Familia

Mkoba wa Mama: kisanduku cha hazina chenye maajabu

Mkoba wa kila mama ni kama kisanduku cha hazina chenye maajabu, kilichojaa vitu vingi vinavyoweza kutatua karibu dharura yoyote inayohusiana na mtoto. Kuanzia magoti yaliyokwaruzwa hadi njaa ya ghafla, mama ana utatuzi . Hebu tuchunguze yaliyomo ndani ya mikoba ya mama wengi wanaowajibika pindi watokapo nje ya nyumba zao, iwe safari ndefu au fupi.

Moja ya vitu muhimu mama hubeba ni dawa za kutuliza maumivu na dawa nyingine muhimu kama vile ya kuzuia kuharisha. Watoto wanaweza kupata homa au maumivu ya ghafla au kula kitu kikachafua tumbo, na hapo unahitaji dawa hizi.

Plasta ni kitu kingine cha lazima katika mkoba wa mama kwa ajili ya kutuliza mikwaruzo midogo na michubuko. Rangi zake angavu na michoro ya kuvutia huwafanya watoto kuziona kama zawadi, badala ya tiba,  na kubandikwa ikawa ni zawadi kwao. Tendo hili rahisi la kufunika jeraha linaweza  sio tu maumivu bali pia  hofu ya mtoto.

Vitafunwa navyo mara nyingi havikosi kwenye mkoba wa mama makini anayetoka na wanawe, akijua wazi kuwa mtoto mmoja anaweza kulalamika njaa muda wowote. Mtoto akilalamika tu, kipande cha keki, bajia au pakiti ya matunda vilivyofichwa mkobani hutolewa kukabiliana na dharura hiyo.

Vitafunwa mara nyingi vimekuwa mkombozi kwa kutoa nishati ya haraka na kumbadilisha mtoto mkorofi kuwa mwenye furaha. Si hivyo tu, mkoba wa mama utakuwa na vipipi na bazoka vya kuwaliwaza watoto waliochoka.

Kingine miongoni mwa vitu ambavyo wakinamama hubeba katika mkoba ni ‘wipes’, taulo za karatasi nyepesi zenye majimaji ambazo hutumika kwa matumizi mengi na tofauti, ikiwemo kufuta vidole vichafu, kuchambia watoto waliojisaidia hadi kusafisha uso.

Taulo hizi ni shujaa asiyeimbwa katika mkoba wa mama, zenye ufanisi, rahisi kutumia na salama kwa ngozi nyororo ya watoto  zikitumika  kudumisha usafi na afya popote walipo.

Kingine kinachofanana na wipes na muhimu katika mkoba wa mama ni tishu, rafiki wa faraja afutaye machozi, asafishae madoa madogo na ambazo ni laini na bora kwa ngozi ya mtoto. Iwapo pua ya mtoto inavuja kamasi au anataka kukamata kitafunwa sehemu ambapo hamna maji ya kunawia mikono, tishu zipo tayari kuthibitisha thamani yake tena na tena.

Mama anayewajibika pia hubeba kisafishaji mikono (maarufu kaa ‘hand sanitizer’), ambacho tone moja tu huhakikisha usafi unapatikana na kudumisha afya hasa kwenye maeneo yenye msongamano. Ni kachupa kadogo lakini kanaangamiza vijidudu haraka na kwa urahisi na hivyo ni muhimu mama abebe hasa wakati hakuna maji na sabuni karibu.

Ni muhimu pia mama abebe vitu vidogo vya kuchezea (toys) hasa kama ana watoto wadogo na wasumbufu. Vitu hivyo vya kuchezea  ni  silaha kali na ya siri ya mama dhidi ya uchovu na kuchoka kwa mtoto kwa kumteka kimawazo. Toys ni njia bora ya kuwahamasisha watoto wakati wa kungojea kwa muda mrefu au kuchelewa kusikotarajiwa.

Sambamba na toys, kalamu na karatasi ni zana muhimu katika kutatua matatizo kwa ubunifu. Kwa watoto, kuchora au kuandika huwapa nafasi ya kuonyesha hisia na mawazo yao ikiwa ni njia rahisi lakini yenye nguvu ya kuwahamasisha. Mama wanajua umuhimu wa kuwasha ubunifu kupitia njia hizi za jadi, hivyo kuzifanya kuwa sehemu muhimu ya mkoba wao.

Vibanio vya nywele pia ni muhimu kwenye mkoba wa mama kwa ajili ya kufunga nywele haraka kuziweka mbali na macho yake wakati wa kucheza au kula. Zaidi ya nywele, vibanio pia vinaweza kutumiwa kwa ubunifu, katika kubana vitu pamoja visitawanyike.

Mara umekaa umegundua mtoto siku nyingi hajakata kucha,na hapo utahitaji ‘nail cutter’ mkobani. Kwa watoto, kukatwa kucha ni sehemu ya burudani hivyo usishangae mashine hiyo ikaukoa kwenye fedheha ya kushindwa kumdhibiti mtoto mlizi.

Wanaita lip balm lakini kwa kiswahili ni aina ya mafuta kwa ajili ya kupaka midomo isikauke. Lip balm huleta faraja kwa midomo iliyokauka na kupasuka, hasa kwenye maeneo ya hali fulani ya hewa kama vile Dodoma. Unyevu wake ni mwororo na mzuri kwa watoto.

Mama pia hakosi pesa taslimu mkobani itakayomuwezesha kukabiliana na dharura zozote. Kwa kujua umuhimu wa mawasiliano wakati wa dharura, chaja pia haiwezi kukosa, sambaba na simu.

Kwa wenye bima za afya, kadi pia hazitakosekana katika mkoba wa mama sambamba na  kadi ya mawasiliano ya dharura inayobeba taarifa muhimu kwa hali zisizotarajiwa.  Kadi hizi, ya afya na ya mawasiliano, huleta utulivu wa akili, kwa sababu mama anajua msaada upo umbali wa simu moja tu ikiwa utahitajika. Vilevile, mtu akiumwa, ni suala tu la kumpeleka kwenye huduma na bima itabeba gharama.

Kitu kingine muhimu sana wakinamama wenye hekima hubeba ni dawa za kutuliza maumivu, kama panadol, na kadhalika dawa nyingine muhimu hususan za kutuliza mchafuko wa tumbo na kuharisha.

Mkobani kwa mama, akitoka na wamawe, pia kutakuwa na mafuta na losheni, akijua kuwa kwa watoto chochote kinaweza kutokea, na hivyo anaweza kuhitaji  mafuta na losheni.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button