
Magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele bado yanatesa wengi
Januari 30, kila mwaka ni siku ya kimataifa ya magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele au kwa Kiingereza “Neglected tropical diseases (NTDs).”
Magonjwa hayo ni mengi, ikiwemo usubi, ukoma, kichocho, donda ndugu, kuumwa na nyoka, na matende, mabusha, vikope au trakoma, malale, chaga, chikungunya, minyoo ya tumbo, usubi na donda ndugu.
Habari njema ni kuwa magonjwa haya yana tiba na kinga na kuna baadhi nchi zilishayatokomeza baadhi yao.
Maradhi haya husababishwa na aina tofauti za vijiumbe maradhi kama vile virusi, bakteria, vimelea, minyoo, kuvu na sumu. Vijiumbe maradhi hivi vinapompata binadamu husababisha madhara kwenye sio tu afya yake kupitia magonjwa, bali pia kiuchumi na kijamii.
Maeneo rafiki kwa NTDs
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, linasema NTDs huathiri zaidi jamii maskini kwenye maeneo ya kitropiki, vijijini, kwenye mizozo na maeneo yasiyofikika kirahisi ambako huduma za maji safi na za afya hupatikana kwa shida, hazitoshelezi au haziko kabisa.
Maradhi haya pia yanashamiri pia kwenye maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi, ambako upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na huduma za kujisafi ni shida. Hata hivyo, baadhi ya NTDs hupatikana katika maeneo mengine yasiyo ya kitropiki.
Kwa nini yasiyopatiwa kipaumbele?
Yanaitwa maradhi yasiyopatiwa kipaumbele kwa sababu kihistoria kwenye ajenda ya magonjwa duniani, yamekuwa yakipatiwa nafasi ya chini, na hata kama yakiwekwa juu, ufadhili bado ni changamoto.
Mathalani, malale, husababishwa na kung’atwa na mbung’o. Kichocho na usubi ambao huhusisha pia mgonjwa kupata upofu husababishwa na minyoo na kuenezwa na nzi wanaozaliana kwenye vijito.
Licha ya kuwa na kinga, magonjwa haya husababisha vifo vya maelfu ya watu kila mwaka. Hadi mwishoni mwa mwaka 2023, watu waliokuwa wanahitaji tiba angalau kwa aina moja ya ugonjwa wa NTDs walikadiriwa kuwa bilioni 1.5.
Nchi zinazoendelea, kila mwaka hugharimika mabilioni ya dola kutibu magonjwa haya yenye kinga. Uzalishaji kazini na tija vinapungua na familia kutumia kipato kwenye tiba badala ya kujiendeleza.
Kijamii kuna ubaguzi na unyanyapaa kwa wagonjwa na hivyo kushindwa kufikia ustawi wao ikiwemo kielimu. Magonjwa haya pia husababisha vifo na ulemavu.
Kinga, tiba dhidi ya NTDs
WHO inasema magonjwa ya NTDs yote yana kinga na hivyo yanaweza kudhibitiwa na kutokomezwa. Mathlan, mwaka 2024 nchi 7 zilitokomeza kabisa aina moja ya NTD ikiwemo Togo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hadi Desemba mwaka 2024, nchi 54 zilifanikiwa kutokomeza angalau aina moja ya NTDs, ikiwa ni zaidi ya nusu ya lengo la WHO la kutaka nchi 100 ziwe angalau zimetokomeza ugonjwa mmoja wa NTDS ifikapo 2030. Nchi kadhaa zimetokomeza aina 2, 3, au 4 za NTDs.
Wenye uhitaji hawafikiriwi
Mwaka 2023, zaidi ya watu milioni 860 walipatiwa tiba dhidi ya NTDs kupitia kampeni za utoaji dawa au usimamizi wa tiba kwa mgonjwa mmoja mmoja. WHO inasema bado kuna pengo, na licha ya kuwepo kwa tiba, mara nyingi wanaohitaji dawa husika hawafikiwi.
Dawa dhidi ya NTDs zinatolewa na kampuni 12 za kutengeneza dawa kupitia mgao wa kimataifa wa dawa.
Kati ya mwaka 2011 na 2024, takribani vidonge na chupa za dawa bilioni 30 vilisambazwa kwa matibabu.
Changamoto na mikakati
Ujio wa COVID-19 ulivuruga tiba na huduma za tiba kwa NTDs. Hata hivyo, hivi sasa mipango inaendelea kurejesha utekelezaji wake.
Mwaka 2020 WHO ilichapishwa Mkakati wa NTDs wa 2021-2030 ili kuhakikisha magonjwa hayo yanadhibitiwa na yanatokomezwa ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo kutokana na uwekezaji hafifu, malengo yaliyowekwa yakilandana na Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, yako hatarini kutofikiwa.
Changamoto ni pamoja na kubadilika kwa mfumo wa ufadhili, nchi husika kutomiliki kikamilifu mipango ya utokomezaji NTDs, ukosefu wa utaalamu, dawa, mbinu za uchunguzi, vifaa na ugumu wa kukusanya takwimu.
WHO inapendekeza mikakati mitano ya kuchagiza kinga, udhibiti na kutokomeza NTDs kubuni na kuimarisha mbinu za usimamizi wa magonjwa, tibakinga kupitia mionzi, kudhibiti mazalia ya vimelea vya wadudu na kuimarisha afya ya umma ya wanyama.
Mapendekezo mengine ni kuhakikisha kuna huduma ya maji safi na huduma za kujisafi na usafi.
Ni katika muktadha huo ndio maana katika siku ya NTDs Januari 30, 2025, WHO inataka kila mtu, wakiwemo viongozi na jamii kuungana, kuchukua hatua na kutokomeza magonjwa yasiyopatiwa kipaumbele, NTDs.