Dkt Naik aisifu SGR, azuru Imaan Media
MHADHIRI wa kimataifa Dkt Zakir Naik amefanya ziara katika vyombo vya habari vya Imaan vilivyo chini ya taasisi ya The Islamic Foundation ya Mjini Morogoro.
Dkt Naik alifika mkoani Morogoro akitokea jijini Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa treni ya kisasa majira ya asubuhi na moja kwa moja alikwenda katika studio za Imaan, akiwa ameambatana na mwenyeji wake mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Aref Nahdi.
Wengine waliombatana na Naik katika msafara huo ni sheikh Arif Surya Mkurugenzi wa DA’AWAH na TABLIGH,Ofisi ya Mufti Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Taifa Sheikh Arif Tanzania, ambapo walijionea maeneo mbalimbali ya ofisi.
Mhadhiri huyo wa kimataifa alijionea studio za Redio Imaan zilivyokuwa za kisasa na namna zinavyorusha matangazo yake ya vipindi mbalimbali kama mawaidha, habari na vingine vya kijamii.
Dkt Naik alifanya mazungumzo na Mwenyekiti Nahdi ambaye alimpa mgeni huyo maelezo ya jinsi taasisi ya The Islamic Foundation inavyofanya kazi zake ikiwemo ujenzi wa shule, misikiti, madrasa, ujenzi wa vituo vya afya na vya dini, uchimbaji wa visima katika maeneo yenye uhitaji na ugawaji wa misaada kwa watu wasio na uwezo. Dkt Naik pia alitembelea msikiti Ghaith unaojengwa na taasisi hiyo ya The Islamic Foundation mjini Morogoro ambapo utagharimu takribani zaidi ya Sh7 bilioni hadi kukamilika kwake na utakuwa na uwezo wa kuchukua waumini zaidi ya 3000 kwa wakati mmoja. Msikiti huu unatajwa kuwa utakuwa mkubwa zaidi katika kanda wa Afrika Mashariki na Kati.