
Upo umuhimuwa kujiandaana Ramadhan
Wakati tukiukaribia mfungo wa mwezi wa Ramadhan, kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kujiandaa kwayo kabla ya kufikiwa na mwezi huo Mtukufu. Sote tunafahamu kwamba Ramadhan ni msimu wa kujikurubisha kwa Allah, na kwa sababu hiyo tunatakiwa kujiandaa vizuri kuupokea mwezi huu wenye fursa kemkem za ibada.
Waislamu tunatakiwa kutumia fursa ya siku zilizobaki kuzizoesha nafsi zetu katika kufanya ibada na mambo mbalimbali ya kheri ili ikifika Ramadhan tuwe wepesi wa kutekeleza ibada.
Kama sote tujuavyo, Ramadhan ni fursa kubwa kwa Waislamu wote duniani kurudi kwa Mola wao na kutafuta radhi na thawabu kutoka kwake. Kwa hiyo, kabla ya kufikiwa na msimu huu wa kheri ni muhimu tufanye maandalizi makubwa ya kimwili na kiroho. Mwezi wa Ramadhan ni mfano wa soko la kheri ambalo Muislamu anatakiwa kulitumia vizuri kwa ajili ya manufaa yake hapa duniani na kesho Akhera.
Ramadhan ni mwezi Mtukufu, ambapo ndani yake milango ya Pepo inafunguliwa na milango ya Moto inafungwa. Ni mwezi ulio bora kuliko miezi mingine. Katika mwezi wa Ramadhan, Allah Aliyetukuka huwaneemesha waja wake kwa kuwafungulia mlango wa matarajio kwa kuachwa huru na Moto.
Ikiwa Allah Aliyetukuka anawaacha huru waja wake na Moto kila usiku miongoni mwa siku za Ramadhan, basi yapasa tujitayarishe kwa ajili ya mwezi huu na kujiandaa kuupokea kwa amali njema, na siyo kuupokea kwa kufanya maasi.
Mwezi bora kuliko yote
Allah Aliyetukuka ameuelezea mwezi mtukufu wa Ramadhan kama mwezi bora kuliko miezi yote kwa kuwa Qur’an imeteremka ndani ya mwezi huu. “Mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa humo Qur’an ili iwe muongozo kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi.
Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na ambaye ni mgonjwa au yuko safarini, basi atimize hesabu katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hesabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.” [Qur’an, 2:185].
Pia, mwezi huu una usiku ulio bora kuliko miezi elfu moja, nao ni usiku wa Al–Qadr, kama anavyobainisha Allah: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’an katika Laylatul Qadri (Usiku wa cheo).” [Qur’an, 97:1].
Enyi waja wa Allah, jiandaeni kuupokea mwezi wa Ramadhan kwa kumcha Mwenyezi Mungu, kufanya vitendo vya utiifu na ibada kwa wingi na kukaa mbali na maovu. Tuelewe kuwa, ndani ya mwezi huu, malipo ya amali njema huongezeka; lakini vile vile malipo ya amali mbaya. Kufunga mchana wa Ramadhan ni wajibu na kusimama kwa ibada usiku ni sunna yenye kukamilisha faradhi. Ukifunga kwa imani na kutaraji malipo, utasamehewa madhambi yaliyotangulia.
Swaumu ni ibada ya pekee
Hakika swaumu ni ibada ya pekee ambayo Mola amejihusishia mwenyewe, kama alivyosema Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) katika hadith ya Bukhari aliyoipokea kutoka kwa Abu Huraira kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Amali zote za binadamu ni zake isipokuwa swaumu. Hakika ya swaumu ni yangu na Mimi ndiye nitakayeilipa, na swaumu ni kinga. Ikiwa ni siku ya mmoja wenu kufunga basi ajiepushe na kufanya jimai, wala asiseme maovu (asibishane na watu).
“Na atakapotukanwa na yeyote au akataka kupigana naye basi amwambie: ‘Mimi nimefunga.’ Naapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake, harufu ya kinywa cha mmoja wenu ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski. Na mwenye kufunga ana furaha mbili: Moja huipata akifungua swaumu, na ya pili ni wakati atakapokutana na Mola wake.”
Ewe mja wa Allah, itakapofika Ramadhan jipinde kwa ibada kwani usipofanya hivyo utakuwa mbali na rehema za Allah Aliyetukuka. Muislamu unatakiwa kutumia fursa ya kupata maghfira na radhi za Mwenyezi Mungu ndani ya mwezi wa Ramadhan kwa kuwajibika katika kutenda mema na kuepukana na maovu.
Pia, miongoni mwa mambo unayotakiwa kufanya wakati unajiandaa kuupokea mwezi wa Ramadhan, ni kujenga uhusiano mwema baina yako na Allah, vilevile kujenga uhusiano mzuri na ndugu, jamaa, marafiki na jamii kwa ujumla kwa kuwa mwezi huu unahitaji mtu mwenye moyo safi, nia njema na hali nzuri kitabia, kiimani na kisaikolojia.
Mtume (rehema za Allah na amani iwe juu yake) na Maswahaba zake (Allah awaridhie wote) walikuwa wakiupokea mwezi wa Ramadhan kwa furaha na shauku ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza ibada za faradhi na za sunna, miongoni mwa amali njema na matendo mazuri. Hivyo, nasi tunatakiwa tuige mfano wao katika hili. Nafasi bado tunayo ikiwa tuna nia ya kuiga mwenendo wa Mtume wetu na wema waliotangulia.