Habari

Miche ya Hass inavyoongeza thamani zao la parachichi

Tanzania inatajwa kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa zao la parachichi baada ya Afrika Kusini na Kenya, ambapo huzalisha wastani wa tani 190,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, parachichi hulimwa zaidi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Songwe na Njombe. Mikoa mingine inayozalisha zao hilo la kimkakati ni pamoja na Kagera, Kigoma, Rukwa, Tanga, Manyara, Iringa, Mara na Ruvuma.

Parachichi zinazolimwa Tanzania soko lake kubwa lipo Uingereza, Uholanzi, China, India na Afrika Kusini. Ifahamike kuwa kuna aina mbalimbali za parachichi zinazolimwa duniani. Kwa hapa nchini zipo aina mbalimbali za parachichi, lakini zinazolimwa kwa wingi ni pamoja na Hass, Fuerte, Pinkerton, Ex–Ikulu, Nabal, Ettinger, Zutano na Waisal.

Kwa msingi huo, leo katika darasa letu la kilimo tutaangalia umuhimu wa kuchagua mbegu bora ya parachichi inayoweza kustahimili magonjwa ili kuzalisha matunda yanayokidhi uhitaji wa soko na hivyo kufikia ajenda ya kilimo biashara.

Kwa kweli, ukitaja taasisi za utafiti zinazofanya tafiti nyingi hapa nchini, huwezi kuacha kuitaja Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 10 ya mwaka 2016 ikiwa na majukumu ya kutekeleza utafiti wa kilimo.

TARI kwa kushirikiana na wadau wa kilimo wa kitaifa na kimataifa ina dhima ya kugundua na kuhimiza matumizi ya teknolojia mbalimbali za kilimo ili kuongeza tija, uhakika wa chakula na lishe, kuwa na kilimo endelevu na chenye mchango chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kwa muktadha huo, kituo cha TARI Tengeru chenye ofisi zake mkoani Arusha, ambacho ni mojawapo ya vituo 17 vya TARI, kimeamua kujikita katika utafiti wa mazao ya bustani, parachichi likiwa ni mojawapo.

Kwa sasa kituo hicho kinaendelea na shughuli za uzalishaji wa miche bora 100,000 ya parachichi aina ya Hass inayotegemewa kuwafikia wakulima kwa bei elekezi ya Serikali katika msimu ujao wa kilimo kupitia uongozi wa Halmashauri walizopo.

Tanzania inaweza kuwa kwenye nafasi za juu katika uzalishaji wa zao la parachichi barani Afrika endapo uzalishaji wa zao hili utafanyika kwa kuzingatia uhitaji wa soko.

Mtafiti wa Kituo cha TARI Tengeru, Yusuph Ng’imba anasema, haitoshi tu mkulima kuishia kutambua kuwa soko la parachichi aina ya Hass ni kubwa ndani na nje ya nchi, bali atambue chanzo cha uhakika cha kupata miche ambayo itafanya parachichi zake ziwe na soko.

Ng’imba anasema, kuna njia za kitaalamu zinazotakiwa kufuatwa ili mche wa parachichi uwe na tija, na kama njia hizo hazitazingatiwa, inawezekana mkulima akatumia nguvu kubwa bila mafanikio kutokana na kutumia miche ambayo haikuandaliwa kitaalamu.

Sifa za parachichi aina ya Hass

Akitaja sifa za miche ya parachichi aina ya Hass, Ng’imba anasema inachukua muda mfupi kuzaa (kati ya miaka miwili na nusu hadi mitatu). Sifa ya pili ni kwamba, miche ya Hass inayozalishwa kitaalamu inakuwa haina magonjwa na wadudu kutokana na uandaaji bora, pia vikonyo vya kubebeshea huchukuliwa kwenye miti halisi ya Hass.

Ametaja sifa ya parachichi aina ya Hass kuwa lina ubora wa hali ya juu, halina nyuzinyuzi na lina kiwango cha mafuta cha asilimia 18 hadi 23. Aidha, Ng’imba amesema parachichi aina ya Hass linaweza kukaa kwa muda wa wiki mbili mpaka tatu baada ya kuvunwa, hivyo kurahisisha usafirishaji katika maeneo ya mbali ukilinganisha na aina nyingine za parachichi.

Ng’imba anasema, maparachichi aina ya Hass yana soko kubwa kitaifa na kimataifa kutokana na mahitaji yake makubwa. Ameongeza kuwa aina hii ya maparachichi ina madini mengi ya calcium, magnesium pamoja na vitamini A,B,C,D,E na K na hivyo kuwa muhimu katika uboreshaji wa afya na lishe.

Ng’imba anasema, sifa zote hizo zinafanya aina hii ya parachichi kuwa na tija kwa mkulima iwapo atakuwa na uhakika wa miche aliyotumia. Kwa kuzingatia hayo, Serikali imeiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha TARI Tenguru ili kuhakikisha kinazalisha miche bora na kuwafikia wakulima kwa bei elekezi.

Wito kwa wakulima

Wakati huu ambao parachichi za Tanzania zinatajwa kuwa na soko kubwa la kitaifa na kimataifa, ni vyema wakulima wakazingatia kanuni bora za kilimo cha zao hili ili kujiongezea kipato wao binafsi na taifa kwa ujumla.

Serikali imeonesha nia ya dhati kuliendeleza zao la parachichi hadi kulitambua kama zao la kimkakati. Watafiti wa kilimo, nao wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya kanuni bora za kilimo katika mazao mbalimbali likiwemo parachichi, hivyo ni muhimu kwa wakulima kutumia fursa ya kujifunza kilimo bora kutoka kwa wataalamu waliopo kwenye maeneo yao.

Wapo baadhi ya wakulima ambao huvuna parachichi zisizokomaa na kuzipeleka sokoni licha ya kutambua kuwa hakuna soko la parachichi zisizokomaa. Jambo hili limekuwa likiharibu soko la parachichi kimataifa.

Hakika, tija inayotajwa katika kilimo cha parachichi inaanza na matumizi ya mbegu/miche bora, hivyo ni wakati wa wadau wa kilimo kunufaika na matunda ya uwekezaji wa Serikali katika kilimo cha parachichi.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button