Kimataifa

Mwalimu Marekani  ajiuzulu kwa kumuita mtoto (12) gaidi

Mwalimu wa shule ya kati ya Central Dauphin mjini  Pennsylvania amejiuzulu kufuatia tuhuma za kutoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya mwanafunzi wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 12 kwa kumuita “gaidi”, tukio ambalo limeibua hasira na miito ya mabadiliko katika mfumo wa elimu ili kuhakikisha heshima na haki kwa Waislamu na jamii zingine za wachache.

Kwa mujibu wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la marekani (CAIR), tukio hilo lilitokea Januari 16 baada ya mwanafunzi huyo kumwomba mwalimu wake abadilishe nafasi ya kukaa darasani. Badala ya kumjibu kwa heshima, mwalimu alijibu kwa maneno ya chuki akisema, “Siwezi kujadiliana na magaidi.” Mwanafunzi huyo ametambuliwa kama Mmarekani mwenye asili ya Palestina na Lebanon.

Baba wa kijana huyo, Adam Rahman, alieleza kuwa mwanaye amepatwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo na ana wasiwasi iwapo atakumbana na ubaguzi kama huo tena shuleni. “Ameathirika sana na matamshi hayo, na hatasahau kwa muda mrefu,” alisema Rahman katika mkutano na waandishi wa habari. Aliitaka shule hiyo kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha matukio kama haya hayajirudii kwa wanafunzi wa Kiislamu na jamii nyingine za wachache.

Wanarakati wamesema tukio hili ni ishara ya ubaguzi wa mizizi ya kina, unaochochewa na upotoshaji wa habari kuhusu Palestina kwenye vyombo vya habari vya Magharibi. “Shule zinapaswa kuwa sehemu za kujifunza na sio uwanja wa propaganda zinazowapotosha walimu na kuwafanya waonyeshe chuki dhidi ya Waislamu,” ilisema taarifa ya jumuiya hiyo.

CAIR na mashirika mengine yamepongeza kujiuzulu kwa mwalimu huyo lakini wakaitaka shule ihakikishe kuwa walimu wake wanapatiwa mafunzo ya usawa wa kidini na kitamaduni. “Hatufurahii tu kwamba mwalimu huyu ameondoka, tunataka kuona hatua kali dhidi ya vitendo vya kibaguzi katika shule,” ilisema taarifa ya pamoja ya CAIR na familia ya Rahman. Wameitaka shule hiyo kuweka mtaala wa elimu ya kimataifa ili kuwasaidia wanafunzi na walimu kuelewa historia kamili ya Palestina na tamaduni za Waislamu.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button