
Chuki dhidi ya Uislamu yakua duniani
Dunia inazidi kushuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu, hali ambayo imeathiri maisha ya Waislamu barani Ulaya, Marekani, na hata Asia Kusini, hususan India.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, makundi ya siasa za mrengo wa kulia yanaendelea kuchochea uhasama huu. Ufaransa, yenye idadi kubwa ya Waislamu, ni mfano wa wazi ambapo chama cha National Rally cha Marine Le Pen kimejipatia umaarufu kwa misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu, kikivutia asilimia 33 ya kura kwenye uchaguzi wa wa mwezi Juni.
Majukwaa ya mitandao ya kijamii kama X (zamani Twitter) yameongeza kasi ya kueneza ujumbe wa chuki.
Hivi karibuni, mmiliki wake, Elon Musk, alichapisha makala akiunga mkono chama cha Alternative for Germany, ambacho kinajulikana kwa misimamo yake ya kibaguzi dhidi ya Uislamu, akikitaja kama “chama pekee kinachoweza kuokoa Ujerumani.”
Hali hii inadhihirisha jinsi ujumbe wa chuki unavyoimarisha mtandao wa makundi yenye ajenda ya kuwapinga Waislamu barani Ulaya na kwingineko.
Hata hivyo, chuki dhidi ya Waislamu si tatizo la makundi ya mrengo wa kulia pekee.
Vyama vya mrengo wa kati na kushoto pia vinaonyesha mifumo ya chuki, ingawa kwa njia za siri. Katika Marekani, Waislamu wengi wameonesha kutoridhishwa na utawala wa Rais Joe Biden, huku ukosefu wa jitihada madhubuti za kushughulikia changamoto zinazowakumba ikiwa ni sababu kuu mojawapo.
Tukio la kushambuliwa kwa soko la Krismasi mjini Magdeburg, Ujerumani, mwezi uliopita lilionyesha jinsi mijadala kuhusu Uislamu inavyobaki kuwa sumu. Hata kabla ya ukweli kuhusu mshambuliaji (aliyekuwa Muislamu mwenye msimamo mkali wa kupinga dini hiyo) kufahamika, Waislamu walikumbwa na lawama.
Katika mazingira haya ya chuki, Waislamu wanaendelea kupigania haki yao ya kuishi kwa amani na usawa. Machi 15, ambayo imetengwa kama Siku ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu, ni fursa ya kukumbusha ulimwengu kwamba mapambano haya hayawezi kufanyika kwa siku moja tu kwa mwaka. Serikali, mashirika ya kiraia, na wafanyabiashara wanapaswa kushirikiana kutengeneza mipango madhubuti ya muda mrefu ya kuondoa chuki hizi, kwa msingi wa haki na usawa kwa jamii zote. Jamii itakayowakubali wote bila kujali dini au historia yao itakuwa bora zaidi kwa kila mtu.