
Kwa nini watoto wanadeka, wananungunika?
Moja kati ya changamoto ambazo wazazi wengi tunakumbana nazo ni tabia ya watoto kulalamika, kulia, kudeka na kuneng’eneka.
Kuna sababu chache za mtoto kunung’unika, kulia na kupaza sauti hadi zikawa zinasikika kama misumari kwenye bati kuliko yule mtoto wetu mtamu tuliyozoea.
Ni muhimu kutambua kwamba tabia hizi hutokea haraka sana, na bila uamuzi wa makusudi wa mtoto wako. Kama vile ambavyo wewe huamui kuwa na hasira, hata mtoto wako pia ni hivyohivyo.
Hata hivyo, aghlab, mtoto atajitahidi kupata mahitaji yake kwa wakati huu, na kwa bahati mbaya, katika mchakato huo, atanung’unika, atakuudhi na atalalamika. Sababu za hali hii ya mtoto kunung’unika zinaingia katika maeneo matatu.
Kwanza, mtoto hulia na kunung’unika kwa sababu anataka kuthibitishwa kuwa anasikilizwa na kuthaminiwa. Pili, mtoto anaweza kuwa anahitaji muunganiko na mzazi, aghlabu tunaita kutafuta ‘attention (kuzingatiwa).’ Tatu, mtoto anaweza kulia na kunung’unika ili kudhibiti hisia (kutaka msaada wa kutulizwa).
Tukianza na sababu ya kwanza, mtoto hutafuta kuthibitishiwa kuwa anapendwa na kuthaminiwa. Kila binadamu ana hitaji la asili la kutambuliwa na kuthaminiwa na hii ni pamoja na kusikilizwa kwa mawazo, hisia na matamanio yake na kutambuliwa na watu wazima wanaoaminika.
Pili, katika suala la kutafuta muunganiko, mtoto wako anahitaji uangalizi wako muda wote na jotojoto la mzazi.
Mtoto asipopata kiasi cha kutosha cha uzingatiwaji na jotojoto la mzazi, ufahamu wake mdogo utamfanya atafute muunganiko huo kwa njia yoyote ambayo ni rahisi zaidi, ikiwemo kilio, kunung’uika na kadhalika. Mtoto anafanya hivyo akielewa kuwa muunganiko hasi ni bora kuliko kukosa kabisa mahusiano na mzazi au mlezi.
Katika sababu ya tatu kuhusu sababu ya mtoto kulia, kulalamika, kusumbua mzazi ni kutafuta msaada wa udhibiti wa Hhsia. Kituo cha hisia cha mtoto wako bado hakijakomaa na hivyo bado atategemea sana walezi kumsaidia kudhibiti hisia zake.
Kunung’unika kunaweza kuwa njia ya mwisho ya mtoto ya kujaribu kukabiliana na kuzidiwa na hisia kabla ya kupoteza kabisa utulivu na kuingia kwenye hali mbaya zaidi.
Mbinu 4 za kumsaidia mwanao aache kunung’unika
Jambo moja la hakika ni kuwa njia ya kufokea, kubweka, kumtisha, pengine hata kumpiga ili ‘kumtuliza!’ haiwezi kuleta tija. Kwa vyovyote, kwa mtoto wa aina hii itabidi uzame ndani zaidi ili kupata mzizi wa tatizo.
Kwa bahati nzuri, kuna vidokezo vichache ambavyo vikifanyiwa kazi mara kwa mara vitatengeneza njia rahisi sana ya kuzuia manung’uniko, malalamiko na maudhi ya mtoto.
Hatua ya 1: Kuwa mchunguzi
Elekeza umakini wako kwa mtoto wako kwani ni kwa kufanya hivyo pekee ndio unaweza kugundua mtoto wako anaweza kuwa na hitaji gani la kuwasiliana.. Aghlab, mtoto (hususan asiyesema) halii tu bila sababu bali atalia ili kuwasilisha hitaji lake.
Mtoto asiyeweza kazi ya kujua hitaji lake ni ngumu kidogo. Unaweza kujaribu kuangalia pampas kama kachafuka au pengine ni joto linamsumbia anahitaji kuoga au pengine ni njaa na kadhalika. Mtoto mkubwa zaidi anaweza kuonesha kwa ishara wakati wale wakubwa wataingea moja kwa moja.
Hatua ya 2: Sikiliza na uthibitishe.
Chukua muda mfupi kusikiliza kile mtoto wako anajaribu kueleza na umjulishe kuwa unasikia (kama ni mtoto mkubwa anayeweza kuelewa) au kama ni mdogo mtekelezee.
Mara nyingi mtoto wako anataka tu kusikilizwa au pengine anataka mahitaji yake kuchukuliwa kwa uzito na baada ya hapo atakuwa na wakati rahisi zaidi wa kuvumilia hata jibu la “hapana” au “baadae”.
Hatua ya 3: Jambo mbadala
Kwa watoto wadogo, kuwapeleka katika jambo mbadala kama vile mchezo fulani wowote, kuimba qasida au kingine chochote kunaweza kusaidia kudumisha umakini wao na kuwaweka nje ya hisia hasi za kuchoshwa (boredom).
Ili hili ulifanye kwa ufanisi, jitahidi uwe na vfaa vingi vya michezo kwa ajili ya watoto ndani ya nyuma ikiwemo mipira, baiskali, ubao wa kuchorea na kuandika na kadhalika. Lakini muhimu zaidi ni kuwa mbunifu.
Hatua ya 4: Kuwa muainifu kwake. Ukijibu kwa utulivu na kwa uhakika kile mtoto wako anachozungumza huku ukizingatia kikomo chako cha kucheza nae, basi atapata mahitaji yake na wakati huohuo kujifunza kukuamini kwa hivyo hamu ya kulia na kusumbua itapungua.