
Dkt. Naik ni mfano wa kuigwa katika da’awah
Kila mmoja wetu hapa duniani ana jambo alilotunukiwa na Allah Ta’ala ili aweze kulifanya na kuleta faida kwa umma. Kwa mantiki hiyo, hapana shaka juu ya kuwepo kwa watu mahususi ambao jamii huwachukulia kama darasa muhimu la kuchota elimu ili kujifunza.
Hata hivyo si watu wote waliojaaliwa uwezo wa kufanya mambo makubwa na muhimu kwenye jamii. Ni wachache mno wanaoingia katika kundi hili.
Miongoni mwa wachache hao ni Dkt. Zakir Abdul Karim Naik, Mhubiri na mlinganiaji maarufu wa dini ya Kiislamu duniani kutoka nchini India. Dkt. Naik, ambaye amebobea katika fani ya Dini Linganifu (Comparative Religion) ni miongoni mwa wahubiri wa Kiislamu wenye ushawishi mkubwa kwa jamii ya Waislamu na wasiokuwa waislamu ulimwenguni.
Mbali na kufanya mihadhara katika mataifa mbalimbali duniani, Dkt. Naik ni muasisi na Rais wa taasisi ya Islamic Research Foundation (IRF) na televisheni mashuhuri ya Peace TV iliyo na makao makuu yake huko Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Hakuna shaka juu ya ziara ya Dkt. Naik hapa nchini kuwa imeleta faida na manufaa makubwa kwa Watanzania kutokana na ujumbe wake wa ‘Jesus and Mohammad are brothers in faith’, yani ‘Yesu na Muhammad ni ndugu katika imani’ kuwavutia wengi.
Kwa hali zote, tuna kila sababu ya kujivunia Dkt. Naik kutokana na da’awah yake kuwa nuru inayowaangazia Waislamu na wasiokuwa waislamu.
Kwa hakika, Dkt. Naik ni mfano bora wa kuigwa na kupongezwa kwani kazi anayofanya inakwenda sambamba na maelekezo ya Allah na Mtume (rehema na amani zimfikie), ambao kwa pamoja wametuusia kuwalingania watu Uislamu kwa kuzingatia kipengele cha juhudi, hekima na mawaidha mazuri.
Katika kulisisitiza hilo, Allah Mtukufu anasema: “Waite watu katika njia ya Mola wako Mlezi kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora…” [Qur’an, 16:125].
Sisi gazeti la Imaan tunaamini kwamba, jitihada za ulinganiaji zinazofanywa na Dkt. Naik zina maana kubwa katika kuujenga umma kiimani na kimaadili.
Tunatambua kuwa moja kati ya matunda na faida kubwa ya ulinganiaji ni kuondoa kutu, uchafu na matamanio mabaya katika nyoyo za waja. Hii ina maana kwamba watu wasipopewa mawaidha nyoyo zao huingiwa na kutu. Hivyo basi, umma wa Watanzania una kila sababu ya kuchukua kwa uzito mafundisho na maelekezo aliyoyatoa Dkt. Naik katika mihadhara yake ili yawaletee faida katika dunia na Akhera waendako. Kila la kheri Dkt. Naik!