Events

Nakuomba niwe rafiki yako Peponi!

Rabi’ah bin Ka’ab al–Aslamiy (Allah amridhie) amehadithia kuwa alikuwa akilala pamoja na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), siku moja akamletea maji ya kutawadha pamoja na mahitaji yake mengine.

Mtume akamwambia: “Omba unachotaka.” Rabi’ah akasema: “Nakuomba niwe pamoja nawe Peponi.” Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akamuuliza: “Kuna jambo lingine lisilokuwa hilo?” Akasema: “Ni jambo hilo tu.” Mtume akasema: “Kama ni hivyo, basi nisaidie kwa wingi wa sala.” [Imepokewa na Muslim].

Rabi’ah bin Ka’ab (Allah amridhie) ni miongoni mwa Maswahaba waliobahatika kumtumikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), akimwandalia maji ya kutawadha na kumsaidia katika mahitaji yake mengine.

Jambo hili litakuwa miongoni mwa mambo ya kuorodheshwa katika fadhila na wasifu wa Rabi’ah bin Ka’ab kwa kule kubahatika kuwa karibu na Mbora wa viumbe wa Allah na kumhudumia japo katika mambo machache.

Kutokana na tukio hili lililomhusisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema za Allah na amani zimshukie) na swahaba huyu mtukufu, kuna mazingatio kadhaa na mambo ya kujifunza. Hebu tujadili mambo muhimu tuliyoyaona.

Kufadhilisha ubora wa mambo

Katika mazingira ya kawaida, mtu anapopata fursa mbele ya kiongozi mkubwa huitumia fursa hiyo kwa kujinufaisha hasa kwa mambo ya kilimwengu ili arahisishe maisha yake kwa kupata anachokitamani. Hii huthibiti zaidi pale kiongozi huyo anapomfungulia mwenye shida katika wahudumu wake mlango wa kuomba au kuchukua kile anachokihitaji.

Kwa upande wake, Rabi’ah bin Ka’ab (Allah amridhie) hakuitaka dunia. Kwanza, alijua kuwa hakuwa karibu na kiongozi wa kawaida, bali Mbora wa viumbe wa Allah, Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), ambaye ndiye kiongozi wa umma mzima.

Isitoshe, wakati Rabi’ah akipewa fursa ya kuomba, alifahamu fika kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwapenda mno Maswahaba zake (Allah awaridhie) na alikuwa ni mwepesi mno wa kutoa. Mtume hakuwa akikifanyia ubahili kile alichokuwa nacho.

Pamoja na yote hayo, nafsi ya Rabi’ah ilikuwa ikitamani yaliyo matukufu. Yeye hakuwa mwenye mtazamo wa mambo ya mpito ambayo hayatamnufaisha katika maisha ya kudumu. Kwa sababu hiyo, Rabi’ah alitumia fursa hii adhimu kuomba kitu muhimu ambacho kinahitaji juhudi kubwa kukipata.

Rabi’ah (Allah amridhie), hakuomba Pepo tu, bali aliomba kuwa pamoja na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) katika Pepo hiyo. “Nakuomba niwe rafiki yako Peponi.” Anamuomba Mtume amuombee kwa Allah awe pamoja naye Peponi. Hayo ndiyo yalikuwa maombi ya Rabi’ah kwa Mtume.

Kupitia kisa hiki na maombi ya swahaba huyu, tunafundishwa umuhimu wa kuitumia fursa vizuri na kutazama yaliyo bora na yenye manufaa ya kudumu.

Kushukuru

Tukio hili linatuonesha umuhimu wa kuthamini msaada wa mtu na kumshukuru kutokana na wema aliyokufanyia. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alitaka kumshukuru Rabi’ah na kumlipa kwa wema aliyomfanyia wa kumtumikia, ndipo akampa fursa ya kuomba kitu anachokitamani.

Imethibiti katika hadith ya Abu Huraira (Allah amridhie) kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hatomshukuru Allah yule asiyewashukuru watu.” [Ahmad]. Mtume alimaanisha kuwa, mtu asiyewashukuru watu juu ya wema wanaomfanyia, basi utamkuta pia si mwenye shukrani kwa Allah kwa neema ambazo Allah amempa.

Kwa maana nyingine pia, yule mwenye kukumbuka wema na akatanguliza shukrani kwa watu, utamkuta pia ni mwepesi wa kumshukuru Allah kwani Yeye, Allah, ndiye chanzo cha kila neema na kila wema ambao mtu amefanyiwa. Tuwe wepesi wa kushukuru kwa neema yoyote kwani asiyeshukuru kwa kichache alichopewa hata akipewa kingi hawezi kushukuru.

Pepo hupatikana kwa matendo mema

Pepo haipatikani isipokuwa kwa kudumisha matendo mema. Kwa kulijua hilo, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimuamrisha Rabi’ah akithirishe sala. Hii ni dalili juu ya ubora na fadhila za kukithirisha sala za sunna.

Allah ametuwekea sala za sunna katika nyakati mbalimbali za usiku na mchana ili tujikurubishe kwake katika nyakati zote. Katika hadith iliyosimuliwa na Thāubān (Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema “Tambueni kuwa matendo yenu yaliyo na ubora kabisa ni sala.” [Ibn Majah].

Hivyo basi, ni vema kufuata usia huu ambao hautamnufaisha Rabi’ah peke yake bali umma wote. Nafasi tuliyopewa ni kukithirisha ibada ya sala za sunna ili tuweze kuwa karibu na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button