MAIMAMU na Walinganiaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation ya Mjini Morogoro,wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani ya nchi iliyopo, isitoweke kwani jamii inawasikiliza na kuwaheshimu viongozi wa dini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala, alipokuwa mgeni rasmi katika kilele cha semina ya Maimamu na Walinganiaji wa Taasisi hiyo ya The Islamic Foundation.
Semina hiyo imewakutanisha Maimamu na walinganiaji kutoka nchi nzima iliyofanyika kwa siku mbili, tarehe 25 na 26.02.2025 katika Masjid Noorah uliopo Msamvu Manispaa ya Morogoro.
Mgeni Rasmi Mussa Kilakala amesema kuwa viongozi hao wa dini wana nafasi kubwa kuwalingania waumini wao katika masuala mazima ya kulinda amani, kutii mamlaka na kuheshimu taratibu za nchi kama katika mafundisho ya dini ya uislamu yanavyoelekeza.
Aidha Mgeni Rasmi Mussa Kilakala ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi kujitokeza katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura litakalo anza tarehe mosi mwezi machi mwaka huu.
Na hapa mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation Aref Nahdi ametilia mkazo kwa maimamu hao kuendelea kuhubiri amani katika nyumba za ibada na kujitokeza katika uchaguzi mkuu wan chi wa hapo baadaye mwaka huu kwenda kuchagua viongozi wenye imani na maono ya kuwatumikia wananchi.
Sheikh Ibrahim Twaha Ibrahim ni Mkurugenzi wa Taasisi ya The Islamic Foundation ameipongeza idara ya Da’awa kwa kuandaa semina hiyo yenye kuwakumbusha nafasi zao maimamu katika kuwaongoza waumini wao, Huku Mkurugenzi wa Idara ya Da’wa Sheikh Ismail Rajab Kundya akitoa shukrani kwa Taasisi kwa maandalizi mazuri ya kuwapiga msasa maimamu.
Kwa upande wake mkufunzi wa semina hiyo Sheikh Mikidadi Lipena amesema kuwa uislamu umekemea na kukataza maandamano na vichochezi vyenye lengo la kuvuruga amani kwani vitu hivyo vitaibua machafuko.
Hata hivyo Mlinganiaji wa Dini Tukufu ya Kiislamu Sheikh Hassan Ahmed amewataka maimamu hao kuendelea kulingania waumini wao kwani mbora wetu ni yule mwenye kuwanufaisha watu.
Wanufaika wa semina hiyo ambao ni maimamu na walinganaji wa dini tukufu ya kiislamu wakatoa ahadi ya kwenda kuwalingania waumini wao suala zima la kulinda amani na kutojiingiza katika vishawishi vyovyote vya kuleta vurugu hususani katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu hapo baadaye.
Jumla ya wanasemina na walinganiaji wote waliohudhuria mafunzo hayo ya semina ni 105 kutoka Tanzania bara na Visiwani na imeandaliwa na idara ya Da’awa chini ya Taasisi ya The Islamic Foundation ya Mjini Morogoro.