
Sauda binti Zum-a ni mke wa pili wa Mtume
Uadilifu katika ukewenza na maeneo yake
Kwa vile makala yetu iliyopita iligusa maisha ya ukewenza baina ya wake wa Mtume ambao ni Sauda na Aisha. Kwa msingi huo, tumependelea kumletea msomaji uchambuzi mfupi kuhusu utaratibu wa kuishi kiukewenza kwa mtazamo wa Uislamu.
Kwanza ifahamike kwamba, mhimili wa ndoa ya zaidi ya mke mmoja (ukewenza) ni kufanya uadilifu. Wanaohofia kushindwa kuwa waadilifu wametakiwa kubaki na mke mmoja tu. [Qur’an 4:3]. Na katika hadith tunajifunza kuwa, mwanamume yeyote atakayekuwa na wake wawili akamili (akazidi) upande wa mke mmoja, atakuja S0iku ya Kiama bega lake likiwa limeshuka, kama alama ya fedheha na kufeli.
Lakini ni vyema pia kujua maana na mipaka ya uadilifu huo na maeneo yake.
Uadilifu na mipaka yake
Uadilifu ni ile hali ya kufanya usawa katika utimizaji wa haki baina ya wake wawili au zaidi ya wawili. Mume anatakiwa afanye uadilifu (usawa) kwenye maeneo makuu manne yafuatayo: makazi, mavazi, kulala zamu na nafaqa (huduma za maisha)
Makusudio ya usawa katika makazi ni kwamba, mume anapaswa kumpatia kila mke makazi maalumu yanayokidhi haja ya maisha. Na ni haramu kuwaweka nyumba moja ila kwa ridhaa yao kwa sharti ya kuwa na vyumba tofauti vya kulala na vyoo. [Taz: Rawdhatu twaalibiin jz 8 uk 348].
Lakini sharia haimlazimishi kufanya usawa katika ukubwa ama uzuri wa nyumba anazowaweka wake zake bali jambo la msingi ni makazi yanayokidhi mahitaji ya kuipa heshima nyumba ya ndoa.
Kwa upande wa mavazi, inampasa kumnunulia kila mke mavazi stahiki kwa kadri ya haja yatakayotunza heshima na utu wake, zikiwemo nguo za kusalia, kutokea na za mapambo (za kuvaa akiwa ndani mwake), kwa kadri ya uwezo wa mume.
Huduma zinazokusudiwa hapa ni pamoja na chakula, matumizi, matibabu na mapambo. Wala si lazima mume kugawa sawa katika aina za vyakula, mavazi au mapambo bali jambo la msingi ni kutosheleza huduma hizo kwa mujibu wa haja na matakwa ya nyumba, pia pakizingatiwe uwezo wa bwana (mume).
Kwa mfano, si lazima mume kila anaponunua mchele kwa ajili ya nyumba kubwa anunue pia tena kwa kiasi hicho hicho kwa ajili ya nyumba ndogo hata kama huko bado kipo cha kutosha. Na kwa upande wa vitoweo, fenicha, nguo na mapambo ni hivyo hivyo.
Kulala zamu. Hii ni haki ya msingi ya kila mke. Kimsingi, wakati wa kugawa zamu ni usiku na kufuatiwa na mchana kwa ambao kazi zao ni mchana. Na kwa ambao hujishughulisha na maisha usiku kama vile walinzi, zamu zao ni mchana na kufuatiwa na usiku. [taz. Umdatu ssaalik uk 201].
Kuingia kwa mke asiye na zamu
Haifai kuingia kwa mke asiye na zamu, labda kwa haja kama vile kupeleka huduma ya chakula au kwa dharura kama kumuona mgonjwa lakini bila ya kukaa sana. Na iwapo atakaa sana, atapaswa kuulipa muda huo kwa mwingine.
Inakatazwa pia kufanya tendo la ndoa kwa mke asiye na zamu. Ama vitangulizi vyake kama kubusu na kugusa haikatazwi kwa mujibu wa hadith ya Aisha (Allah amridhie) pale aliposema: “Kila siku Mtume akitupitia sote, mke baada ya mwingine, humsogelea na kumgusa bila ya kumuingilia mpaka anaishia kwa mwenye zamu analala huko.” [Ahmad].
Iwapo ataingia kwa asiye na zamu (wakati wa zamu ya mwingine) na akamuingilia, atalazimika kulipa kiasi cha wakati alichokaa wala hapaswi kulipa tendo la ndoa.
Kugawa mapenzi na jimai
Mume hapaswi kugawa sawa mapenzi na tendo la ndoa baina ya wake zake ingawa kufanya hivyo inapendeza zaidi. Hii ni kwa sababu vichocheo vya mapenzi na visogezaji vya matamanio hutofautiana baina ya wanawake. Hii pia ndio maana ya kauli ya Allah: “Na wala kamwe hamtoweza kufanya usawa baina ya wanawake hata mkitamani sana (kufanya hivyo) basi msielemee kila muelemeo (upande mmoja) na kumuacha (mwingine) kama aliyetundikwa (hajijui kama ana mume ama mjane)…” [Qur’an, 4:129].
Ibn Abbas (Allah amridhie), katika kuiweka wazi aya hii, amesema: “Yaani katika mapenzi na tendo la kitandani” na hii ndio hasa maana ya kauli ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kwamba alikuwa akifanya usawa katika kugawa zamu huku akisema: “Ewe Allah, huu ndio (upeo wa usawa katika) mgao wangu kwa ninaloliweza, basi usiniadhibu kwa unaloliweza ambalo mimi siliwezi.”
Kugawa zamu iwe katika hali zote
Mume anapaswa kumlalia zamu mkewe katika hali zote, akiwa mzima au mgonjwa, akiwa katika tohara au yu ndani ya ada yake ya mwezi/ nifasi au kuwa kizee.
Ikumbukwe, lengo la kugawa zamu si kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa tu bali ni ile hali ya kuwepo katika nyumba ya ndoa na kumliwaza mke ili ajisikie kuwa yupo chini ya kivuli cha mume.
Katika hali ya safari
Iwapo mume anataka kusafiri na mmoja wa wake zake, patapigwa kura na kusafiri na atayeshinda katika kura hiyo. Pia, hatapaswa kulipa siku za safarini kwa mke aliyebaki. Na haifai kusafiri na mmoja bila ya kura au ridhaa ya mwingine.
Ikiwa mke mmoja ana vizuizi vya kusafiri, kwa mfano ni mwanafunzi, mfanyakazi, mgonjwa au kwa sababu nyingine yoyote, mume atalipa siku za safarini kwa aliyebaki. [taz: Almuhadhab uk 485].
Na iwapo mke atasafiri bila ya idhini ya mumewe au kwa idhini yake lakini kwa haja yake mwenyewe (mke), basi hatakuwa na haki ya kulipwa zamu zake. Na akisafiri kwa ruhusa au kwa haja ya mume (au yao pamoja), atalipwa siku alizokuwa hayupo. [taz: Manhaju twulaab jz 1 uk 121].
Tanbihi
Mosi, mume anatakiwa aanze kugawa kwa uadilifu mara tu baada ya kuwa na wake zaidi ya mmoja. Hivyo, si lazima kila anachomnunulia mke mtarajiwa, kumnunulia pia mke aliyetangulia. Lakini ni vyema kumfanyia wema kwa kumzawadia vitu vya kumliwaza.
Pili, iwapo nyumba moja mke ameondoka kwa sababu yoyote, sharia haimlazimishi mume kwenda kulala (kugawa zamu) lakini itafaa kufanya hivyo kwa malengo mengine kama vile ulinzi na kutunza watoto.
Kwa mrejesho wasiliana na mwandishi kwa namba 0773181494 WABILLAHI TAWFIIQ