
Vikwazo tele kwa Waislamu wa Uyghur kusafiri nje ya China
Serikali ya China imeweka vikwazo vikali zaidi kwa jamii ya Waislamu wa Uyghur wanaoishi katika jimbo la Xinjiang ikilenga kuwanyima haki yao ya kusafiri nje ya nchi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch (HRW) iliyonukuliwa na shirika la AsiaNews Waislamu wa Uyghur wanakabiliwa na masharti magumu ya kuwa na mdhamini wa safari au kushikiliwa kwa familia zao kama dhamana ya kurudi kwao.
Aidha, hawaruhusiwi kuwa na mawasiliano na wanaharakati wa Kiislamu waliopo nje ya nchi.
Ripoti hiyo pia inabainisha kuwa China inazuia Wauyghur kwenda katika mataifa yenye idadi kubwa ya Waislamu, kama Uturuki na Kazakhstan hata kama ni kibiashara.
Kwa waliokimbilia nje ya nchi na kutaka kurejea nyumbani, China inawalazimisha kutoa maelezo ya kina kuhusu madhumuni ya safari yao na kuwataka kuwa na mwaliko rasmi kutoka kwa familia zao.
Mbali na hayo, ripoti ya HRW inasema kuwa watu wa Uyghur wanaorudi kutoka safari zao, huhojiwa vikali na mamlaka za China, wakilazimishwa kueleza kila mtu waliyekutana naye na mazungumzo waliyofanya.
Baadhi ya wanaorudi wamekiri kuwa wanajihadhari hata kula katika mikahawa ya Kiuyghur ili kuepuka kufuatiliwa mazungumzo yao na vyombo vya usalama vya China.
Ripoti inaeleza hata kwa wale wanaohitaji viza kuingia China, mchakato wa maombi yao unachukua hadi miezi sita.
Kwa miaka mingi, China imekuwa ikilaumiwa kwa kuendesha kampeni kali ya mateso, ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya Waislamu wa Uyghur kwa kuwakamata kiholela na kuwafunga katika kambi za “marekebisho ya kitabia,” ambazo serikali inazielezea kama vituo vya mafunzo.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa tangu 2017, zaidi ya Waislamu milioni moja, hasa wa Uyghur, wamefungwa katika vituo hivi kwa kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi. Hata hivyo, China inakanusha madai haya, ikiyaita “uongo wa karne.”
Ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu inatoa wito kwa China kuheshimu haki za Uyghur za kusafiri na kuwasiliana na familia zao. Yalkun Uluyol, mtafiti wa HRW kuhusu China, amesema: “Haki ya kuwasiliana au kutembelea familia haipaswi kuwa fursa maalum kwa wachache, bali ni haki ya msingi ambayo serikali ya China inapaswa kuheshimu.” Wakati hayo yakiendelea, jumuiya ya kimataifa imeendelea kushinikiza China kusitisha ukandamizaji dhidi ya jamii hiyo.