Fahamu usyoyajua

Dkt Zakir Naik na Afrika

Dkt. Zakir Naik ni msomi wa Kiislamu anayejulikana kwa mchango wake mkubwa katika kueneza ujumbe wa Uislamu duniani, ikiwa ni pamoja na bara la Afrika. Akiwa na elimu ya udaktari, alijitosa katika ulinganiaji (da’awah) kwa kutumia mbinu za kielimu na mijadala ya kidini ili kufafanua mafundisho ya Uislamu na kuyalinganisha na dini nyingine (comperative religion).

Katika safari zake barani Afrika, Dkt Naik amewahi kutembelea nchi kadhaa kama vile Nigeria, Ghana, Afrika Kusini, The Gambia, Morocco, Algeria, Egypt na vilevile Kenya na Uganda nchi ambazo amezitembelea hivi karibuni na kisha atatua Tanzania. Kote huko amekuwa akitoa mihadhara inayovutia maelfu ya watu. Mihadhara yake imejikita katika kufafanua mafundisho ya Uislamu, kujibu maswali ya wasikilizaji, na kuondoa dhana potofu kuhusu dini ya Uislamu.

Mbinu yake ya da’awah inajumuisha kutumia maandiko ya dini mbalimbali ili kuonyesha ulinganifu na tofauti zake na Uislamu. Anatumia hoja za kimantiki na ushahidi wa maandiko matakatifu ili kuwavutia wasikilizaji kutoka dini tofauti.

Mbinu hizi za kiuwasilishaji zimemsaidia kujenga daraja la mawasiliano kati ya Waislamu na wasio Waislamu, hasa katika jamii zenye mchanganyiko wa kidini kama ilivyo kwa Afrika. Kadhalika, imemsaidia kwa ufanisi mkubwa kuonesha usahihi, ukweli na utukufu wa dini ya Kiislamu.

Katika moja ya ziara zake nchini Nigeria katika jiji la Abuja mwaka 2023, Dkt Naik alifanya mihadhara iliyohudhuriwa na maelfu ya watu, akijadili mada kama “The Muslims Choice – Dawah or Destruction.” Mihadhara hii ililenga kuwahamasisha Waislamu kuchukua jukumu la kueneza ujumbe wa Uislamu kwa amani na busara.

Huko Kumasi, Ghana mwaka 2014, Dkt Naik alifanya mhadhara uliolenga tu kujibu maswali ya wasio Waislamu na kusilimisha Waislamu wengi. Katika nchi nyingine pia alifanya makubwa.

Kwa hivi karibuni alitembelea Uganda na Kenya na kutoa mihadhara mingi, ikiwemo Da’awah – Jukumu la kila Muislamu (Da’wah – The Duty of Every Muslim) katika hafla ya Shaikh Ali Sufi International Qiraat Award 2024 jijini Nairobi. Katika mhadhara huu, alionesha namna Uislamu umefanya ulinganiaji kuwa jukumu la kila mmoja wetu.

Akiwa Nairobi, katika siku chache zilizopita, pia alitoa mada nyingine kama vile Chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia), Uislamu katika mtazamo sahihi, na Mtume Muhammad katika Biblia.

Hukohuko Kenya katika mji wa Mombasa, Dkt Naik anawasilisha mada kuhusu mambo yanayopotoshwa kuhusu Uislamu, mada ambayo kwa uzito wake anaiwasilisha kwa siku mbili mfululizo Disemba 28 na 29  katika ukumbi wa Sheikh Zayed uliopo Bombululu, Mombasa, Kenya.

Hakika mchango wake katika da’awah umemletea heshima na kutambuliwa kimataifa. Mwaka 2015, alitunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Mfalme Faisal katika  kuhudumia Uislamu, ikiwa ni kuthamini juhudi zake katika kueneza na kufafanua mafundisho ya Kiislamu duniani.

Dkt Naik pia ameanzisha kituo kikubwa cha televisheni cha Peace TV, ambacho kinatangaza mafundisho ya Kiislamu kwa lugha mbalimbali, ikiwemo Kiingereza, Kihindi, na Kiarabu. Kupitia vyombo hivi, amefanikiwa kufikia mamilioni ya watazamaji barani Afrika na duniani kote, akichangia katika kueneza ujumbe wa Uislamu kwa njia ya kisasa.

Mbali na mihadhara, Dkt. Naik ameshiriki katika mijadala ya kidini na viongozi wa dini nyingine, akijibu maswali na changamoto zinazotolewa dhidi ya Uislamu. Mijadala hii imesaidia kuondoa dhana potofu na kujenga uelewa bora kati ya dini mbalimbali, hasa katika nchi za Kiafrika zenye mchanganyiko wa kidini.

Athari za kazi zake barani Afrika zimeonekana katika ongezeko la watu wanaokubali Uislamu na kuimarika kwa uelewa wa mafundisho sahihi ya dini hiyo. Pia, amewahamasisha Waislamu wa Afrika kujivunia dini yao na kushiriki kikamilifu katika kueneza ujumbe wa amani na upendo unaofundishwa na Uislamu.

Hata hivyo, kazi zake zimekumbana na changamoto, ikiwa ni pamoja na upinzani kutoka kwa baadhi ya makundi na serikali. Licha ya hayo, ameendelea na juhudi zake za da’awah kwa amani, akisisitiza umuhimu wa mazungumzo na kuelewana kati ya dini mbalimbali. Kwa ujumla, urithi wa Dkt. Zakir Naik barani Afrika ni wa kudumu, ukiakisi juhudi zake za kueneza ujumbe wa Uislamu kwa njia ya amani na kielimu. Mbinu zake za kutumia hoja za kimantiki na maandiko ya kidini zimechangia katika kujenga maelewano na kuondoa dhana potofu kuhusu Uislamu katika bara hili la Afrika.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button