Fahamu usyoyajua

Utambulisho wa Kiislamu na umuhimu wa lugha ya Kiarabu

Watafiti wengi wanaichukulia lugha kama kipengele cha utambulisho, na baadhi yao hiki ni kipengele muhimu sana cha utambulisho. Hilo ni kweli kwa kuwa utambulisho katika muundo na uwepo wake unazingatia utaifa.

Kwa sababu hii, haituingii akilini kumuona Mfaransa asiyezungumza Kifaransa, au Mjerumani asiyezungumza Kijerumani, lakini inatuingia akilini kumuona Muislamu akizungumza Kijerumani, Kifaransa au lugha nyingine yoyote.

Waislamu wengi leo hawazungumzi lugha yoyote kati ya hizo au nyinginezo zilizonasibishwa na mataifa mbalimbali, lakini bado wanabeba utambulisho ule ule, ambao ni wa Uislamu, na wanajitofautisha na wengine kwa ufahari.

Ama lugha – iwe sehemu ya utambulisho au la, kila mmoja anatambua umuhimu wake katika ushawishi inayoutoa kwa watu binafsi au makundi wakati wa kujenga mitazamo yao. Lugha ni ufunguo wa kufikia utamaduni na nyenzo ya kupata maarifa.

Allah ‘Azza wa Jallah’ amekichagua Kiarabu kama lugha ya Qur’an Tukufu, na kutokana na hilo ndiyo Kiarabu kikawa lugha ya Uislamu: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’an kwa Kiarabu ili mpate kuzingatia.” [Qur’an, 12:2]. “Hiki ni Kitabu kilichopambanuliwa aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanaojua.” [Qur’an, 41:3]. “Hakika Sisi tumeifanya Qur’an kwa Kiarabu ili mfahamu.” [Qur’an, 43:3].

Lugha ya Kiarabu ni muhimu sana kwa sababu, kupitia kwayo muunganiko na Allah ‘Azza wa Jallah’ unafanyika kupitia ibada mbalimbali, usomaji wa Qur’an au sala. Isitoshe, ndiyo ufunguo unaotuwezesha kuzifikia maktaba zilizojaa elimu kiasi kwamba tunathamini utajiri wake wa kiutamaduni.

Kupitia lugha ya Kiarabu, ufahamu pamoja na utambulisho unapanuka na kusaidia kuimarisha zaidi msingi wake. Wema waliotangulia waliinuka kupitia lugha hii na wakataka watu waisome.

Imesimuliwa kutoka kwa Ubayy Ibn Ka’ab (Allah amridhie) akisema: “Jifunzeni lugha ya Kiarabu kama mnavyojifunza Qur’an.” Imesimuliwa pia kutoka kwa Ubaydullah Ibn Ubayd Al–Kalaa’I kwamba, Umar bin Khattwab (Allah amridhie) mara kwa mara alikuwa akisema: “Someni Qur’an kwa sababu ipo katika Kiarabu.”

Na imesimuliwa kutoka kwa Ibn Abbas (Allah amridhie) akisema kuwa: “Iwapo huelewi sehemu ya Qur’an, basi itafute kwenye ushairi kwa sababu hii ni lugha ya Waarabu.” Imam Malik alipata kusema: “Iwapo mtu hakuelewa lugha ya Waarabu na akajaribu kuielewa Qur’an, basi ningemuadhibu.”

Lugha ya Kiarabu siyo somo tu ambalo mtu huchagua kulisoma, bali ni wajibu wa kidini ambao umma wa Kiislamu unafanya kosa kubwa pale inapoitelekeza lugha hii.

Chakula cha Muislamu hukamilika tu kwa lugha hii. Kuipuuza kunapelekea udhaifu katika ufahamu sahihi wa dini, na hiyo ndiyo sababu ya kuwepo aina zote za uzushi, upotoshaji na makosa.

Hii ndiyo sababu mtaalamu bobezi wa lugha, Ibn Jinn, anasema katika kitabu ‘Al-khasaes’, na maneno yake ni sahihi: “Wengi miongoni mwa wale waliokengeuka kutoka kwenye shariah, walikengeuka kwa sababu hawakuelewa makusudio kwa kuwa walikuwa dhaifu katika lugha hii tukufu na yenye heshima.”

Ningependa kuweka wazi kupitia mifano mahsusi kuhusu umuhimu wa lugha ya Kiarabu na haja ya Waislamu kuwa mahiri katika lugha hii.

Muujiza wa Quran

Qur’an Tukufu inabeba maana za msingi na maana nyingine za ziada ambazo zipo katika mifumo, mtindo wa uelezaji na nguvu ya ufasaha. Ufasaha na mitindo ya ajabu ya maana zake za ziada zinaweza tu kueleweka kwa yule aliye mahiri wa lugha katika maeneo yote hayo mawili, na yule anayetambua kutowezekana kuzalisha kitu kingine kinachofanana na Qur’an.

Asiye mwarabu anafahamu tu maana ya msingi ya maneno na hawezi kuelewa vizuri mtindo wa ufasaha, ambao hubeba maana za ziada bila ya kuomba ushahidi kutoka kwa mtu wa tatu.

Muislamu asipojua lugha ya Kiarabu ni lazima akimbilie kwenye maana iliyotafsiriwa katika lugha anayoimudu. Hata lugha hiyo ikiwa nzuri au fasaha kiasi gani, itaeleza tu maana za msingi na siyo zile za ziada.

Hatukatai kwamba kuna ufasaha katika lugha nyingine, lakini tunathibitisha kwamba ufasaha huu utakuwa unakaribia tu ule wa lugha ya Kiarabu. Mfano ni maneno haya ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ambayo yametafsiriwa kwa Kiswahili: “Je, nyinyi mnao watoto wa kiume na Yeye (Allah) ndio awe na watoto wa kike? Huo ni mgawanyo wa dhuluma!” [Qur’an, 53:21–22].

Lakini, tafsiri hiyo haitoi maana fasaha na kuonesha matumizi wala chaguo la maneno maalumu katika aya hizi. Aya hizo, kwa hiyo, zimetafsiriwa kwa maneno ya kawaida ya Kiswahili. Ili kuelewa ufasaha wa aya hizi, ni lazima tuzingatie mazingira ya kufunuliwa kwake.

Matumizi ya maneno yanaonesha kwamba waarabu makafiri walikamilisha uzushi mara tatu. Kwanza, kwa kujumuisha miungu (masanamu), pili kwa kujiona bora kuliko masanamu yao, na tatu kwa kuwafikiria malaika kama wenye jinsia ya kike wakati wao wanawadharau wanawake, na hata walipokuwa wakitukanana, kila mmoja alimuita mwenzie mwanamke.

Ni kutokana na sababu hiyo, Allah ‘Azza wa Jallah’ hakutumia istilahi ya Kiarabu ‘dhulma’, ‘isiyo sawa’ au ‘isiyolingana’, bali ametumia neno: ‘Dhwizaa.’ Hili ni neno geni mahali hapa, tena lenye sauti ya kulaani. Kwa hiyo, tafsiri hazilingani au haziko sawa ingawa zinawasilisha maana moja tu. Mtu asiye mahiri wa lugha ya Kiarabu hawezi kuelewa au kuhisi ufasaha na utamu wa maneno yanayotumiwa.

Kuielewa shariah

Shariah haiwezi kueleweka bila ya ufahamu wa kina wa maandiko ya Kitabu (Qur’an), Sunna Tukufu za Mtume na Ijtihad kutokana na vyanzo hivyo. Hili haliwezi kufanyika bila ya kuwa mahiri wa lugha ya Kiarabu.

Mara zote kumekuwa na maafikiano ya wanazuoni kwamba, lugha ya Kiarabu ni sharti muhimu la kufanya Ijtihad, na yeyote asiyekuwa na maarifa ya kutosha ya lugha ya Kiarabu hana haki ya kufanya Ijtihad.

Siku hizi watu wanajifanya wanajua sana mpaka wamefikia hatua ya kujiita ‘Islamic thinkers’, na wanadai kufanya Ijtihad katika dini, wanazungumzia halali na haramu na wanakosoa mpaka fiqhi ya Kiislamu, ambayo misingi yake iliwekwa na wanazuoni wazito kabisa wa Kiislamu.

Kwanza hawaijui vizuri lugha ya Kiarabu, na kwa sababu hiyo hawawezi kuelewa maana za kina za Qur’an na Sunna, na pili hawajasoma vizuri maneno ya wanazuoni wakubwa. Sasa inawezekana vipi watu kama hawa kufanya Ijtihad na kuikosoa fiqhi kwa kutumia utashi na akili binafsi tu?

Mtu hajui chochote kuhusu Muwatta ya Imam Malik, au Risala ya Imam Shafii, au Musnad ya Ahmad lakini anakosoa tu fiqhi ya Kiislamu kwa  malengo ya kuipotosha. Wanadhani Qur’an na Sunna vinaweza kufasiriwa kwa namna ambayo inaendana na maadili yao, tamaduni zao na fikra zao!

Nimalizie kwa kusema, lugha ya Kiarabu ni muhimu sana na haiepukiki ikiwa tunataka kujenga ufahamu wa kina na utambulisho wetu, na ili tuimarishe uhusiano wetu, utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button