Kimataifa

Serikali, Waislamu Uingereza wabishania tafsiri ya  ‘Islamophobia’

Baraza Kuu la Waislamu wa Uingereza (MCB) limeitaka serikali ya Uingereza kutambua rasmi tafsiri ya ‘Islamophobia’ iliyopendekezwa mwaka 2018 na Kikundi cha Wabunge wa Vyama Vyote (APPG).

Katika maelezo yake ya kuelezea dhana ya Uislamofobia, APPG ilisema: “Islamophobia is rooted in racism and is a type of racism that targets expressions of Muslimness or perceived Muslimness.”

Kwa Kiswahili kisicho rasmi, tafsiri hiyo inasema: Uislamofobia una asili katika ubaguzi wa rangi na ni aina ya ubaguzi wa rangi unaolenga kila kitu kinachoelezea/kuwasilisha Uislamu au kinachodhaniwa kuwasilisha Uislamu.

Kwa mujibu wa MCB, Serikali inaonesha dalili za kupinga tafsiri hiyo na badala yake kupendekeza kuanzishwa baraza jipya litakalotoa maana ya dhana hiyo ambayo msingi wake ni chuki dhidi ya Waislamu.

MCB, kupitia taarifa yake kwa Middle East Eye (MEE), ilisema: “Tunakaribisha juhudi za serikali za kukabiliana na Uislamofoboa, lakini badala ya kubuni upya mchakato, tunawahimiza wakubali tafsiri ya APPG.”

Kwa mujibu wa gazeti la The Telegraph, serikali inapanga kuunda baraza la watu 16 ndani ya Wizara ya Makazi, Jamii na Serikali za Mitaa litakaloshauriana kuhusu namna ya kupambana na chuki dhidi ya Waislamu na kutoa tafsiri isiyo na nguvu za kisheria kuhusu ubaguzi dhidi ya Waislamu.

Hatua hii imeibua maswali kuhusu dhamira halisi ya serikali, hasa baada ya utawala wa awali wa chama cha Conservative kutambua rasmi tafsiri ya chuki dhidi ya Wayahudi (antisemitism) lakini kushindwa kufanya hivyo kwa Uislamofobia.

Wakati chama cha Labour kilichokuwa upinzani kilikubali tafsiri ya APPG, serikali ya Conservative ilikataa na kudai kuwa inaweza kuzuia uhuru wa kujadili dini ya Uislamu.

Lakini sasa, chama cha Labour  nacho, kwa mshangao wa wengi, wamegeuka na kumeonesha  kuwa licha ya matarajio ya wengi, inajiondoa katika kuidhinisha tafsiri ya APPG na badala yake inataka kuibadilisha au kuandaa mpya.

Waziri wa Masuala ya Imani, Lord Wajid Khan, hakukosa visingizio aliposema kuwa tafsiri ya APPG, haiko sambamba na Sheria ya Usawa ya 2010, ambayo inatafsiri ubaguzi wa rangi kwa misingi ya rangi, utaifa, na asili ya kikabila.

Baraza Kuu la Waislamu wa Uingereza limeonya kuwa vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu vinaongezeka na vinaathiri jamii kwa ujumla. “Ghasia tulizoshuhudia mwaka jana kufuatia machafuko ya Southport na chuki inayoendelea dhidi ya Waislamu, zinaonyesha wazi kuwa changamoto hii ni halisi,” ilisema taarifa ya MCB.

“Pamoja na mashambulizi dhidi ya Waislamu, wale wasio na nia ya kuwalinda Waislamu, wanadai kuwa jitihada hizi ni njia ya kuanzisha sheria za kukataza matusi kwa Uislamu kwa siri,” iliongeza taarifa hiyo. Haya yanatokea katika kipindi ambacho machafuko yaliyotokea majira ya joto 2024 yaliyosababishwa na vikundi vya mrengo wa kulia, yamedhihirisha kwa mara nyingine madhara ya Uislamofobia.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button