
Peace TV inavyoacha athari ndani, nje ya Afrika
Mnamo Januari 2006, wakati dunia ikiwa katika mabadilko ya kasi kutokana na ukuaji mkubwa wa sayansi na teknolojia, kituo cha televisheni cha Kiislamu kinacholenga kueneza ujumbe wa amani, elimu, na uelewa wa dini ya Kiislamu kimataifa kilianzishwa na mmoja wa wahubiri wakubwa wa Kiislamu duniani kutoka India, Dkt Zakir Naik.
Peace TV imekuwa na athari kubwa katika jamii ya Waislamu duniani, ikiwemo bara la Afrika, kwa kutoa maudhui yanaimarisha imani na maarifa ya Kiislamu na kupunguza upotoshaji kuhusu dini hii tukufu.
Kupitia Peace TV, mwanzilishi wake, Dkt. Zakir Naik ameweza kufikisha mihadhara na mijadala inayohusu Uislamu na kulinganisha dini mbalimbali, akilenga kujenga daraja la maelewano kati ya dini na tamaduni tofauti.
Peace TV inarusha matangazo yake katika lugha za Kiingereza, Kiarabu, Kihindi, Kibangla, na Kichina, ikilenga kufikia hadhira pana zaidi. Kwa mujibu wa taarifa, kituo hiki kina watazamaji wengi kutoka Mashariki ya Kati na nchi za Afrika na hivyo kuwa chanzo muhimu cha elimu ya Kiislamu kwa Waislamu na hata wasio Waislamu.
Katika bara la Afrika, Peace TV imekuwa na mchango mkubwa katika kueneza elimu na ufahamu wa Uislamu hasa katika nchi zenye idadi kubwa ya Waislamu kama Tanzania, Nigeria, Ghana lakini pia kwenye nchi zenye idadi ndogo ya Waislamu kama Afrika Kusini lakini wenye nguvu na ushawishi mkubwa.
Kupitia programu zake, kituo hiki kimeweza kujibu maswali na changamoto zinazowakabili Waislamu wa Kiafrika na pia duniani kwa ujumla, na hivyo kusaidia katika kuimarisha imani na utambulisho wao wa Kiislamu.
Hata hivyo, Peace TV imekumbana na changamoto kadhaa, ikiwemo kupigwa marufuku katika baadhi ya nchi kutokana na madai ya kueneza maudhui yenye utata. Kwa mfano, nchini Bangladesh, kituo hiki kilipigwa marufuku mwaka 2016 baada ya shambulio la kigaidi lililotokea Dhaka, ambapo ilidaiwa kuwa wahusika walihamasishwa na mafundisho ya Dkt. Zakir Naik, jambo ambalo ni la uongo kabisa.
Licha ya changamoto hizi, Peace TV imeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika jamii ya Waislamu duniani. Kupitia programu zake, kituo hiki kimeweza kuhamasisha mijadala ya kidini na kielimu, na hivyo kuchangia katika kuimarisha uelewa na maelewano kati ya dini na tamaduni mbalimbali.
Wakati ambapo mabadiliko makubwa yakitokea katika jamii nyingi ulimwenguni, kituo hiki kimenakili njia mpya za urushaji matangazo kupitia mifumo ya kidijitali na wavuti.
Peace TV imejitahidi kufikia watazamaji wake kupitia njia mbalimbali za kisasa. Kwa mfano, kituo hiki kinapatikana kupitia programu za simu kama Peace TV kwenye App Store, Apple Apps na Google Play, na hivyo kurahisisha upatikanaji wa maudhui yake kwa watazamaji duniani kote.
Athari ya Peace TV chini ya uongozi wa Dkt Naik ni mkubwa na wenye manufaa katika jamii ya Waislamu duniani, ikiwemo Afrika.
Kupitia jukwaa hili, Dkt. Naik ameweza kueneza ujumbe wa amani na elimu ya Kiislamu, na hivyo kuchangia katika kuimarisha uelewa na maelewano katika jamii. Katika zama ambazo tunahitaji kufanya juhudi kubwa kutangaza dini ya Allah chombo hiki kikubwa cha Kiislamu kinabeba jukumu la asili la kufikisha Daawah na kuutangaza Uislamu kwa amani duniani.