Events

Ujio wa Dkt. Naik ni fursa kwa wahadhiri wa ndani kujifunza

Disemba 30, 2024, ‘InshaAllah’ Tanzania itapokea ugeni wa mhubiri na mlinganiaji maarufu wa dini ya Kiislamu duniani, Dkt. Zakir Abdul Karim Naik sambamba na mwanawe, Sheikh Fariq Naik.

Dkt. Naik na Sheikh Fariq watawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume tayari kwa mihadhara mitatu mikubwa, mmoja Zanzibar na miwili jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo ya kida’awah inayolenga kuzungumzia amani na imani, Dkt. Naik anatarajiwa kukonga nyoyo na kugusa hisia za watu wengi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufafanua masuala mbalimbali kuhusu Uislamu na Dini Linganishi, lakini pia kujibu maswali ya papo kwa papo kwa ufasaha.

Dkt. Naik, ambaye anazuru Tanzania kwa mara ya kwanza, ujio wake unatajwa kuwa fursa muhimu kwa walinganiaji wa hapa nchini kukuza uelewa wao katika nyanja ya da’awah.

Ikumbukwe kwamba, miaka kadhaa iliyopita baadhi ya wahubiri wa Kiislamu hapa nchini walijikuta wakiingia matatani kwa kukamatwa na vyombo vya dola kwa kile kilichotajwa kuwa ni  ‘kukashifu’ imani za watu wengine.

Hali hii ilichochewa zaidi na kitendo cha kuchambua maandiko ya Biblia, hususani zile ibara zenye utata pasipo kutumia lugha laini na upole, jambo ambalo lilipelekea mihadhara ya dini linganishi kupigwa marufuku.

Kutokana na yaliyojitokeza huko nyuma, ni muhimu kwa walinganiaji wa Kiislamu kurejea historia ya da’awah kwa sababu, hali halisi ya ulinganiaji imekuwa ikibadilika kulingana na mifumo ya nchi, mitazamo na imani za watu.

Mhubiri wa Kiislamu anatakiwa amtakasie Allah nia na atumie hoja thabiti, ushahidi wa kimaandiko na kutumia lugha ya staha katika kulingania kwake, kama alivyoagiza Allah:

…enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: kwamba tusimuabudu yeyote isipokuwa Allah, wala tusimshirikishe na chochote, na wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa waola badala ya Allah. Wakikengeuka, basi semeni: Shuhudieni kwamba sisi ni Waislamu.

[Qur’an, 3:64].

Lakini pia tusisahau kuwa msingi wa kumlingania mwingine ni huruma na upole. Allah alimwambia Mtume Muhammad (rehema na amani imshukie):

Na hatukukutuma (Muhammad) ila uwe rehema kwa walimwengu wote.

[Qur’an, 21:107].

Hizi ni mbinu muhimu ambazo Dkt. Naik amekuwa akizitumia katika ulinganiaji wake. Kwa hiyo, tutakapokuwa tunafuatilia mihadhara ya Dkt. Naik pale Zanzibar na Dar es Salaam, ni jambo jema na la kheri kwa walinganiaji wetu  kujifunza kutoka kwake mbinu/ njia hizi.

Tunalisisitiza hili kwa sababu, mbinu hizi ndizo zimemuwezesha kwa idhini ya Allah kusilimisha maelfu ya watu nchini mwake (India), barani Ulaya na maeneo mengine duniani.

Mafanikio hayo kwa mujibu wa maelezo katika tovuti yake, yametokana na kanuni alizojiwekea katika maisha yake na kupitia kipaji alichonacho, kwamba kila sehemu anayotembelea na kufanya mihadhara anahakikisha anasilimisha watu kupitia hoja mbalimbali za kwenye Qur’an na Biblia. Mwisho tunawahimiza Watanzania – Waislamu na wasio Waislamu – kujitokeza kwa wingi kusikiliza ujumbe utakaotolewa na Dkt. Zakir Naik na Sheikh Fariq katika mhadhara utakaofanyika Disemba 31 kwenye msikiti wa Jaamiu Zinjibar Mazizini, mhadhara wa tarehe 2 Januari pale Diamond Jubilee na ule wa kilele katika uwanja wa Benjamin Mkapa mnamo Januari 5, 2025.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button