba lini?”, unaweza kumjibu: “Hakika, muda ukifika, mambo yataenda sawa” au “Nyumba muhimu sana, ishaAllah tuombeane dua.” Jibu hili linatoa taarifa bila kutoa maelezo mahsusi ambayo mtu anaweza kushikilia na kuendelea kuuliza maswali mengine.
Sita, tumia lugha ya mwili kuweka mipaka
Lugha yako ya mwili inaweza kusaidia kutoa taarifa kuwa hauko tayari kujibu swali fulani. Ukihisi swali linaingilia sana mambo binafsi, tabasamu kwa upole huku ukionesha huna hamu ya kuendelea na mazungumzo. Unaweza pia kuepuka kumtazama moja kwa moja, kutikisa kichwa kwa upole, au kubadilisha mwelekeo wa mwili wako ili kufikisha ujumbe kuwa hapaswi kuendelea kuuliza.
Saba, epuka kuwakosea heshima wanaouliza
Mara nyingi, watu wanaouliza maswali ya kibinafsi hawana nia mbaya, ingawa maswali yao yanaonekana hayana mipaka. Hivyoo, kwa kuelewa nia yao njema, ni muhimu kujibu kwa njia isiyo ya ukali ili kuepuka kuonekana kama mtu jeuri na asiye na heshima.
Ikiwa mtu anaendelea kuuliza maswali bila kusoma dalili kuwa hujisikii vizuri kujibu, unaweza kuhitimisha mazungumzo kwa kusema kwa utulivu: “Naona umejaa udadisi sana kuhusu maisha yangu, lakini napendelea kutozungumzia sana masuala ya kibinafsi. Tunaweza kuzungumzia jambo jingine!?” Kauli hii inahakikisha kuwa umeweka mipaka yako kwa uwazi bila kuonekana jeuri, unayejisikia na usiye na heshima.
Nane, sema hapaana ukionesha tabasamu
Watu wengine wanahitaji kujifunza kuwa si kila swali linahitaji jibu. Jifunze kusema “Hilo ni jambo langu binafsi” au “Napendelea kutolizungumzia kwa sasa” huku ukiweka tabasamu la kirafiki. Kwa njia hii, unahifadhi heshima bila kulazimika kutoa maelezo.
Hitimisho
Kukabiliana na maswali ya kibinafsi kwa ustaarabu ni sanaa inayohitaji mchanganyiko wa busara, ucheshi, na ujasiri. Kutumia mbinu kama kuelekeza mazungumzo kwingine, kujibu kwa ucheshi, au kukataa kwa lugha ya wazi lakini ya upole na heshima kunaweza kusaidia kuepuka yasiyofurahisha.
Kumbuka, huwajibiki kutoa taarifa zako binafsi ikiwa hauko tayari kufanya hivyo. Ukijifunza kupambana na maswali haya kwa njia ya upole lakini thabiti, utaweza kuwasiliana kwa ufanisi huku ukihifadhi faragha yako na kutunza mahusiano mazuri na watu wengine.