
Ebola yaibuka upya Uganda
Wizara ya Afya ya Uganda ilitangaza mlipuko wa Ebola siku ya Alhamisi baada ya muuguzi mwenye umri wa miaka 32 anayefanya kazi katika Hospitali ya Mulago jijini Kampala kufariki dunia kwa ugonjwa huo, ikiwa ni mlipuko wa nane wa ugonjwa huo hatari katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Shirika la Afya Duniani limesema linafanya kazi kwa karibu na mamlaka ya afya ya Uganda kuanzisha upya mfumo thabiti wa ufuatiliaji na udhibiti wa wagonjwa, uhamasishaji wa jamii na mawasiliano ya hatari katika kukabiliana na mlipuko.
Jumla ya watu 45 wametambuliwa na kutengwa, wakiwemo wahudumu 30 wa afya na wagonjwa katika Hospitali ya Mulago, wanafamilia 11 wa marehemu na wahudumu wanne wa afya katika Hospitali ya Kiislamu ya Saidina Abubakar iliyopo Matugga, kwa mujibu wa Diana Atwine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
“Chanjo ya watu wote waliotangamana na marehemu dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Ebola inapaswa kuanza mara moja. Dozi zilizopo za chanjo ya Ebola zinapewa kipaumbele kwa watu waliotangamana na marehemu na wahudumu wa afya,” Atwine aliwaambia waandishi wa habari mjini Kampala siku ya Alhamisi.
Virusi vya Ebola vinaambukiza sana na husababisha dalili mbalimbali, ikiwa ni pamoja na homa, kutapika, kuhara, maumivu ya jumla au kujisikia udhaifu, na mara nyingi, kutokwa na damu ndani au nje. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kiwango cha vifo kwa wale wanaoambukizwa Ebola ni kati ya 50% na 89% kulingana na aina ndogo ya virusi.