Fahamu usyoyajua

EMU: Ndege mwenye kasi ya ajabu kutoka Australia

Naam ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa safu hii, karibu tena katika makala hizi kuhusu viumbe mbalimbli wa Allah, Mbora wa uumbaji na anayejua kukadiria. Juma hili acha tukaone ukubwa wa Allah kwa kumtazama ndege anayefahamika kwa jina la emu.

Ndege huyu kutoka Australia ana umbo kubwa kiasi, mwili mnene na miguu miwili mirefu yenye vidole vitatu kila mmoja. Urefu wake kutoka kichwani hadi miguuni unafikia mita 1.9 sawa na futi 5 na anaweza kukua hadi kufikia uzito wa kilogramu 45.

Kimuonekano, emus wanafanana na mbuni karibu kila kitu, ingawa mbuni ni wakubwa zaidi na wana miguu yenye nguvu sana. Allah, Mbora wa uumbaji amewapamba ndege hawa kwa manyoya ya rangi ya kahawia. Maeneo yao ya shingo na kichwani wana rangi ya kijivu giza.

Uzazi na chakula

Majike ya emus huchukua takribani siku 60 (miezi miwili) kutaga mayai kati ya saba hadi 10 yenye rangi ya kijani kibichi. Mayai yao yana urefu wa sentimita 13 sawa na inchi tano. Ndege hawa hawana muda maalum wa kujamiiana, wao hukutana muda wowote na sehemu yoyote kwa ajili ya kupandana.

Kwa upande wa chakula, emus hupendelea kula mbegu, matunda, maua na mashina ya mimea. Pia, wanakula wadudu na wanyama wadogo wenye uti wa mgongo.

Ndugu yangu msomaji, yapo mambo mengi yanayomhusu emu ambayo huwezi kuyakuta kwa ndege wengine wa jamii yake. Inaelezwa kuwa emu ni ndege waharibifu na wenye hasira sana.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes, mnamo mwaka 1932 jeshi la Australia lilitangaza vita dhidi ya emus baada ya kufanya uharibifu wa mali na mazao mashambani katika mji wa Campion uliopo Magharibi mwa nchi hiyo.

Zao kuu lililokuwa linalimwa na watu wa mji huu ni ngano, lakini ndege hawa walikuwa wengi kiasi cha kuharibu mazao yote mashambani na kuwaacha wakiwa hawana chakula. Ili kutatua tatizo hilo, Serikali ya Australia ilipeleka wanajeshi wenye silaha za moto mashambani ili kupambana na ndege hawa waliokuwa wanatishia kuleta baa la njaa nchini humo.

Inaelezwa kuwa wanajeshi wengi wakiwemo waliostaafu waliingia mashambani kupambana na ndege hawa ambao idadi yao ilitajwa kufikia 20,000. Ajabu ni kwamba ndege hao walikuwa wanakimbia ili kukwepa risasi hali iliyowafanya wanajeshi kuwashambulia kwa kushtukiza, mbinu ambayo iliwawezesha kuwaua ndege wachache.

Kadiri ndege hao walivyokuwa wanapigwa risasi ndivyo idadi yao ilikuwa inaongezeka. Hakuna idadi kamili ya ni ndege wangapi waliuawa katika operesheni hiyo lakini inaelezwa kuwa waliuliwa ndege 900 kati ya 20,000.

Mambo 10 usiyoyafahamu kuhusu emu

Kwanza, emu ni ndege wa pili kwa ukubwa duniani baada ya mbuni.

Pili, ndege hawa wana tabia ya kumeza kokoto kubwa ili kuwasaidia katika mchakato wa umeng’enyaji wa chakula.

Tatu, wana seti mbili za kope; moja kwa ajili ya kupepesa macho na nyingine kwa ajili ya kuzuia vumbi.

Nne, emus na kangaroo hawawezi kutembea kwa kurudi nyuma, ndiyo maana wamewekwa kwenye nembo ya taifa ya nchi ya Australia.

Tano, ndege hawa wana miili mikubwa kiasi na mabawa madogo.

Sita, wana uwezo mkubwa wa kuruka juu, kuogelea na kukimbia kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa.

Saba, madume ya ndege hawa hulinda mayai na kuwasaidia majike kulea watoto wanaozaliwa.

Nane, wana uwezo mkubwa wa kupambana na maadui zao kwa kuwarushia mateke.

Tisa, pamoja na kwamba chakula chao hutokana na mimea, emus hawali nyasi kavu na majani yaliyokomaa. Kumi, umri wao wa kuishi ni miaka 20 wakiwa porini.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button