
Kusherehekea Valentine ni kunajisi Uislamu wako
Ni siku ya kuzini na kunywa pombe kwa wingi! Ndivyo unavyoweza kuielezea sikukuu ya wapendanao au ‘Valentine’s day’ inayoadhimishwa Februari 14 ya kila mwaka. Sikukuu hii ambayo chimbuko lake ni karne ya tatu huko Roma huadhimishwa na tawala zote zisizo za kiislamu duniani.
Katika sikukuu hii, watu wengi duniani kote watakuwa wakitoleana salamu za Valentino, kupeana mawaridi mekundu (Red Roses), kubadilishana maneno ya mapenzi, kucheza muziki, na kwa wale walio katika ndoa ndiyo msimu wa kukumbuka mapenzi yao.
Kwa walio wengi, sikukuu hii imekuwa chanzo cha kufanya maasi, na miongoni mwa hayo ni unywaji wa pombe na uzinzi. Ukitaka kuthibitisha hili tembelea nyumba za kulala wageni (Guest houses), nyingi utakutana na bango lililoandikwa ‘vyumba vimejaa!’
Matokeo yake wasichana wengi hujuta baada ya kujikuta wamebeba mimba wasizotarajia na hata kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwamo Ukimwi.
Inasikitisha kuona baadhi ya Waislamu wakiwamo wanandoa, nao wanaihesabu siku ya Februari 14 kama ‘Siku ya Wapendanao’ eti siku ya kuhuisha mapenzi baina yao. Hakika huu ni ujinga uliopitiliza, kwamba eti kuna siku maalum ya watu kupendana.
Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) ametuonya kwa kusema: “Mtafuata desturi (mwenendo) za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua hata kama waliingia katika shimo la mbulukenge, na nyinyi mtaingia pia.” Wakasema (Maswahaba): “Ewe Mtume! Unamaanisha Mayahudi na Manasara?” Akasema: “Nani wengine kama si wao.” [Bukhari na Muslim].
Kwa hakika sikukuu ya wapendanao haimo katika upendo uliobainishwa na Uislamu, bali ni katika itikadi za dini ya Kinasara na malengo yake ni batili. Na Mtume hakuziunga mkono sikukuu za makafiri na za kijahili.
Na katika sifa za waja wa Allah Aliyetukuka ambao amewasifu nazo katika Qur’an ni kwamba wao hawashuhudii uzushi, na wala hawahudhurii pumbao na burudani za haramu. Allah Aliyetukuka anasema: “Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uongo, na pindi wapitapo kwenye upuuzi, hupita kwa heshima yao.” [Qur’an, 25:72].
Kwa kuzingatia hayo, inatubainikia wazi kuwa sikukuu ya Valentine si sikukuu ya Waislamu, bali ni sikukuu ya wapagani wa Kinasara. Hivyo basi haifai Kisharia kujumuika nao katika kusheherekea sikukuu hii au kuwa na alama au ishara inayofahamisha kuunga mkono sikukuu hii.
Asili ya sikukuu hii
Chanzo na asili ya sikukuu ya wapendanao (Valentine’s Day) ni wapagani wa Roma ambapo mmoja katika wafalme wao alikataza wanajeshi wake wasioe kwa hoja kuwa watakapooa akili zao zitafungamana zaidi na familia zao na hivyo kuzorotesha ushiriki wao mzuri katika medani ya vita.
Baada ya kutolewa amri hiyo ya Mfalme wa pili wa Warumi wa kale, aliibuka Kasisi wa Kinasara aitwae Valentino na kupinga amri ya Mfalme, na akawa anahamasisha watu kufunga ndoa kwa siri.
Habari hii ilimfikia Mfalme, ambaye aliamuru Valentino akamatwe na kufungwa gerezani. Akiwa gerezani, Valentino alikutana na binti mmoja ambaye naye alikuwa mfungwa, akampenda. Valentino alihukumiwa kunyongwa kutokana na kupinga amri ya Mfalme wa Warumi, lakini kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo alimpelekea kadi ya upendo binti mfungwa aliyetokea kumpenda kule gerezani.
Kadi hiyo iliandikwa hivi: “Kutoka kwa mtu mwenye upendo wa kweli Valentino.” Hukumu ya kunyongwa kwake ilikuwa tarehe 14 Februari mwaka wa 270 baada ya kuzaliwa Masihi, na ndiyo maana siku hiyo ikatangazwa rasmi kuadhimishwa kila mwaka kwa ajili ya kumkumbuka.
Na kuanzia hapo Valentino akapewa jina la Mtakatifu ilihali alikuwa Kasisi kabla hata ya kupewa utakatifu huo. Walifanya hivyo kwa madai kuwa Valentino aliukomboa unasara kwa kutoa roho yake, na alisimama kidete kutetea watu wanaopendana.
Katika siku hii, kwa mujibu wa itikadi yao, vijana wa kike na wa kiume hujishughulisha kwa kubadilishana maua na mawaridi, barua na kadi za upendo. Watu wa Magharibi wakiwemo Wamarekani na watu wa Ulaya huichukulia sikukuu hii kama sehemu ya kuhamasisha kufanya ngono kwa kiwango kilichopetuka mipaka.
Vipi basi Waislamu tunajitumbukiza katika sherehe ambazo zinakinzana na itikadi yetu ya Kiislamu! Tumekwishajua sasa kuwa siku iitwayo ‘Valentine Day’ asili yake ni uzushi, shirk na upotofu wa wazi – hivyo ni haramu kwetu. Ni wajibu wetu kujiepusha sisi na vizazi vyetu kushiriki katika sikukuu hii ya kijahili. Na kwa sababu Waislamu wengi hasa vijana kwa namna moja ama nyingine husherehekea siku ya wapendanao, itapendeza sana Maimamu wa misikiti, Masheikh na walinganiaji waukumbushe umma juu ya uharamu wa inayoitwa ‘Sikukuu ya Valentine’ na wala wasisubiri ifike Februari 14 ndiyo waanze kuwalingania watu.