
Ugonjwa wa seli mundu: sababu, dalili na namna ya kuishi nao
Seli mundu ni ugonjwa wa kurithi unaoathiri chembe nyekundu za damu, na kuzipa umbo la mwezi au mundu badala ya kuwa duara.
Umbo hili lisilo la kawaida husababisha matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na kuziba kwa mishipa ya damu, kupungua kwa usafirishaji wa oksijeni mwilini, na maumivu makali. Ugonjwa huu ni wa kudumu na huathiri zaidi jamii za Afrika, Karibiani, Amerika Kusini, India, na Mashariki ya Kati.
Sababu za seli mundu
Seli mundu husababishwa na mabadiliko katika jeni ya hemoglobini, inayojulikana kama hemoglobin S. Hemoglobini ni protini inayopatikana katika chembe nyekundu za damu, ambayo inasaidia kusafirisha oksijeni mwilini.
Watu wenye jeni moja ya seli mundu (carrier) huwa hawana dalili kali lakini wanaweza kurithi jeni hiyo kwa watoto wao. Ikiwa mtoto anarithi jeni mbili za seli mundu kutoka kwa wazazi wote wawili, atakuwa na ugonjwa huu.
Dalili za Seli Mundu
Dalili za seli mundu hutofautiana kwa watu tofauti, lakini mara nyingi ni kali na zinaweza kuwa sugu. Hapa tutataja baadhi ya dalili hizo.
Maumivu makali (sickle cell crisis): Hutokea ghafla na kwa vipindi, hasa katika mifupa, viungo, tumbo, na mgongo. Maumivu haya yanaweza kudumu kwa masaa au siku kadhaa.
Upungufu wa damu (anemia): Chembe nyekundu za damu zenye umbo la mundu zinaishi kwa muda mfupi kuliko chembe nyekundu za kawaida, na hivyo kusababisha upungufu wa damu. Dalili zake ni uchovu, kupumua kwa shida, na ngozi kuwa na rangi ya njano (jaundice).
Uvunjaji wa chembe nyekundu: Mwili huharibu chembe nyekundu haraka, hali inayoweza kusababisha homa ya manjano na kuathiri ini.
Kuziba kwa mishipa ya damu: chembe nyekundu za damu zenye umbo la mundu hujikusanya na kuziba mishipa midogo ya damu, jambo linaloweza kusababisha kiharusi, matatizo ya figo, au uharibifu wa viungo vingine.
Maambukizi ya mara kwa mara: Watu wenye seli mundu wana kinga dhaifu ya mwili, hivyo wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi kama vile nimonia na homa ya uti wa mgongo.
Matibabu na namna ya kudhibiti seli mundu
Ingawa hakuna tiba ya uhakika kwa seli mundu, kuna njia kadhaa za kudhibiti dalili na kuboresha maisha ya wagonjwa. Dawa za Kupunguza Maumivu: Wagonjwa hutumia dawa kama vile ibuprofen na morphine ili kupunguza maumivu makali.
Matumizi ya dawa ya Hydroxyurea: Dawa hii husaidia kuongeza uzalishaji wa fetal hemoglobin ambayo huzuia seli nyekundu kubadilika kuwa umbo la mundu.
Uongezaji wa Damu: Wagonjwa wanaweza kupokea damu ili kuongeza kiwango cha ‘hemoglobini’ na kuzuia matatizo kama kiharusi.
Matibabu ya kinga: Chanjo kadhaa wa kadhaa na ‘antibiotics’ hutolewa ili kusaidia kupunguza hatari ya maambukizi.
Upandikizaji wa uboho: Hili ni chaguo la tiba pekee lenye uwezo wa kuponya ugonjwa wa seli mundu, lakini ni nadra kutokana na ugumu wa kupata wafadhili wa uboho unaofaa.
Namna ya kuishi na seli mundu
Wagonjwa wa seli mundu wanapaswa kuchukua tahadhari maalum ili kupunguza hatari ya kuzidiwa na dalili. Baadhi ya njia muhimu ni kunywa maji mengi kila siku ili kuepuka msongamano wa damu.
Njia nyingine ni kuepuka hali ya baridi kali au joto kali, kwani inaweza kusababisha shambulio la maumivu. Pia, ni muhimu kula chakula chenye madini ya chuma ‘folic acid’ ili kusaidia utengenezaji wa chembe nyekundu za damu.
Inashauriwa pia kufanya mazoezi mepesi na kuepuka uchovu wa kupita kiasi na vilevile kupata chanjo na kutumia dawa za antibiotics ili kuzuia maambukizi.
Hitimisho
Seli mundu ni ugonjwa wa kurithi unaoathiri maisha ya mamilioni ya watu duniani, hasa katika maeneo yenye watu wa asili ya Kiafrika. Ingawa hauna tiba ya uhakika, kuna njia mbalimbali za kudhibiti dalili na kuboresha maisha ya wagonjwa. Elimu kuhusu seli mundu ni muhimu kwa jamii ili kusaidia wagonjwa na kuzuia maambukizi kwa vizazi vijavyo kupitia upimaji wa jeni. Kwa wagonjwa wa seli mundu, matunzo ya kiafya na mtindo bora wa maisha ni muhimu kwa kudhibiti ugonjwa huu na kuishi maisha yenye ubora zaidi.