Fahamu usyoyajua

Safia bint Huyay, mke wa Mtume kutoka jamii ya Kiyahudi

Maisha ya mitume na maswahaba

Allah alipomtuma Mtume aliyetokana na Waarabu wa Bani Hashim (Makureish) kwa watu, Wayahudi walichukia sana na nyoyo zao zikawaka moto wa husda na chuki. Matokeo yake, wakawatia  watu shaka juu ya ukweli wa utume wake na juu ya usahihi wa dini aliyokuja nayo, huku wakisema: “Mtume tuliyekuwa tukimsubiri si huyu Muhammad, na wala dini yake si hii aliyokuja nayo.”

Hatua nyingine waliyochukua ni kuvitafuta kwa juhudi vitabu vyao vilivyotabiri ujio wa Muhammad, wakabadilisha aya husika zilizomtabiri kwa jina, sifa au kwa ishara. 

Ikumbukwe kuwa sehemu kubwa ya mafunzo aliyokuja nayo Mtume yanakubaliana na yaliyokuja katika vitabu vyao vya Taurati na Injili. Lakini, utashi wa nafsi pamoja na tabia za Wayahudi za kujipendelea ziliwazuia kumkubali Muhamad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwani waliamini kwamba wao ni wabora kuliko wanadamu wote kwa sababu wao ni wana wa Mwenyezi Mungu, wateule na ni vipenzi vyake.” [Qur’an, 5:18].

Hivyo, kwa sababu wao ndio bora, basi hata Mitume wote wangeliteuliwa miongoni mwao tu, kwa mtazamo wao potofu. Walihoji: “Inakuwaje mtume leo ametokea katika jamii nyingine (ya Waarabu)?”

Basi jambo hilo la kumfuata Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) likawiwia uzito na hapo ndipo walipodhihirisha uadui, chuki na vitimbi juu ya Mtume tangu waliposikia habari zake akiwa Makka.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alipohamia Madina, Wayahudi haohao walikuwa wa kwanza kumkataa, na kuzidisha vituko vyao. Waliwaonya wafuasi wao kwa kuwaambia: “Wala msimuamini yeyote ila aliyefuata dini yenu…” [Qur’an, 3:73]. Hawakuishia hapo, bali waliwashawishi baadhi ya Waarabu waliokuwa wakiishi huko wawe wanafiki. Waliwaandaa kudhihirisha Uislamu na kuficha ukafiri ili wasaidiane nao katika kuupiga vita Uislamu.

Baada ya Mtume (rehma za Allah na amani zimshukie) kuiona khiana yao waziwazi, aliwataka wafunge mkataba wa amani utakaolinda haki ya kila upande na uhuru wa mtu kufuata dini aitakayo bila ya kubughudhiwa, na ambao ungeibakishia Madina na wakazi wake (licha ya tofauti zao za kiimani), amani ya kudumu.

Makubaliano hayo yalipitishwa, lakini haukupita muda mrefu, makhiana hao walivunja maelewano, na kuendeleza uadui wao dhidi ya Mtume na Waislamu, ikiwemo kufanya jaribio la kumuua (Mtume).

Qur’an ikamuelekeza naye awashughulikie kwa kuwapiga vita waziwazi. Inaeleweka kwamba, Wayahudi wa Madina waligawika katika makabila makuu matatu: Banu Qainuqa, Banu Nadhir na Banu Quraidha.

Mtume alianza na kabila la Qainuqa kwa kuwatoa Madina bila ya kuwaua (mwaka wa pili), kisha Banu Nadhir (mwaka wa nne). Ilipofika mwaka wa tano Hijriya na baada ya hila zao kuwa hatari zaidi kwa Waislamu, wanaume wa Banuu Quraidha walikamatwa  wakauliwa, na wanawake na watoto wakabaki mateka.

Tumetanguliza historia ya Wayahudi na hasadi yao dhidi ya Waislamu kwa sababu mzungumzwa wa makala yetu wiki hii anatokana na wao. (Wayahudi kutoka Bani Nadhir),  lakini Allah Mtukuka alimuonesha mwanga wa dini na akamjaalia kuwa miongoni mwa wake wa Mtume na mama wa Waislamu. Hata kisa chake cha kuolewa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kina uhusiano mkubwa na Wayahudi, kama tutakavyoona baadaye.

Nasabu na wasifu wake

Aliitwa Safia bint Huyai bin Akhtab bin Say’a. Ni katika vijukuu vya Lawi bin Ya’qoub bin Is-hak bin Ibrahim [Taz. Sahabiyaat hawla rasoul uk.224].  Safia ni mmoja wa wanawake waliosifikana kwa tabia njema tangu alipokuwa mdogo. Baba yake alikuwa kiongozi wa kabila lake na watu wote walimtii.

Safia alikuwa mwanamke mwenye akili pevu na mzuri wa umbo, kama anavyomuelezea Imamu Aldhabi [Siyar a’lam Anubalaa j2/231]. Kwao aliishi maisha ya fakhari sana. Safia alipokuwa tayari kuolewa, watu maarufu wa jamii yake walipigana vikumbo kwenda kumchumbia,  lakini bahati ikamuangukia Sallaam bin Abil-haqiqi. Bwana huyu  alipomuacha, aliolewa na nduguye Kinana bin Abil-haqiqi. Mabwana hawa walikuwa washairi mashuhuri sana katika kabila lao Bani Nadhir.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button