Hapa na Pale

Serikali yazionya Hospitali zinazozuia maiti kisa deni

Serikali imesema itaanza kuchukua hatua kali kwa madaktari wanaozuia maiti kuchukuliwa na ndugu zao baada ya kushindwa kulipa gharama za matibabu, kinyume na maelekezo ya serikali.

Kadhalika, serikali imetoa maelekezo kwa hospitali binafsi na za umma kuhakikisha wanatoa kwanza huduma kwa wagonjwa na si kuweka maslahi ya fedha mbele.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, lililokuwa likiuliza serikali inatoa tamko gani la wazi kwa wananchi wanaoshindwa kupata mwili baada ya kushindwa kulipa deni.

Akijibu swali hilo, Dkt. Mollel alisema serikali imekuwa ikipokea malalamiko ya ndugu kuchelewa kupewa miili kwa kushindwa kulipa madeni. Amesema, serikali itachukua hatua kwa daktari atakayesababisha usumbufu kama huo, ikiwa mwananchi anafuata taratibu zinazohitajika.

Aliongeza kuwa serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia Waraka Namba Moja wa Mwaka 2021 wa kutozuia mwili na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili. Aidha, Dkt. Mollel aliwaomba wabunge kuwaelimisha wananchi wao kufuata taratibu watakazopewa pale wanaposhindwa kulipa deni.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button