
Jumuiya ya kimataifa yaamuru Rwanda kuondoa vikosi DRC
Jumuiya ya kimataifa imeitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuacha kuwafadhili waasi wa M23 wanaosema kwamba wanalenga kusonga mbele hadi mji mkuu, Kinshasa.
Kwa mujibu wa DW, shinikizo hilo linaongezeka kwa utawala wa Rais Paul Kagame wakati waasi wa M23 wakiendelea kusonga mbele kuelekea mji mwingine wa Mashariki mwa Congo, Bukavu.
Mapigano yameendelea kuripotiwa maeneo mbalimbali mashariki mwa DRC ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakielekea katika mji wa Bukavu baada ya kuchukua udhibiti kamili wa Goma.
Licha ya mapigano kupungua huko Goma, hali ya kibinadamu inaelezwa kuwa mbaya. Uhaba wa chakula na bidhaa muhimu, mgawo wa umeme umevurugika, hakuna maji safi, huku kukiwa matatizo pia kwenye mtandao wa intaneti.
Raia wa Goma walisema wanahitaji msaada kwa kuwa mji wao umekuwa kama meli isiyo na nahodha. Hawa ni Isaac Mastaki na Louise Furaha. Hayo yanajiri wakati kiongozi wa kisiasa wa muungano wa waasi wa Kongo unaolijumuisha kundi la M23, Corneille Nangaa aliapa jana kuwa wapiganaji wake hawatauachia mji wa Goma.
Hata hivyo, Nangaa alisema wako tayari kwa mazungumzo na serikali ya Kongo. Rais wa DRC, Felix Tshisekedi alitoa wito wa kufanyika kwa uhamasishaji mkubwa wa kijeshi ili kukabiliana na uasi huo, huku akitupilia mbali miito ya kufanya mazungumzo na waasi wa M23.