Habari

Tuzo za Qur’an za dunia mwaka huu kabla Ramadhan

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tanzania, Sheikh Othman Kaporo amesema kwa mara ya kwanza tuzo za Qur’an duniani zitafanyika kabla ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kwamba wamefanikiwa kupata wadhamini wapya kutoka serikali ya Saudia Arabia.

Mbali ya mabadiliko hayo machache, pia mtaalam huyo amesema tuzo hizo kwa mara ya kwanza zitahudhuriwa na mmoja wa Maimamu kutoka Misikiti Mitakatifu ya Makka na Madina na kwamba kiongozi huyo wa kiimani anatarajiwa kufika mapema kabla ya Februari 23, 2025 ambapo tuzo zitatolewa.

Sheikh Kaporo ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika hafla maalum ya kuzindua tuzo hizo zinazotarajiwa kufanyika Jumapili, Februari 23, 2025 katika uwanja wa Benjamini Mkapa kuanzia saa mbili asubuhi.

“Ugeni wa Imam kutoka moja ya misikiti hii unatarajiwa kunogesha tuzo hizi. Nawashauri wapenzi wa Qur’an wajitokeze kwa wingi katika Uwanja wa Taifa kuona tuzo hizi zinavyotolewa,” alisema.

Pia, alisema mafanikio ya kupata viongozi wa aina ya imam wa misikiti mikubwa duniani ni kutokana na kazi kubwa inayofanywa na waandaji wa mashindano ya Qur’an hapa nchini. Watu wengi wanaona huko duniani na wanavutiwa na kazi inayofanyika hapa Tanzania.

Kuhusu zawadi, Sheikh Kaporo amesema bado ni siri, huku akiweka wazi kuwa kutakuwa na tiketi tano za ufadhili wa Hijja daraja la kwanza, ambazo zitatolewa kwa watu watakaowahi kufika uwanjani, akitaja kuwa watu hao watano watakuwa ni wageni wa Mfalme.

“Kutakuwa na zawadi kwa washindani 25 watakaoshiriki lakini pia Mfalme wa Saudi Arabia naye ametoa ofa kugharamia safari ya kwenda kuhiji miongoni mwa wale watakaofika uwanjani,” alisema.

Kwa mujibu wa Sheikh Kaporo, taarifa zaidi kuhusu wageni wengine mashuhuhuri watakaohudhuria mashindano hayo zitazidi kutolewa kadri tarehe ya mashindano inavyozidi kukaribia.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uzinduzi, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amepongeza kazi inayofanywa na waandaji wa tuzo za Kimataifa za Qur’an Tukufu kwa kuendelea kuwa makini, wabunifu na endelevu, akisema mashindano hayo yameipa Tanzania heshima kubwa kimataifa.

Vilevile, Ulega alisifu uamuzi wa kumualika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo, akisema kiongozi huyo wa nchi ni ishara ya kuhimiza maadili mema katika jamii.

“Siyo siri kwamba Rais Samia ni alama ya maadili mema katika jamii yetu, ambayo inakabiliwa na tatizo kubwa la mmomonyoko wa maadili. Mmefanya jambo sahihi kumwalika, kwani watu wengi wanaomfuatilia watapata fursa ya kusikiliza mawaidha ya kumuenzi Mwenyezi Mungu,” alisema Ulega.

Tuzo za Qur’an chini ya Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tanzania zimekuwa zikifanyika kwa zaidi ya miaka 33 sasa, zikianza kama za kitaifa na baadae kuvuka mipaka. Ukiacha kuienzi Qur’an, tuzo hizi pia zimeletea taifa heshima na kuchangia shughuli za kiuchumi kutokana ujio wa wageni. Mbali na faida hiyo, pia mashindano haya na mengine ya Qur’an kwa ujumla wake yamechangia kusimamisha maadili hususan miongoni mwa vijana. Katika mashindano hayo, zawadi mbali hutolewa kwa lengo la kujenga hamasa kwa vijana kupenda kukisoma kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button