
Utafiti: Kujitolea kunapunguza kasi kuzeeka
Utafiti mpya umegundua kuwa kujitolea, hata kwa saa moja tu kwa wiki, kunaweza kusababisha ‘kuzeeka polepole kibaolojia,’ haswa miongoni mwa wastaafu.
Umri wa kibaolojia hujulikana kwa kupima umri wa seli na tishu zako, na huonyesha jinsi uzee wako ulivyo polepole au haraka ikilinganishwa na umri wako wa mpangilio wa miaka ya kuzaliwa.
Wataalamu wanasema kujitolea kunaweza kukusaidia kuishi maisha marefu kwa sababu ya mchanganyiko wa manufaa ya kimwili, kijamii na kisaikolojia, nami naongeza pia kiroho.
Utafiti huo, uliopangwa kuchapishwa katika toleo la Januari la Sayansi ya Kijamii na Tiba (Social Science & Medicine), uligundua kuwa kujitolea – hata kwa saa moja tu kwa wiki – kunahusishwa na kuzeeka polepole kwa kibaolojia, ambayo inaonyesha umri wa seli na tishu zako ikilinganishwa na umri wako halisi
Watafiti walidhibiti vigezo vingine vya kiafya ambavyo vinaweza kupunguza kasi ya kuzeeka kwa kibaolojia-ikiwa ni pamoja na mzunguko wa shughuli za kimwili, hali ya kuvuta sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, unene wa kupindukia, na zaidi-na bado wakapata uhusiano kati ya kujitolea na kuzeeka polepole kwa kibayolojia.
Kiungo kati ya kujitolea na uzee wa kibiolojia
Watafiti walichanganua data kutoka kwa Wamarekani 2,605 wenye umri wa miaka 62 na zaidi. Walikagua ni mara ngapi washiriki walijitolea, wakabainisha ikiwa walikuwa wakifanya kazi au walistaafu, na wakabainisha umri wao wa kibaolojia kwa kutumia zana za hali ya juu kupima kuzeeka katika kiwango cha seli.
Matokeo yalionyesha kuwa watu waliojitolea kwa muda wa saa moja hadi nne kwa wiki walipata uzee wa polepole wa kibaolojia ikilinganishwa na wale ambao hawakujitolea kabisa. Wastaafu walionekana kufaidika zaidi, na uhusiano mkubwa kati ya kujitolea (hata kwa saa moja ya kujitolea kwa wiki) na kuzeeka polepole kuliko wafanyakazi wanaoudumu sasa.
Pia, kadiri mtu anavyojitolea zaidi, ndivyo athari za kiafya zinavyozidi kuwa wazi. Kujitolea zaidi ya saa nne kwa wiki kulihusishwa na upunguzaji mkubwa zaidi wa kasi ya kuzeeka (umri wa kibaolojia) bila kujali hali ya kazi ya mtu.
Hii inalingana na utafiti wa awali unaoonyesha kuwa kujitolea kunaweza kupunguza vifo miongoni mwa watu wazima. Utafiti wa 2023 ulitumia mbinu sawa na hiyo kuangalia athari za kujitolea kwenye uzee wa kibaolojia na pia iligundua kuwa kujitolea kulihusishwa na uzee wa polepole wa kibaolojia. Utafiti mpya uligundua tofauti za ziada kati ya watu waliostaafu na wanaofanya kazi.
Hata hivyo, utafiti unatajwa kuwa na mapungufu. Inaelezwa kuwa ili kujitolea, lazima uwe na afya njema, lazima uwe na wakati na lazima uwe na mapato – mambo hayo matatu huenda ndio sababu kutozeeka kuliko suala la kujitolea kama lilivyotajwa. Wote wanaojitolea wana haya mambo matatu na wasiojitolea hawana. Je huenda hizi ndio sababu hasa za kutozeeka?
Kujitolea kunawezaje kupunguza kasi ya kuzeeka?
Kwa nini kujitolea kuna athari kubwa kwa afya na maisha marefu? Wataalamu wanaelekeza kwenye mchanganyiko wa manufaa ya kimwili, kijamii, na kisaikolojia. Kwanza, kujitolea mara nyingi huhusisha shughuli za kimwili, kama vile kutembea, jambo ambalo huchangia kuimarisha afya kimazoezi.
Si hivyo tu, miunganisho ya kijamii pia ina mchango muhimu katika kupunguza kasi ya kuzeeka. Ukweli ni kuwa tunaishi katika jamii ambayo huwa hatuna uhusiano na wanajamii wenzetu jinsi tunavyopaswa kuwa. Kujitolea kunaweza kupelekea kuundwa kwa mtandao huo wa kijamii, jambo ambalo litaweza kupunguza msongo wa mawazo.
Ikiwa mtu amejitenga, anakuwa hana mazungumzo mengi na anakuwa hana uhusiano wa kihisia na wengine. Mazungumzo na uhusiano wa kihisia na wengine husaidia kuongeza muda wa kuishi. Kwa upande mwingine, kujitolea pia kunaweza kuboresha afya ya akili na hivyo kupunguza kuzeeka na kuongeza umri wa kuishi. Kujitolea kunaweza kumuinua mtu kisaikolojia na kumfanya mtu ahisi kama anajaribu kufanya kitu ili ulimwengu kuwa bora zaidi. Hii inasaidia kumfanya mtu aridhike moyoni.