
Tujiandae, kifo huja ghafla, mahali popote
Abdullahi bin Mubaarak (Allah amrehemu) amesimulia kwamba, wakati Abu Huraira (Allah amridhie) alipoumwa maradhi yake ya mwisho alilia sana, akaulizwa: “Ni kitu gani kinachokuliza ewe Abu Huraira?” Akasema: “Kwa hakika mimi sililii hii dunia yenu, bali kinachoniliza ni umbali wa safari yangu na uchache wa masurufu yangu. Hivi sasa nipo katika ngazi ya kuteremka – ima Peponi au Motoni na sijui ni wapi kati ya sehemu mbili hizi nitapelekwa.” [Taz: ‘Ibn Sa’ad katika Twabaqaat, na Bukhari katika Taariykhul – Kabiir’].
Mafundisho ya tukio hili
Kifo ni miongoni mwa matukio yenye kutisha, ambayo wengi wetu tumeghafilika nayo. Hakika hii ni safari inayohitaji masurufu (matumizi), hivyo mtu anatakiwa kujiandaa nayo kwa kufanya matendo mema yatakayomfaa katika maisha yajayo huko Akhera.
Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametuusia kukikumbuka kifo mara kwa mara kwa kuwa kinakata ladha ya maisha haya ya dunia na kumfanya mja awe ni mwenye kukumbuka maamrisho ya Allah, kujiepusha na aliyoyakataza na kuchunga mipaka aliyoiweka. Mtume ametwambia: “Kithirisheni kumkumbuka mkata ladha, yaani kifo.” [Tirmidhi].
Uhalisia wa maisha yetu
Tukijaribu kufananisha maisha yetu na yale ya wema waliotangulia tutaona tofauti kubwa mno. Abu Huraira, mmoja wa Masahaba waandamizi wa Mtume (rehema na amani zimshukie) alifanya mambo mengi ya kumpa matumaini ya kupata Pepo lakini hofu ilimjaa huku akijiuliza ameandaa nini kitakachomfaa baada ya kufa.
Hali hii ni tofauti kabisa na sisi Waislamu wa sasa, kwani tulio wengi maisha yetu yamejaa udanganyifu, uzembe na kasoro kubwa. Kibaya zaidi hatuna habari na kifo na wala hatufanyi maandalizi ya kutosha. Wengi hatufanyi matendo mema ambayo ndiyo msingi wa matumaini na usalama katika safari hii nzito.
Hata tunapokuwa msibani, wengi wetu hatujumuiki kwenye ibada ya kumsalia maiti licha ya ukweli kuwa ni ibada yenye ujira mkubwa. Baadhi yetu tunahisi hatuwajibiki kumsalia maiti kwa sababu ni faradhi ya kutoshelezana.
Aidha miongoni mwetu tumekuwa tukisindikiza jeneza huku tukizungumzia mambo ya soka, siasa na mipango mbalimbali ya kupata pesa. Hili ni kosa kubwa ambalo masheikh na walinganiaji wanapaswa kulikemea kwa nguvu zote.
Tujiandae na Akhera kwa kufanya mema na kuepuka maovu
Dunia ni shamba la kupanda mazao, ambayo mavuno yake yatapatikana kesho Akhera. Hivyo tuna kila sababu ya kutumia muda wetu, nguvu zetu, afya na mali zetu kuwekeza katika shamba hili ili tupate mavuno yenye tija Siku ya Kiyama.
Usiwe na matarajio ya kuvuna thawabu Siku ya Kiyama ilihali huna unachokifanya katika shamba hili la dunia. Ni muhimu tutubie kwanza makosa yetu na kumuomba Allah msamaha huku tukiendelea kufanya istighfar kila mara. Kisha tujipambe kwa matendo mema katika kauli na matendo yetu.
Tujiandae vyema na Siku ya Kiyama kwani hakuna cha kutufaa siku hiyo isipokuwa amali njema tulizozifanya hapa duniani.
Tusibezane wala kunyoosheana vidole
Haipasi Muislamu kumnyooshea ndugu yako kidole wala kukadiria siku atakayokufa hata kama anaugua maradhi yasiyotarajiwa kupona, kwani unaweza kutangulia wewe kufa na kumuacha huyo unayemuuguza. Vivyo hivyo mtoto anaweza kufa kabla ya mtu mzima, kadhalika kijana anaweza kufa kabla ya mzee.
Hayo ni makadirio ya Allah na mipango yake ambayo hakuna wa kupingana nayo. Kila tunapowasindikiza wenzetu makaburini, basi tukumbuke kuwa safari kama hiyo inatungoja. Vifo vya wenzetu viwe ni somo kwetu na sehemu ya mabadiliko katika kuyakimbilia mema na kudumu katika kukikumbuka kifo, kwani kadiri siku zinavyokwenda ndivyo kifo kinavyotusogelea.