
Mchoma Qur’an wa Sweden auawa kwa risasi
Mwanamume aliyekuwa maarufu kwa kuteketeza mara kwa mara Qur’an mwaka 2023 nchini Sweden, kitendo kilichozua ghadhabu katika mataifa ya Kiislamu, amepigwa risasi na kuuawa, vyombo vya habari vimeripoti mwishoni mwa wiki hii.
Polisi wakinukuliwa na Radio France International (RFI), wamethibitisha tukio hilo wakisema kwamba mtu mmoja alifariki dunia katika ufyatulianaji risasi siku ya Jumatano.
Salwan Momika, raia wa Iraq aliyekuwa Mkristo, alihusika na vitendo vya kuchoma Qur’an hadharani, hali iliyosababisha uhusiano mbaya kati ya Sweden na mataifa yenye Waislamu wengi. Mahakama ya Stockholm ilikuwa imepanga kutoa hukumu Alhamisi dhidi yake kwa shtaka la uchochezi wa chuki ya kikabila lakini iliahirisha hadi Februari 3 baada ya kifo chake kuthibitishwa.
Polisi walisema walipokea taarifa za ufyatulianaji risasi ndani ya jengo moja katika mji wa Sodertalje, ambako Momika alikuwa akiishi, na walipowasili eneo la tukio, walimkuta Sodertalje akiwa amejeruhiwa kwa risasi na alifariki dunia baadae akiwa hospitalini.
Inadaiwa kuwa tukio hilo la mapambano ya risasi lilirushwa mubashara kwenye mitandao ya kijamii. Uchunguzi wa mauaji umefunguliwa rasmi na mamlaka za Sweden.
Vitendo vya Momika vilisababisha maandamano makubwa katika nchi za Waislamu huku waandamanaji wakichoma moto ubalozi wa Sweden mjini Baghdad mara mbili Julai 2023. Kufuatia matukio hayo, idara ya ujasusi ya Sweden iliongeza kiwango cha tahadhari ya usalama hadi kiwango hadi namba nne kati ya tano, ikitaja kuwa Sweden imekuwa “lengo la kipaumbele” kwa mashambulizi.
Licha ya Serikali ya Sweden kulaani kitendo cha kuchoma Qur’an, ilisisitiza kuwa katiba ya nchi hiyo inalinda uhuru wa kujieleza na kuabudu.