Habari

Azam Halal Pesayaingia sokonikwa kishindo

  • Yatajwa suluhisho usimamizi wa fedha misikitini

KWA WALE ambao wamekuwa na wasiwasi juu ya uhalali wa gawio wanalotumiwa na makampuni ya simu yanayotoa huduma za pochi za kidijitali (digital/mobile wallets) hawana sababu tena ya kuishi kwa mashaka ya kuingizwa kwenye miamala ya dhambi baada ya huduma mpya kuingia sokoni inayozingatia Shariah ya Kiislamu ambayo inayokataza riba.

Aidha, huduma hii inaweza kuwa sehemu ya suluhisho la migogoro ya kifedha misikitini kwani ina ubunifu unaolazimisha uwazi, nidhamu na udhibiti wa matumizi. Azam Halal Pesa, iliyopata ridhaa ya Ofisi ya Mufti na pia kibali cha Benki Kuu ya Tanzania, ilizinduliwa wiki hii visiwani Zanzibar na inategewa kupanua wigo wa uchaguzi kwa wateja wanaohifadhi pesa kwenye pochi za kidijitali.

Akieleza kwa nini Azam Pesa imekuja na huduma hii, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Azam Pesa, sheikh Khalfan Abdallah, amesema pochi za kidijitali ni moja uvumbuzi mkubwa katika huduma za kifedha lakini kilichokosekana, licha ya kuwepo mahitaji, ni kuweko kwa pochi la kidijtali linalozingatia maadili ya Kiislamu (halal digital wallet).

Akielezea nafasi ya pochi za kidigitali katika maisha ya Watanzania, Sheikh Abdallah alinukuu utafiti wa taasisi ya Finscope Tanzania ambao ulionesha kuwa asilimia 72 ya Watanzania huweka fedha kwenye simu, ukilinganisha na asilimia 22 wanaoweka fedha benki.

“Na katika hizi pochi za kidijitali, kwa miaka yote hiyo, kumekuwa na hilo pengo sokoni la ukosefu wa huduma ambazo Waislamu na wananchi wote wanaweza kutumia wakiwa na faraja na amani katika nafsi zao (wakijua) kwamba fedha zao ziko katika kusimamiwa kwa misingi ya uadilifu na inayofungamana na imani zao,” alisema sheikh Abdallah.

Aliongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa mahitaji hayo, Azam Pesa imekuwa ya kwanza kuja na ubunifu huo wa kuleta pochi la kidijitali la halal. Akiitambulisha Halal Azam Pesa, mjumbe huyo wa bodi alisema: “Napenda kuitambulisha kwenu bidhaa hii inayofungamana na maadili ya dini ya Kiislamu ambayo vilevile inafungamana na maadili ya uadilifu na ujumuishi kwa watu wote.”

Akifafanua tofauti ya Halal Azam Pesa na huduma za pochi za kidijitali ya kawaida, alisema fedha zitakazohifadhiwa katika pochi hiyo zitatunzwa kwa misingi ya sharia na uadilifu na kipato kitakachogawiwa kitatokana na uwekezaji unaofuata misingi ya kisheria na sio riba, kama ilivyo kwa mitandao mingine.

Faida nyingine ambayo sheikh Abdallah ameitaja kuwa mtu ataipata kwa kuweka fedha katika Halal Azam Pesa, atakuwa ameunga mkono uwekezaji wa kimaadili ambayo inachangia katika ukuaji wa uchumi na ustawi na maendeleo ya watu.

Suluhisho usimamizi wa fedha misikitini

Naye Mkurugenzi Mtendaji, Azam Pesa, Ibrahim Malando amesema moja kati ya ubunifu wa kipekee unaoetwa na Halal Azam Pesa ni kuwezesha Waumini katika misikiti kuchangia pesa kwenye namba ya Lipa Hapa ya msikiti.

Kupitia idhini ya viongozi wetu wa misikiti mbalimbali, tutawapatia suluhisho rahisi na la kimaadili ambalo watumiaji wanaweza kutumia lipa namba ya misikiti kuchangia moja kwa moja kwenye akaunti zetu.

“Huduma ya lipa hapa ya Azam Pesa inawaruhusu Waumini kutoa sadaka au michango yoyote wanayobarikiwa kwa njia ya haraka, salama, uwazi. Pesa zote zitakusanywa na kupitia huduma hii zinaweza kutumika kwa njia mbalimbali,” alisema Malando.

Akifafanua zaidi, Malando alisema viongozi na Waumini wanaweza kuwa na chaguo la aidha kukusanya pesa zote ambazo Waumini watachanga na kuzipeleka kwenye akaunti ya benki moja kwa moja pasipo mtu yoyote kuwa na uwezo wa kutoa hizo pesa au msikiti wenyewe unaweza kuamua huduma gani pesa iliyochangwa inaweza kutumika kulipia.

“Kwa mfano, msikiti unaweza kuchagua pesa zote zilizochangwa zitumike kununua umeme, Azam Pesa tuna huo uwezo wa kufunga huduma nyingine zote kwenye hiyo akaunti na kuacha hiyo akaunti kuwa na uwezo wa kununua umeme peke yake,” alisema Mkurugenzi Malando.

Alisema ingawa mfano alioutoa ni wa umeme, mfumo huo wa kudhibiti matumizi, kwa mujibu wa matakwa ya msikiti, unaweza kutumika kwa huduma nyingine pia ikiwemo maji na kadhalika. Aidha, Malando alisema, Azam Pesa ina uwezo wa kuzuia fedha kuhamishiwa akaunti nyingine yoyote, iwapo itaamuliwa hivyo na uongozi wa msikiti.

Malando alisema faida kubwa ya mfumo huo wa lipa hapa kutumika kwa msikiti ni kuleta uwazi na kujenga imani kwa watu ya kuchangia bila ya wasiwasi wa fedha zao kufunjwa.

Licha ya faida za kimaadili, Malando amejinasibu kuwa Azam Pesa ina unafuu mkubwa katika makato na kwamba kuhamisha fedha kati ya akaunti ya Azam Pesa kwenda Azam Pesa ni bure, yaani hakuna makato kabisa.

Sambamba na hayo, Azam Pesa, ikiwa ni kampuni halisi ya Kitanzania, ina huduma zote za malipo mbalimbali zinazopatikana kwa watoa huduma nyingine ikiwemo malipo ya Luku, huduma ya maji, muda wa maongezi, tiketi za ndege na kadhalika.

Uzinduzi wa huduma hiyo ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif ambaye alimshukuru Mwenyekiti wa Makampuni ya Bakhresa akimtaja kuwa biashara zake zimegusa kila nyanja ya maisha ya Mtanzania.

Sharif licha ya kuahidi kuiunga mkono huduma hiyo kwa kujiunga nayo yeye binafsi, pia alihimiza wananchi, hususan Waislamu, ambao riba kwao ni haramu kujisajili ili kufaidika duniani na akhera.

Wadau kadhaa waliotoa maoni yao kuhusu ujio wa Azam Pesa wamesema licha ya uchanga wao, Azam Pesa, wameonesha ukomavu mkubwa katika nyanja ya pochi za kidijitali huu wengine wakitaja kuwa kinachotakiwa ni kuongeza hamasa na kutoa elimu kwa umma waone thamani ya kutumia huduma hii.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button