Fahamu usyoyajuaFamilia

Fariq Naik, anavyofuata nyayo za baba yake

Sheikh Fariq Naik, mtoto wa Dkt. Zakir Naik, ni mmoja wa wanazuoni vijana wa Kiislamu ambao wamejenga jina kubwa katika ulimwengu wa ulinganiaji wa dini. Mzaliwa Julai 10, 1994, Mumbai, India, sheikh Fariq amejitokeza kwa umahiri katika kuelezea mafundisho ya Kiislamu kwa ufasaha, uelewa mpana wa maandiko ya kidini, na uwezo wa kujihusisha moja kwa moja na hadhira yake.

Safari ya sheikh Fariq katika ulinganiaji wa Kiislamu ilianza akiwa mtoto mdogo. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Kimataifa ya Kiislamu (Islamic International School) huko Mumbai, ambapo alipata mafunzo ya kina katika Qur’an na lugha ya Kiarabu. Akiwa na umri wa miaka 13, aliweza kutajika kama Haafidh wa Qur’an wa nzima, hatua iliyompa heshima kubwa katika jamii za Kiislamu.

Tangu akiwa na umri mdogo sana wa miaka 8 alifuatana na baba yake katika safari za kida’awah ambapo alianza kutoa khutba fupi fupi kwa Kiingereza na Kiarabu na vile vile kusoma Qur’an mbele ya umati mkubwa wa maelfu ya watu duniani kote. Katika safari hizo za kida’awah, sheikh Fariq alipata fursa ya kuhutubia zaidi ya watu 50,000 akiwa katika umri wa kati ya miaka 9 hadi 12.

Elimu yake haikuishia katika maandiko ya Kiislamu pekee. Kwa kufuata mfano wa baba yake, Fariq alijifunza kujenga hoja zenye mantiki katika mijadala ya kidini, akielewa kwa undani maandiko ya kidini kutoka dini mbalimbali. Hii ilimwezesha kuanza safari yake kama mzungumzaji mahiri wa kidini katika umri wa miaka 15.

Akiwa ni mhitimu wa Shahada ya Awali ya Sharia ya Kiislamu kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Imam Muhammad Ibn Saud, Sheikh Fariq Naik ananukuliwa kama miongoni mwa wanazuoni wenye kuyaelekea maswali kwa ufasaha akitumia na kuzitegemea dalili za Qur’an na  Sunna.

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, Fariq ametoa mihadhara zaidi ya 150 katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na India, Uingereza, Malaysia, na mataifa kadhaa ya Afrika. Mihadhara yake imejikita katika kuondoa mitazamo potofu kuhusu Uislamu, hasa miongoni mwa vijana. Anajulikana kwa uwezo wake wa kunukuu Qur’an, Hadith na hata maandiko kutoka dini nyingine, akifanya mazungumzo yake kuwa yenye mantiki na kuvutia.

Fariq ameshiriki katika matukio makubwa ya Kiislamu, kama vile Peace Conference International, ambayo imekusanya maelfu ya watu kutoka kote ulimwenguni. Hotuba zake zinalenga mada kama “Umuhimu wa Qur’an katika maisha ya kila siku” na “Kujenga maisha ya amani kupitia mafundisho ya Kiislamu.”

Kwa mtazamo wake wa kipekee, amekuwa akiwahamasisha vijana kuishi maisha ya uadilifu na kuyahusisha na imani yao.

Ingawa Fariq hajahusika sana katika mijadala ya moja kwa moja kama baba yake, amekuwa mstari wa mbele katika kujibu maswali magumu kutoka kwa hadhira yake, hasa katika mikutano ya vijana. Majibu yake hutegemea dalili za wazi zilizopo kwenye Qur’an na Hadith, marejeo ya moja kwa moja kutoka kwenye maandiko ya kidini, mantiki na mtazamo wa kisasa unaorandana na maisha ya kila siku.

Fariq amewekeza juhudi kubwa katika kufikia bara la Afrika, akitambua umuhimu wa jamii za Kiislamu katika bara hili. Mnamo mwaka 2024, alitembelea Nigeria, Kenya, na Afrika Kusini pamoja na baba yake, ambapo walitoa mihadhara ya aina mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuimarisha imani ya Kiislamu katika mazingira ya kijamii na kiuchumi.

Ziara zake barani Afrika zimeacha alama ya kudumu, hasa kwa vijana ambao wamehamasika kuendeleza masomo yao ya dini huku wakikabiliana na changamoto za kilimwengu.

Kuanzia 30 Disemba hadi Januari 6 Sheikh Fariq Naik na baba yake wanatarajiwa kutembelea Tanzania na kushiriki katika mihadhara mikubwa katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania Bara iliyoandaliwa na taasisi ya The Islamic Foundation inayoongozwa na mwenyekiti wake, Aref Nahdi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti, Zanzibar na washirika wa vyombo vya habari wakiwemo kampuni ya Azam. 

Kwa miongo ijayo, katika ulimwengu wa Kiislamu jina la Fariq Naik litakumbukwa kwa mchango wake wa kipekee katika kuimarisha imani ya Kiislamu miongoni mwa vijana, kushiriki mazungumzo yenye kulingania dini ya Allah, na kuhamasisha maisha ya uadilifu.

Kwa juhudi zake, sheikh Fariq anaendeleza urithi wa familia yake huku akiunda njia yake mwenyewe kama mwanafikra na mlinganiaji wa Kiislamu wa kizazi kipya. Sheikh amefanikisha hayo yote bila kupuuzia shughuli nyingine za kijamii na burudani. Anatajwa kuwa ni mwanamichezo mahiri pia katika soka, kuogelea, karate, judo na  hata taekwondo.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button