
Walinda amani wawili wa JWTZ wafariki dunia DRC
Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limethibitisha kuwa askari wake wawili wamefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa wakati wakitekeleza jukumu la kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda, huku ikithibitishwa kuwa mashambulizi hayo yalitokea Januari 24 na 28 katika maeneo ya Sake na Goma, mashariki mwa DRC.
“Kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma yaliyofanywa na waasi wa M23 Januari 24 na 28, 2025, JWTZ limewapoteza askari wake wawili na wengine wanne kujeruhiwa. Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Goma.
“Taratibu za kuisafirisha miili ya marehemu wetu pamoja na majeruhi waliotokana na mapigano hayo zinaendelea kupitia Sekretarieti ya SADC.
“Mwenyezi Mungu awape uponyaji wa haraka majeruhi wetu na aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo imeeleza kuwa vikundi vya JWTZ vilivyopo nchini DRC vipo salama, imara, na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa JWTZ linaendelea kulinda amani kwa mwamvuli wa SADC (SAMDRC) huko mashariki mwa DRC, eneo ambalo limekumbwa na mgogoro uliozua mashambulizi kati ya waasi wa M23 wanaopambana na Jeshi la DRC (FARDC) katika maeneo hayo.
Vifo vya askari wengine
Taarifa ya JWTZ imetolewa huku kukiwa na taarifa nyingine za vifo vya wanajeshi 13 kutoka Afrika Kusini na watatu kutoka Malawi waliouawa katika mapigano Goma. Wanajeshi hao walikuwa wamepelekwa kama sehemu ya juhudi za kudumisha amani za kikanda.
Nchi za Afrika Kusini, Malawi, na Tanzania ndizo zenye wanajeshi wanaolinda amani DRC kwa mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SAMDRC). Uvamizi wa M23 mashariki mwa DRC umeendelea kusababisha vifo vya wanajeshi na raia, hali inayozua taharuki na changamoto za kibinadamu.