
Ajali Morogoro
Lori la mafuta lililokuwa likisafirisha bidhaa hiyo kutoka Dar es Salaam limeanguka kwenye barabara kuu ya Morogoro Dar es salaam, katika eneo la Mzambarauni Manispaa ya Morogoro, na kuanza kumwaga mafuta.
Tukio hilo limeleta taharuki kubwa, ambapo wananchi wamekusanyika kwa wingi eneo hilo, wakijaribu kuchota mafuta yaliyomwagika kutoka kwenye lori,Hali hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa na kuleta hatari ya moto kwa kuwa mafuta ni bidhaa inayoweza kuchochea moto kwa urahisi.
Jeshi la Polisi limelazimika kufika eneo la tukio na kuingilia kati ili kulinda usalama wa wananchi na kuepusha maafa yanayoweza kutokea.
Polisi wamewafukuza wananchi kutoka kwenye eneo hilo kwa kuwa walikuwa katika hatari kubwa kutokana na uwepo wa mafuta hayo.
Hali ya taharuki ilidumu kwa muda, lakini Jeshi la Polisi liliweza kudhibiti hali hiyo kwa kufunga maeneo ya tukio ili kulinda usalama wa raia.






