
Sheikh Fariq ataja mbinu za kufikia malengo ya da’awah
Ili kutatua changamoto mbalimbali za kidini na kijamii, Waislamu nchini na duniani kote wamesisitizwa juu ya umuhimu wa kutafuta elimu ya dini na mazingira.
Pia, Waislamu wametakiwa kuishi kwa kufuata barabara miongozo ya Uislamu kupitia mafundisho ya Mtume Muhammad (rehema na amani iwe juu yake) kwani hakuna mafanikio pasipo kumfuata Mtume.
Hayo yamebainishwa na Mhadhiri wa Kimataifa, Sheikh Fariq Naik kwenye kongamano la kimataifa la amani lililofanyika Januari 2, 2025 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Sheikh Fariq aliieleza hadhira ya kongamano hilo lililoandaliwa na taasisi ya The Islamic Foundation kuwa, Mtume Muhammad (rehema na amani iwe juu yake) ndiye kiumbe pekee aliyeikomboa dunia kutokana na vitendo vya udhalilishaji, manyanyaso na dhuluma za kijinsia, na ndiyo maana tafiti mbalimbali zinamtaja kuwa ndiye binadamu mwenye ushawishi mkubwa zaidi duniani.
Mtume wetu (rehema na amani iwe juu yake) siku zote alitamani mema kwa umma wake, kwa ajili ya watu wake, hivyo basi awe kigezo chema kwetu, matamanio yake yawe ni matamanio yetu, maono yake yawe ni maono yetu na kazi yake iwe ni dhamira kwetu,
alisema Sheikh Fariq.
Akitaja namna Mtume alivyoukomboa ulimwengu katika nyanja mbalimbali, Sheikh Fariq alisema, Mtume Muhammad alikuwa muaminifu na alirudisha vitu vyote vya watu walivyompa avitunze.
Kwa ukombozi wa watu, alikuwa mkweli, muaminifu na mwenye huruma. Sifa zote hizi zinapatikana kwa Mtume wetu Muhammad (rehema na amani iwe juu yake), na ndiyo sababu alikuwa mkombozi wa ulimwengu,
aliongeza kusema.
Sheikh Fariq alitaja miongoni mwa tabia ambazo Mtume Muhammad (rehema na amani iwe juu yake) alijipamba nazo, ambazo Waislamu wanapaswa kumuiga kuwa ni kuwapenda watoto.
Katika kulisisitiza hilo, Sheikh Fariq alinukuu hadith ya Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) inayosema:
“Si katika sisi yule asiyewahurumia wadogo wetu na akaitambua haki ya wakubwa.”
Pia alirejea hadith ya Mtume isemayo:
“Asiyewahurumia watu hatohurumiwa na Allah.” [Bukhari, Muslim na Ahmad].
Huku akinukuu aya katika sura ya Al–Baqara isemayo:
(Allah) humpa hekima amtakaye. Na anayepewa hekima, basi kwa hakika amepewa kheri nyingi,
Sheikh Fariq alieleza kuwa mafanikio makubwa aliyoyapata Mtume (rehema za Allah na amani iwe juu yake) katika da’awah hayakutokana na kupigana vita bali kwa ulinganiaji mwema, hekima, busara na maelewano kwa watu wote.
“Ni kwa sababu hiyo watu wengi leo hii wanakubali Uislamu kuwa ndiyo dini ya kweli,” aliongeza kusema.
Mbali na hayo, Sheikh Fariq aligusia suala la haki na malezi ya watoto ambapo amewasihi wazazi, walezi na Waislamu kwa ujumla wao kwamba, wote ni wachunga kwa amana walizopewa, hivyo wana dhima kubwa ya kuhakikisha wanatenda haki na uadilifu katika amana walizopewa.
Alisema, mume ni mchunga kwa familia yake, na mke nae ni mchunga wa nyumba ya mumewe, na kwamba wote wawili watakuja kuulizwa juu ya amana walizopewa kuzichunga.
…ausia uvumilivu katika dini
Kuhusu changamoto katika dini, Sheikh Fariq aliwatoa wasiwasi Waislamu akisema kuwa njia ya kuelekea Peponi imezingwa na matatizo mengi.
Sheikh Fariq alitoa mfano wa familia ya Ammar bin Yaasir, mojawapo ya familia za mwanzoni kusilimu katika mji wa Makka. Alisema, Ammar bin Yaasir, baba yake, pamoja na mama yake, Sumayyah waliadhibiwa na makureish kwa kulazwa juani ili wauache Uislamu lakini hawakuwa tayari kuritadi. Sheikh Fariq aliwataka Waislamu kuchukua funzo kutokana na yale yaliyoisibu familia ya Ammar na kusisitiza kuwa Pepo ya Allah iko karibu na wenye subira na wavumilivu.