Kimataifa

Hali tete Waislamu wa Rohingya walio India

Waislamu wa Rohingya waliokimbilia India wakitafuta hifadhi na maisha bora wanakabiliwa na ukatili wa kisiasa, huku vyama vya AAP na BJP vikishindana kuwashambulia kwa maneno na vitendo ili kujipatia kura katika uchaguzi wa Februari 5.

Hali hii imechangiwa na agizo la hivi karibuni la Waziri Mkuu wa Delhi, Atishi Marlena, aliyepiga marufuku wanafunzi wa Rohingya kujiunga na shule za umma jijini humo.

Vyama vya AAP na BJP vinatumia jumuiya ya Rohingya kama chambo cha kisiasa, kila upande ukijaribu kuonekana mkali dhidi ya wakimbizi hawa Waislamu.

BJP, chama cha Kihindu chenye msimamo mkali, kimewataja Rohingya kama “wavamizi haramu” na kuahidi kuwaondoa endapo kitashinda uchaguzi. Aidha, chama cha AAP, ambacho awali kilijitangaza kuwa cha wapenda haki, kimechukua mkondo uleule wa ubaguzi kwa hofu ya kupoteza kura za Wahindu.

Katika kambi ya wakimbizi ya Madanpur Khadar, hali ya maisha ni mbaya zaidi kwa Waislamu wa Rohingya. Kwa miezi minane, wakimbizi wa Rohingya wamekuwa wakiishi bila umeme, huku maji ya kunywa yakisambazwa mara mbili tu kwa wiki. Familia nyingi zinaishi kwa misaada, huku watoto wao wakizidi kunyimwa haki ya elimu.

Kwa miongo kadhaa, Waislamu wa Rohingya wameendelea kunyanyaswa, wakibaguliwa na serikali za Myanmar na sasa India.  Kukataliwa kwa watoto wao kupata elimu ni mwendelezo wa dhuluma wanazokumbana nazo. Baadhi yao wanasema kuwa wana matumaini kuwa Mahakama Kuu ya India itawatendea haki.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button