Zanzibar na Tanzania Bara ziko tayari kumpokea mhadhiri wa kimataifa, Dkt Zakir Naik, ambaye anategemewa kutua nchini Jumatatu Desemba 30 kwa ziara ya kidaawah, ikiwa ni mara ya kwanza Tanzania.
Ziara ya nguli huyo wa daawah nchini imepewa jina la Kongamano la Amani ambapo kauli mbiu yake inasema “Jesus and Mohammad are brothers in faith’ (Isa na Muhammad [amani iwe juu yao] ni ndugu katika imani).”
Katika ziara yake itakayomfikisha pia Dar es Salaam, Dkt Naik ambaye ni msomi mahiri, mzoefu katika nyanja ya dini linganishi (comparative religion) anaambatana na mkewe ustadhat Farhat Zakir Naik na mwanawe sheikh Fariq Zakir Naik ambao nao ni walinganiaji wenye uzito mkubwa kimataifa.
Kwa huko Zanzibar, wahadhiri hao wanatarajiwa kuwasilisha mada katika makongamano mawili, moja likiwa ni kwa wanawake pekee.
Katika tukio la kwanza litakalofanyika Januari 31 katika viwanja vya Masjid Jamiu Zanzibar, Mazizini kuanzia saa moja na nusu asubuhi, Mufti Mkuu wa Zanzibar, sheikh Saleh Omar Kaab ataongoza mamia ya Watanzania kumsikiliza Dkt Zakir Naik atakayetoa mada kuhusu Elimu kwa ajili ya Dunia zote mbili (Education for both the worlds).
Kabla ya Dkt Naik kuongea, mwanawe sheikh Fariq Naik atatangulia kwa kuwasilisha mada juu ya Qiyaamullayl, Sunna muhimu zaidi baada ya zile za faradhi.
Naye ustadhah Farhat, mkewe Dkt Naik atakuwa na kongamano hukohuko Zanzibar kwa ajili ya wanawake pekee litakalofanyika Januari 1 katika ukumbi wa mikutano wa Sheikh Idris Abdul Wakil ulioko Kikwajuni. Baada ya tukio hilo, wageni hao wanatarajiwa pia kutembezwa katika maeneo kadhaa ya vivutio vya utalii.
Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, sheikh Khalid Ali Mfaume, akizungumza kwa njia ya simu na Gazeti Imaan amesema maandalizi yote muhimu yamekalimika ikiwemo kualika viongozi waandamizi wa kidini, kiserikali na kijamii huku akiwataka Watanzania kuhudhuria kwa wingi ili kujiongezea maarifa ya dini.
Mtendaji huyo wa juu katika Ofisi ya Mufti amesema ujio wa Dkt Naik ni fursa kwani wahadhiri wa Tanzania watajifunza mambo muhimu sanaa ya ulinganiaji kutoka kwake, akisisitiza kuwa ni mwanazuoni mwenye uzoefu mkubwa, anayekubalika na mwenye mafanikio duniani.
“Kwetu sisi ni fahari viongozi wakubwa wa kidini kufika hapa Zanzibar. Mtakumbuka tulikuwa na ugeni kutoka Zimbabwe wa Mufti Menk alifika hapa na dunia iliona. Siku ya Jumanne, Disemba 31, 2024, tutakuwa na Dkt Naik. Dunia itaona kupitia chaneli ya Peace TV na za hapa nyumbani,”
alisema sheikh Mfaume
Akitaja faida zaidi za ujio wa viongozi hawa sheikh alisema wazawa watajifunza, wananchi wataona wahadhiri wapya na wa kimataifa na pia idadi ya watalii kutoka nchi jirani watafika Zanzibar na hivyo kuongeza faida za kiuchumi, .
Pia, alisema nchi itafuatiliwa sana huko mitandaoni katika vituo vya luninga hasa miongoni mwa Waislamu watakaotaka kujua Dkt Naik ana ujumbe gani kwa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Matukio ya Dar es Salaam
Ratiba iliyotolewa na The Islamic Foundation (TIF) taasisi inayoratibu ziara hiyo ya Dkt Naik, na taarifa za ziada kutoka kwenye kurasa za kijamii za mitandao ya kijamii ya Dkt Naik na sheikh Fariq,, baada ya Zanzibar, mgeni huyo na ujumbe wake wataelekea Dar es Salaam ambako Januari 2, 2025 kutakuwa na kongamano katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Katika tukio hilo la Diamond Jubilee, litakalofanyika kuanzia saa 12 jioni hadi saa tano usiku, Sheikh Naik anatarajiwa kuhudhurisha mada isemayo “Nini malengo ya maisha yetu?” akitanguliwa na mhadhara wa sheikh Fariq Naik kuhusu nafasi ya Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kama mkombozi wa ubinadamu.
Funga kazi itakuwa ni Januari 5, ambapo maelfu ya Waislamu watamshuhudia Dkt Naik katika uwanja wa michezo wa Benjamin Mkapa ambapo atazungumza kuhusu mfanano kati ya Uislamu na Ukristo. Kabla ya Dkt Naik, mwanawe sheikh Fariq atatangulia kupanda jukwaani kutoa mada kuhusu Qur’an na Sayansi. Matukio hili kubwa linatarajiwa kuanza saa 12 asubuhi ambapo yatarushwa mubashara kupitia Luninga za Peace TV, Imaan TV, ZBC2 na nyingine.
Kwa upande wake, Januari 4, ustadhat Farhat atakuwa na mhadhara wa wanawake pekee utakaofanyika katika ukumbi wa New Library ulioko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Tayari Dkt Naik na Sheikh Fariq kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii ikiwemo YouTube wamewahakikishia Waislamu na Watanzania wote wa imani zote kuwa wanatarajia kufika hapa nchini hiyo Disemba 30, 2024, inshaAllah, na kuwaomba kuhudhuria kongamano hilo kwa wingi.
“Naitwa Dkt Naik, InshaAllah hivi karibuni nitakuja Tanzania, ardhi ya Kilimanjaro na Zanzibar. InshaAllah nitafika Disemba 30, 2024 kuhudhuria Kongamano la Amani linaloandaliwa na ofisi ya Mufti Zanzibar na Taasisi ya The Islamic Foundation TIF